Nakusalimu katika jina la Bwana wetu Yesu Kristo aliye hai, zawadi nyingine tena njema kabisa machoni pa Bwana ameona vyema kutupa kibali cha kuiona siku ya leo. Sifa na utukufu tumrudishie yeye Bwana mwenza wa yote.

Tunapookoka wengi wetu huwa tunashindwa kuelewa tuombaje ili Mungu aweze kutusikia maombi yetu, wengine huwa tunakosa namna ya kupanga maneno ya kuombea jambo fulani. Tunapotazama na kuwasikiliza wengine wanavyoomba tunaona wao wanaomba vizuri zaidi kuliko sisi.

Tumeshindwa kufahamu maombi ni mazungumzo baina yetu na Baba yetu aliye mbinguni, maombi ni mawasiliano kati ya mwanadamu na Mungu wake, maombi ni uhitaji wa jambo/kitu fulani kutoka kwa Mungu. Ni kama unavyokuwa na hitaji lako unampelekea mzazi/mlezi wako akusaidie, na unajua maneno gani ya kuzungumza na mzazi/mlezi wako.

Huwezi kwenda kwa baba yako au mama yako au mlezi wako, ukiwa na hitaji la kwenda kumwomba akusaidie alafu ukafika pale ukaanza kushindwa kuzungumza naye. Hapo kutakuwa na mambo haya, huenda mahusiano yako na yeye yana shida au huenda kile unataka akusaidie huamini kama anaweza kukusaidia au huenda umetengeneza picha fulani mbaya juu yake.

Uhusiano wetu mzuri na Mungu unatufanya tuendelee kujifunza mengi ya kuweza kutusaidia kujua mengi ya kuweza kumpendeza Mungu wetu. Huwezi kupata wasiwasi labda umeomba vibaya ndio maana hujapokea kile uliomba, utakuwa na imani kile umeomba kwa mapenzi ya Mungu kitajibiwa.

Wasiwasi unakuja pale uhusiano wetu na Mungu unapokuwa mbali, tunaweza kuwa tumeokoka sawa ila ule ushirika na Mungu wetu unakuwa mbali. Tunaposema ushirika ni ule wa kuwa mtu wa ibada, ni kuwa msomaji wa Neno la Mungu na kupenda ibada za mafundisho.

Maombi yetu muda mwingine yamekosa mwelekeo kwa sababu tunaomba vibaya, tunaweza kuwa tunaomba vitu ambavyo vinatafuta kujinua, tunaweza kuwa tunamwomba Mungu vitu ambavyo tayari ameshatupa, tunaweza kuwa tunaomba vitu ambavyo vinaendelea kuondoa uhusiano wetu na Mungu.

Najua umewahi kuona mtoto anapewa ada na mzazi wake, ila anaenda kuzitumia kulewa pombe, anaenda kutumia na makahaba/malaya. Lakini wakati anaomba aliomba kwa kigezo cha ada au matumizi yake ya mahitaji ya shule/chuo. Mungu wetu anajua nia zetu za ndani, ndio maana mambo mengine tunaomba hatupewi kwa sababu tunataka tupewe tukatumie kwa tamaa zetu wenyewe.

Kuna maelekezo muhimu unapoenda mbele za Mungu kumwomba, na maelekezo hayo wengi tumeshindwa kuelewa, na badala yake tumejikuta tunaomba tu huku tukiendelea kumtenda dhambi.

Mfano mtu anaomba Mungu amsamehe makosa yake, alafu kuna ndugu yake hajamsamehe na ameapa hatakaa amsamehe kamwe. Mfano mwingine unakuta mtu anamwomba Mungu amjaze Roho Mtakatifu lakini ndani yake ana uchungu mwingi wa kutoachilia aliyemkosea/waliomkosea.

Wakati huo Neno la Mungu linasema tunapaswa kuwasemehe kwanza waliotukosea ndipo na yeye aweze kutusamehe makosa yetu. Yaani tunapaswa kutengeneza kwanza na wale waliotukosea na kuwaachilia mioyoni mwetu, hata wao wakiwa na kinyongo/chuki na sisi, sisi kama wakristo tunapaswa kuwasemehe.

Rejea: Nanyi, kila msimamapo na kusali, sameheni, mkiwa na neno juu ya mtu; ili na Baba yenu aliye mbinguni awasamehe na ninyi makosa yenu. [ Lakini kama ninyi hamsamehe, wala Baba yenu aliye mbinguni hatawasamehe ninyi makosa yenu.] MARKO 11:25‭-‬26 SUV.

Umeona hilo andiko, hebu fikiri umejaza watu moyoni mwako ambao hujawasemehe kabisa na wala hutaki kuwasemehe. Je unafikiri Mungu anaweza kutengua hilo andiko? Lazima usamehe ndipo na Mungu aweze kukusamehe, lazima uachilie uchungu juu yao. Maana kisasi ni juu ya Bwana.

Rejea: Wapenzi, msijilipize kisasi, bali ipisheni ghadhabu ya Mungu; maana imeandikwa, Kisasi ni juu yangu mimi; mimi nitalipa, anena Bwana. Warumi 12:19 SUV.

Usipojua haya unaweza kufikiri Mungu hakuoni wala huwa hakusikii maombi yako, omba yako inaweza isiwe na maana yeyote kama utakuwa na mambo mabaya juu ya wale waliokukosea. Tunajua wapo watu hawapendi kurejesha uhusiano mzuri pale tunapokosana, ila wewe hakikisha huruhusu uzembe wowote wa kutoachilia moyoni mwako.

Neno la Mungu linatupa maelekezo muhimu sana ya namna ya kuomba Mungu, haya yote huwezi kujua kama husomi Neno la Mungu. Hata unapoenda mbele za Mungu umejikuta huna salamu nzuri ya kumsalimia Mungu wako, umejikuta huna tabia ya kumshukuru Mungu kwanza na anapokutendea jambo, umejikuta huna tabia ya kutubu kwanza.

Unapokuwa na tabia ya kusoma Neno la Mungu, moyoni mwako unazidi kujenga vitu vya msingi sana, yapo makosa mengi sana utayarekebisha kadri unavyozidi kujifunza Neno la Mungu. Utajua na namna ya kuomba vizuri kwa sababu umejifunza, mchungaji wako anaweza asipate nafasi ya moja kwa moja kukufundisha unatakiwa uombaje, Neno la Mungu litakusaidia kujua hayo yote.

Soma Neno la Mungu kwa bidii zote, ili uwe imara kila kona, Neno la Mungu halikupi tu ahadi za Mungu alizokuahidi kukutendea. Bali Neno la Mungu linatupa uwezo wa kwenda mbele za Mungu kwa ujasiri.

Ikiwa Neno la Mungu linaweza kutusaidia kujua mengi ambayo hatuwezi kuyapata sehemu yeyote ile nje na Neno lake. Kwanini tusijikite kwenye hili, kwanini tusiweke nguvu kubwa kuhakikisha kila siku tunasoma Neno la Mungu. Muhimu kulitafakari hili kwa kina na kuchukua hatua mapema.

Bila shaka utakuwa umepata kitu cha kukusaidia katika kuinua usomaji wako wa Neno la Mungu, hakikisha unafanyia kazi yale umejifunza.

Mungu akubariki sana kwa kutoa muda wako kusoma ujumbe huu, endelea kutembelea ukurasa wetu wa Chapeo Ya Wokovu.

Chapeo Ya Wokovu.

Email: chapeo@chapeotz.com

Blog: www.chapeotz.com

WhatsApp: +255759808081.