Nakusalimu katika jina la Yesu Kristo aliye hai, siku nyingine tena mpya kabisa Bwana ametupa kibali cha kuiona. Sifa na utukufu tumrudishie yeye Bwana mwenza wa yote.
Mara nyingi huwa tunaanza vitu vizuri sana, hii inatokana na mtu jinsi alivyohamasika kuhusu hicho alichoanza kukifanya. Lakini mara nyingi mwendelezo wa yale tuliyoanza kufanya huwa hatufiki nayo mbali sana, unakuta tumeishia njiani.
Kunaweza kukawepo sababu za msingi kuhusu kuacha kufanya hicho kitu alichoanza nacho mtu kukifanya, inaweza kuwa alikuwa bado hajajua anapenda nini. Sasa wakati anaendelea kujitafuta ni eneo gani anaweza kufiti vizuri, anajikuta anafanya mambo mengi mpaka pale atakapoona hapa sasa nimefika eneo langu nililoletewa duniani na Mungu.
Inashuriwa mara nyingi kama hujajitambua unapenda nini, vizuri ukawa unafanya kila kitu kinachokusukuma kufanya ilimradi kisiwe kinamkosea Mungu. Njia hii ni rahisi sana kukufikisha eneo lako la wito alioweka Mungu ndani yako.
Muda mwingine unaweza kukaa tu bila kujishughulisha kujua unapenda kufanya nini, na usipate hicho unachopenda kufanya kwa Mazingira yeyote yale. Unajua ukishapata kitu kilicho ndani yako, ni ngumu sana kukatishwa tamaa kirahisi rahisi alafu ukakubaliana na hiyo hali.
Pamoja na kujifuta huko, unapaswa kuelewa sio kila kitu utafanya kwa sababu ni wito wako kufanya. Bali vipo vitu unapaswa kufanya kwa sababu ni wajibu wako kufanya hivyo, uwe unapenda au uwe hupendi unapaswa kukifanya. Na usipofanya madhara yake ni hutokua katika eneo unalopaswa wewe uwepo.
Hakuna mtu atakuja kukuambia usipokula utakufa, wewe mwenyewe unajua kabisa kutokula chakula kwa muda fulani kwa kigezo cha kutopenda kula. Madhara ya hicho unachofanya utakijua haraka sana pale mwili wako utakapoanza kukosa nguvu.
Kuhangaika kujitafuta huku imetokana na mfumo wa malezi yetu, hayajatutengeneza mapema kujua nini tunapenda ili tuweze kujitofautisha. Ndio maana tunakuwa watu wazima lakini mambo mengi bado hatujitambui.
Unaweza kuona vipo vitu vinahitaji uchaguzi kuvifanya na vipo vitu hupaswi kufanya uchaguzi bali vinakulazimu ufanye hata kama sio kwa hiari yako. Mfano unaweza kuona eneo la kumtumikia Mungu ni kwenye kuimba, ukatoa muda wako katika hilo, pia unaweza kuona eneo lako la kumtumikia/kumzalia Mungu matunda ni kuhubiri nyumba kwa nyumba au mtaa kwa mtaa, ukasimama katika eneo hilo na Mungu akubariki sana.
Tunapokuja kwenye suala la kusoma Neno la Mungu, lenyewe halihitaji uwe mwalimu, mwinjilisti, mtume, nabii, mchungaji ndio uanze kulisoma. Unapokuwa mkristo mwenye safari ya kwenda mbinguni, kusoma Neno la Mungu ni muhimu sana kwako, hakuna kusema hili ni jukumu la watu fulani.
Wengi tunafikiri vibaya sana ndio maana unamkuta mtu anaanza vizuri kusoma Neno la Mungu, alafu baada ya muda fulani anaacha kabisa hilo zoezi aliloanza nalo.
Unapaswa kujua kipi kimekufanya uache kusoma Neno la Mungu na wakati unaanza kipi kilikusuma kusoma Neno la Mungu. Ukishajua sababu zake ni rahisi sana kwako kutulia na kufakari kwanini unakuwa na tabia za kuanza na kuacha.
Tushakubaliana kwamba kuna vitu havina uchaguzi, uwe unapenda au uwe hupendi unapaswa kuvifanya, yaani uwe unapenda kuvaa nguo au hupendi kuvaa. Huwezi kusema Leo sitaki kuvaa nguo ukatoka kutembea barabarani ukiwa uchi, moja kwa moja watu watakuona umerukwa akili. Na huwezi kuwaaminisha watu kuwa hujisikii kuvaa nguo au huwezi kuwaambia umeacha kuvaa nguo kwa sababu zinakupa usumbufu fulani.
Hongera wewe unayesoma Neno la Mungu kila siku, swali kwako kwa wewe uliyeacha kusoma Neno la Mungu, ina maana umeona haina maana kabisa na haifai kabisa kusoma Neno la Mungu au kitu gani ambacho unaweza kujitetea nacho.
Umeokoka na Yesu Kristo ni Bwana na Mwokozi wa maisha yako, shida ni nini iliyokufanya uone kusoma Neno la Mungu ni suala lisilo la lazima kwako. Umeamua kuishia njiani, ni sawa hujajengwa tangu mdogo, wewe kama wewe unawezaje kuondokana na hili tatizo.
Kama Umeamua kuishia njiani maana yake umechagua kuendelea kuwa mtoto mchanga kiroho, maana yake umechagua kutembea mtupu. Nikiwa na maana moyoni mwako huna Neno la Mungu linaloweza kukusaidia kukufanya kuwa imara katika imani yako.
Ushauri wangu kwako ni kusoma Neno la Mungu maisha yako yote, hii iwe sehemu yako ya maisha. Unachokitafuta ndani ya Neno la Mungu ni kujenga uhusiano wako na unayemwamini, kama unavyozijua taratibu za kanisa lako, kama unavyojua ikitoka kwaya au waimbaji binafsi kinafuata nini. Ndivyo unavyopaswa kujua utaratibu wako wa kila siku ni kusoma Neno la Mungu.
Mungu akubariki sana kwa kutoa muda wako kusoma ujumbe huu, endelea kutafakari zaidi kuhusu wewe na Neno la Mungu. Ukiona ni ngumu kuliweka hili moyoni hakikisha unalazimisha urafiki na Neno la Mungu, uwe unapenda au uwe hupendi hakikisha umekuwa na urafiki mzuri na Neno la Mungu.
Chapeo Ya Wokovu.
Email: chapeo@chapeotz.com
Blog: www.chapeotz.com
WhatsApp: +255759808081.