Nakusalimu katika jina la Bwana wetu Yesu Kristo aliye hai, Mungu ni mwema sana kwetu ametupa kibali kingine cha kuiona tena siku ya leo. Ni fursa kwetu kwenda kufanya yale yanayompendeza yeye Bwana, ili tuweze kumzalia matunda yaliyo mema.

Tunapo tafuta kujenga tabia njema na mpya ndani mwetu, tabia ambayo hatukuwa nayo hapo mwanzo. Lazima kuna gharama kubwa tutatumia ya kuweza kutengeneza hiyo tabia mpya unayoitamani kuwa nayo, ndani ya kutengeneza hiyo tabia kuna maumivu ndani yake.

Vizuri ukafahamu kujenga tabia njema na mpya ndani yako, kuna hitaji ujitoe kwa moyo wote bila kujali mazingira, na bila kujali hali inayokujia wakati mwingine kujiona unachofanya huoni matunda yake sana. Upaswa kuuona mwisho wa hilo jambo, picha unayopaswa kuwa nayo ni ile baada ya kuweka bidii utapata faida kubwa sana.

Pamoja na hayo yote unapaswa kuzingatia haya mambo mawili wakati unaanza kusoma Neno la Mungu, ili ikitokea jambo moja linataka kukurudisha nyuma. Uwe na uwezo wa kutumia jambo lingine kukuwezesha kuendelea na mpango wako wa kusoma Neno la Mungu.

Hizi njia mbili napenda uzijue na uzifanyie kazi, zipo nyingi na nitaendelea kukushirikisha pale ninapopata nafasi ya kufanya hivyo. Ila hizi za leo zichukulie kwa uzito wake na fanyia kazi yale maelekezo nitakayokupa hapa.

Njia ya kwanza ni Uhiari;kwanza kabisa unapaswa kujua suala la kusoma Neno la Mungu, ni jambo la hiari kwako kama mkristo. Uhiari huu ni kama kuokoka, kila mmoja aliamua kuokoka kwa hiari yake mwenyewe, haijalishi ulibanwa na tatizo fulani akaja mtu akakuambia mkabidhi Yesu maisha yako ukamua kuokoka kuepukana na mateso. Bado tutasema ni jambo la hiari kwa sababu ulikiri kwa kinywa chako mwenyewe kuwa Yesu Kristo ni Bwana na Mwokozi wa maisha yako.

Uhiari huu ukiuchukulia kwa mtazamo hasi, unaweza kuona hata usiposoma Neno la Mungu hakuna jambo utakosa, utaona usome usisome yote ni sawa. Lakini ukilichukulia hili suala la kusoma Neno la Mungu kwa mtazamo chanya, utaona uhiari unaozungumzwa hapa ni kama ule wa kuamua kuokoka.

Ukijenga uhiari ndani yako, upendo wa kile unachofanya utajengeka ndani yako na kujikuta unajisukuma mwenyewe kufanya bila kuambiwa na mtu yeyote fanya. Uhiari ukishaingia ndani yako, utafanya zaidi ya vile ulivyopanga kufanya yaani utaongeza uwezo wa ziada kuhakikisha umefanya vizuri.

Muda mwingine huu uhiari unafanya wengi wasione umhimu wa hili jambo, ndio maana nilikuambia hupaswi kuwa na mtazamo hasi kuhusu uhiari huu wa kusoma Neno la Mungu. Uhiari unaopaswa kuelewa hapa ni ule wa kukufanya ufurahie kusoma Neno la Mungu.

Sasa uhiari huu muda mwingine unapaswa kulazimishwa ili upaswe kuwa ndani ya mtu, wapo watu wanatamani na wanaona wapo tayari kusoma Neno la Mungu. Ila huo utayari wa kuwafanya wachukue hatua zinazopaswa kuchukua, wanakuwa wazito kuchukua hatua. Sasa ili mtu huyu achukue hatua tutapaswa kutumia njia ya pili.

Njia ya pili ni Ulazima;njia hii nimeiweka ya pili ili ile ya kwanza ikujengee msingi na kuona umhimu wa hili jambo, njia ya pili ambayo tunasema ulazima. Unapaswa kuitumia pale unapoona imeshindikana kufanya kwa uhiari, muda mwingine uhiari unatengenezwa kwa nguvu.

Ndio maana kama upo Chapeo Ya Wokovu whatsApp group,utakuwa shahidi wa hili kwa jinsi tunavyosukumana kwa nguvu kuhakikisha kila mmoja anaenda pamoja na wenzake. Baada ya muda huyu aliyekuwa anasukumwa, anajikuta hili jambo la usomaji wa maandiko Matakatifu linamwingia ndani ya moyo wake.

Jambo likipenya ndani ya moyo wa mtu na likajenga makazi ndani yake, uwe na uhakika hilo jambo halitakuwa la uhiari tena bali litakuwa la ulazima kwake. Pale atakapoona hawezi kutumia nguvu ya uhiari, atatumia nguvu ya ulazima maana anajua asipofanya hatakuwa na amani ndani ya moyo wake.

Kuhakikisha unajiwekea mizizi isiyoweza kung’olewa na changamoto yeyote unayokutana nayo, jenga tabia hii ya ulazima. Ulazima utakufanya ujisukume hata pale unapoona hujisikii kufanya, ulazima utakufanya uwasikilize wengine wanaokuambia usiache kusoma Neno la Mungu.

Ukiona kujisimamia siku za mwanzoni huwezi, kubali kuongozwa, kubali kusimamiwa, tena usiruhusu hali yeyote kuona unaonewa. Usijenge dhana yeyote kuona anayekusimamia anakuonea, ona hiyo ni kwa ajili ya faida yako mwenyewe.

Ndio maana tumepewa agizo la kuhubiri habari za Yesu Kristo kwa wale ambao bado hawajamkiri kama Bwana na Mwokozi wao. Kwa maana rahisi kabisa unaweza kuona ya nini tuhangaike na mtu mwingine wakati wewe tayari umeokoka, hapo utajua wokovu muda mwingine unapaswa kutangazwa kwa nguvu zote ndipo uweze kuingia kwenye masikio ya watu.

Ulazima utakulinda pale unapoona uhiari umekutoka, utatumia nguvu ya ulazima kufanya kile ambacho ulishaamua kukifanya kwenye maisha yako ya kila siku. Mfano kuamka asubuhi na mapema, moyoni unaweza kuwa unajisikia kuamka mapema ili ufanye shughuli zako. Ila ukashindwa kufanya hivyo pale unapoona muda wa kuamka umefika, kilaukitaka kuamka unajisikia mzito. Sasa hapo usipotumia nguvu ya ulazima utaendelea kulala na mambo yako mengine yatakufa siku hiyo.

Inafika saa ya kusoma Neno la Mungu kama ulivyojipangia, unaona kabisa mwili hutaki wala akili haitaki kutulia kwenye biblia. Tumia ulazima, haijalishi umechoka sana wala haijalishi unaona huelewi vizuri, fanya kurudiarudia hata mara tatu ili kuelewa. Nakwambia baada ya muda fulani utaona ule uchovu unakuachia na moyoni unajisikia amani kwa kufanya hicho kitendo.

Bila shaka umeelewa vizuri kuzitumia hizi silaha mbili Uhiari na Ulazima,nina imani utakuwa umepata kitu cha kukusaidia katika usomaji wako wa Neno la Mungu. Nikushauri usiishie kufurahia bali weka katika matendo, utaona mwelekeo mzuri wa kupanda viwango vya juu zaidi kuliko mwanzo.

Mungu akubariki sana kwa kutoa muda wako kusoma ujumbe huu, usiache kutembelea ukurasa wetu wa Chapeo Ya Wokovu. Kwa masomo mengine mazuri zaidi ya kukusaidia kukua katika usomaji wako wa Neno la Mungu.

Chapeo Ya Wokovu.

Email: chapeo@chapeotz.com

Blog: www.chapeotz.com

WhatsApp: +255759808081.