Nakusalimu katika jina la Bwana wetu Yesu Kristo aliye hai, siku nyingine tena mpya kabisa Bwana ametupa kibali cha kuiona tena. Sifa na utukufu tumrudishie yeye Bwana mwenza wa yote kutupa kibali kingine cha kuiona leo.

Kuna mafundisho mengine sijui huwa yanaibuliwa wapi na sijui kama kuna mtu huwa anakaa chini na kufakari kuhusu ukweli wa jambo lenyewe. Nasema hivi kwa sababu nimesikia watu wengi sana wakisema nalala na biblia yangu pembeni mwa mto wangu, na mwingine anasema biblia ni kama mto wangu wa kulalia.

Dhana hii imepelekea wengi sana kuwa na imani kwamba kulala na biblia ni ulinzi tosha kwao, hatari kwao ni kwamba wanalala na biblia ila hawaisomi. Wanafikiri shetani atawaogopa kwa sababu wana biblia pembeni yao, wanafikiri wakiweka biblia pembeni yao itasimama kuwatetea.

Kumiliki silaha ya moto alafu uwe hujui namna ya kuitumia, siku adui zako wakijua kuwa silaha uliyonayo huna uwezo wa kuitumia, uwe na uhakika utapigwa tu. Sawa sawa na mtu awe na Bastola yake nzuri alafu maadui zake wakajua huwa anabeba kama urembo ila hana uwezo wa kupiga risasi hata moja.

Utaratibu huu wa kulala na biblia kama mlinzi wa usiku kucha, unaendelea kurithisha watoto wetu, wadogo zetu, na wale wanaotuzunguka. Badala yake tunapata kizazi kivivu/kizembe kisichopenda kujifunza Neno la Mungu, ukimweleza mtu kuhusu kusoma Neno la Mungu anatafuta kila sababu za kumkinga kubaki kuwa na utaratibu wake wa kutokusoma biblia.

Tunajenga kizazi ambacho watajua ni halali kulalia biblia kama mto, wakijua kufanya hivyo ni jambo zuri na la kuwakoa na nguvu za giza wakiwa wamelala. Maana mwingine atakuambia kama unasumbuliwa na nguvu za giza usiku, wewe lala na biblia pembeni yako.

Wengine wanaenda mbali zaidi, wanachukua ndulele wanaziweka pembeni mwa kitanda na biblia yao pembeni. Hiyo ni kama ulinzi kwao, ili nguvu za giza zikija zisiweze kuwadhuru na chochote.

Huu ni upangani wa kiwango cha juu sana, tumeanza kuingiza ibada ya sanamu majumbani mwetu kidogo kidogo pasipo kujua. Kama utakuwa na dhana ya kulala na biblia ndio mlinzi wako, nakwambia unajitengenezea ujinga kichwani. Maana utakuwa huna Neno la Mungu moyoni mwako zaidi ya kufikiri njia ya kukusaidia wewe ni kulala na biblia.

Huo ni upotoshaji kukufanya usisome Neno la Mungu lililo ndani ya biblia yako, biblia inaweza kumilikiwa na mtu yeyote yule, awe ameokoka awe hajaokoka. Mbaya zaidi unaweza kuwakuta akina babu huko kijijini wanazifanya karatasi za kusokotea sigara/bangi, nenda huko kijijini utajua ninayokueleza hapa. Hii ni kwa sababu hawajui hiyo ni silaha muhimu kwao, hawajui hicho kitabu kimebeba ahadi za maisha yao ya kiroho na kimwili, hawajui hicho kitabu ndio dira ya maisha yao.

Utasema haiwezekani kabisa mtu kusokota karatasi za biblia, kwani mtu akichukua mipini ya SMG akaifanya kuni, ugali hautaiva au nyama hazitaiva au wali hautaiva au maharage hayataiva? Bila shaka vyote vitaiva vizuri kabisa, wametumia nini? Wametumia mipini iliyotumika kama kiungo cha silaha.

Tumia Neno la Mungu likiwa moyoni mwako kukusaidia katika maisha yako, nasema hivi; kubeba biblia kwenye begi/mkoba wako, haikufanyi usimtende Mungu dhambi, ila ukiliweka Neno la Mungu moyoni mwako utaweza kuepuka kumtenda Mungu dhambi kwa sababu unajua Mungu anasema nini kuhusu hilo unalotaka kufanya.

Kuna mwingine hajanielewa ninachokisema hapa, nasema hivi; dawa ya mbu inaua kweli ila kwenda kununua chupa ya RUNGU/RISASI ukaja kuiweka ndani kwako. Haiwezi kuua mbu/mende wanaokusumbua ndani kwako, mpaka pale utakapoifungua na kuipuliza kila kona ya nyumba yako yenye wadudu.

Ikiwa Rungu/Risasi haiwezi kuua wadudu wanaokusumbua ndani bila kufuingua na kuipuliza, inawezekana vipi biblia kukusaidia kama hutoisoma na kujua kilichoahidiwa kwako. Utasema hiyo ni Rungu/Risasi, ila biblia ni tofauti kabisa.

Nakwambia unaweza kujaza fire extinguisher ndani kwako hata kama zipo 20, kama hutajua kuzitumia, ikitokea moto ukashika nyumba yako. Moto hautaogopa vifaa vyako vya kuzimia moto, moto utashika nyumba yako na ma fire extinguisher yapo humo ndani.

Sasa wewe unayelalia biblia bila kuisoma, ni kujidanganya na shetani ataendelea kukuchezea akili yako kila siku. Kwa sababu una kifaa kweli ambacho asiyejua chochote anaweza kukuogopa, ila akija kujua kuwa umeweka tu urembo atakuchapia na biblia yako hiyo hiyo.

Soma biblia, acha kuilalia, nakwambia unajihangaisha bure kama hutokuwa na utaratibu wa kuisoma biblia yako. Basi kama unaipenda sana biblia yako, isome kwanza kabla ya kuilalia alafu ukimaliza iweke kama mto wako.

Mungu akubariki sana kwa kutoa muda wako kusoma ujumbe huu, naamini kuna kitu umejifunza kupitia ujumbe huu. Endelea kutafakari zaidi uelewe kile nimekueleza ili uweze kuchukua hatua sitahiki.

Usiache kuendelea kutembelea ukurasa wetu wa Chapeo Ya Wokovu, kwa masomo mengine mazuri zaidi ya kukusaidia kukua na kuimarika katika usomaji wako wa Neno la Mungu.

Chapeo Ya Wokovu.

Email: chapeo@chapeotz.com

Blog: www.chapeotz.com

WhatsApp: +255759808081.