Nakusalimu katika jina la Bwana wetu Yesu Kristo aliye hai, siku nyingine tena njema kabisa Bwana ametupa kibali cha kuiona. Sifa na utukufu tumrudishie yeye Bwana mwenza wa yote, sio kila aliyetamani awepo leo ameweza kufikia.
Kila mmoja anapaswa kuwa na juhudi zake zote kuweza kuisoma biblia yote, na kurudia siku hadi siku, tena kurudiarudia tu haitoshi. Inapaswa kutafakari zaidi yale unayojifunza, usipopata muda wa kutafakari yapo mengi sana hayataweza kukuingia vizuri moyoni.
Tunapopambana kuisoma biblia na kuhakikisha tumeanza mwanzo mpaka ufunuo, zipo mbinu nyingi kila mmoja anapambana kuhakikisha amefikia lengo hilo. Changamoto nyingine inakuja pale mtu anakwambia ameisoma biblia yote ila hafanani kabisa na kile anakwambia, maana yake huyu mtu alisoma tu bila kupata muda wa kutafakari au alisoma tu bila kumruhusu Roho Mtakatifu au alivyosoma na kuimaliza biblia aliishia hapo hakuendelea tena kujifunza.
Wapo wengine pia wanaanza leo kusoma Neno la Mungu, wanakuwa na kasi kubwa mno, kiasi kwamba ukiwatazama unawapenda wenyewe. Mtu huyu anaweza kukusomea sura 10 kwa siku, kiu yake kubwa anataka kuwa miongoni mwa watu walioimaliza kuisoma biblia.
Mapambano haya yote ni mazuri sana kwa upande mwingine ikiwa tu huyu mtu atajitambua anachofanya. Maana si wote tunaweza kufanana na si wote tunaweza kufanana kazi tunazofanya, wapo watu muda wao mwingi wanautumia/wanautenga kwa ajili ya Mungu na shughuli zake zingine zikawa zinaenda vizuri tu.
Shida inayokuja Kwenye kundi hili la kutaka kuisoma biblia yote kwa muda mfupi, wengi sana huwa wanaishia njiani, wengi niliowahi kuwaona wakifanya hili. Hawakuweza kuendelea na mpango wa kusoma Neno la Mungu, nini kiliwakuta? Wengine walichokea njiani, wengine mpaka leo wanasema nitaanza tena kesho, wengine wameacha tu.
Nikueleze kwamba, kuisoma biblia yote kwa muda mfupi uimalize, ni kujidanganya na kujitafutia kujivunja moyo mwenyewe. Kama utakimbizana na mbio za kufuta kabisa zoezi la kusoma Neno la Mungu kwa muda mfupi, nakueleza kitu nilicho na uzoefu nacho, hutofikia kiwango kizuri cha kukua kiroho.
Kwanini usikue kiroho na wakati umeishaimaliza kuisoma biblia yote? Ni kwa sababu kuna siku utafika utaanza kuhangaika kukimbizana na sura za kitabu na kuna siku unaweza kusoma hata sura 20 kwa pamoja. Kukimbizana huku kutakuondoa kwenye kitu kinaitwa kutafakari, ule muda wa kuipa akili yako itafakari yale unajifunza haitakuwepo kwa sababu inawaza kuimaliza mwanzo, kutoka, Walawi, Hesabu na vitabu vingine vinavyoendelea mbele.
Ila ukijenga utaratibu wa kutaka kuelewa unachosoma, itakufanya uwe mtulivu na mwenye nidhamu ya kwenda hatua kwa hatua. Tena bila kuhangaika kukimbiza upepo umalize biblia nzima, huku unaachwa bado upo vile vile.
Kumbuka biblia imebeba maisha yako yote, nikiwa na maana ya maisha ya kiroho na kimwili. Hasa kiroho, maana matokeo yote ya mwilini yawe mazuri au yawe mabaya, yalianzia katika ulimwengu wa roho. Ukifanikiwa kukua kiroho na ukakomaa vizuri, maisha yako ya kimwili yatakuwa rahisi sana kuyaendesha.
Kitu kilichobeba maisha yako, kwa maana nyingine tunaweza kusema kitu kilichobeba uhai wako. Hakiwezi kurahishwa kihiivyo. Tunapaswa kukipa uzito na kujenga umakini na nidhamu ya kuweza kusimama vizuri, kuhakikisha tunaenda hatua ambazo hatutafika siku tukachokea njiani.
Nakusihi sana, achana na habari za kukimbiza upepo, yaani acha kuhangaika kutaka kuimaliza biblia kwa muda mfupi. Vitabu vingine unaweza kufanya hivyo maana venyewe vimebeba vitu vichache sana, tena kinaweza kugusa kipande kidogo sana cha maisha. Kama unauwezo wa kukisoma hicho kitabu cha kawaida siku moja, unaweza kufanya hivyo ila sio kwa biblia.
Kubali kwenda hatua kwa hatua, narudia tena ondoa fikira za kusoma Neno la Mungu haraka haraka ili umalize. Tafuta kuelewa, tafuta kile unasoma kinakaa kwenye fahamu zako, kutafuta hicho kutakupa nidhamu fulani ya ajabu sana. Maana wewe shida yako sio uonekane umesoma, shida yako ni kupata kitu ndani ya usomaji wako.
Bila shaka utakuwa umepata kitu cha kukusaidia katika safari yako ya usomaji wa Neno la Mungu, kile umekipata kifanyie kazi.
Mungu akubariki sana kwa kutoa muda wako kusoma ujumbe huu, endelea kutembelea Chapeo Ya Wokovu kwa masomo mengine mazuri zaidi.
Chapeo Ya Wokovu
Email: chapeo@chapeotz.com
Blog: www.chapeotz.com
WhatsApp: +255759808081.