Nakusalimu katika jina la Bwana wetu Yesu Kristo aliye hai, siku nyingine tena mpya kabisa Bwana ametupa kibali cha kuiona. Nafasi kwetu kwenda kumzalia Bwana matunda yaliyo mema, na nafasi yetu kutengeneza pale tulipokosea kwa kwenda kinyume na Mungu wetu.
Hivi kesho yako bado haijawahi kufika tangu mwaka unaanza na leo tumeingia sehemu ya pili kuelekea mwishoni mwa mwaka huu. Maana wakati unaanza mwaka huu ulisema huu ni mwaka wako wa kujenga mahusiano mazuri na Mungu wako.
Uliahidi utakuwa mtiifu katika kulisoma Neno la Mungu, uliahidi kuweka bidii ya kusoma Neno la Mungu, uliahidi kuhakikisha unapenyeza upate muda wa kusoma Neno la Mungu, uliahidi kuweka muda wako mwingi kusoma Neno la Mungu.
Mbona leo unaendelea na uimbaji wako ila hutaki kuweka ratiba zako kulisoma Neno la unayemwimbia, hizo nyimbo zako unazitolea wapi ikiwa huna muda wa kusoma Neno la unayemwimbia.
Mbona unaendelea na kuhubiri na kufundisha habari za Yesu Kristo lakini huna muda wa kusoma Neno lake. Unayofundisha unayatolea wapi, unawalisha watu nini ikiwa wewe mwenyewe hujala.
Ndege atawatemeaje chakula makinda wake ikiwa yeye mwenyewe hajala hicho chakula, ng’ombe atamnyonyesha ndama wake nini ikiwa hajala majani na kunywa maji ya kutosha. Maziwa ya ng’ombe huyu yatatokaje ikiwa hapati chakula kinachomfanya yeye mwenyewe apate nguvu.
Utawezaje kukabiliana na fujo za dunia hii iliyojaa ushawishi mwingi wa kukuvuta upotevuni, ikiwa hutokuwa na chujio la hayo maneno. Chujio hilo ni Neno la Mungu, hili ndilo linaweza kukusaidia kujua hizi ni mbivu na hizi ni mbichi.
Umeahidi sana, kila siku umekuwa mtu wa maneno tu, mwaka ndio unaishia hivyo bado hutaki kusoma Neno la Mungu. Kipi kinakufanya usisome Neno la Mungu, changamoto gani zinakubana kiasi kwamba ushindwe kusoma Neno la Mungu. Na huo muda mwingine unaupata wapi wa kufanya huduma zingine.
Sawa umeanza kujifunza Neno la Mungu, mbona unasoma biblia kama jambo la ziada sana yaani usome au usisome wewe yote ni sawa tu. Unafikiri ukisoma ilimradi tu unasoma utaweza kuona ile ladha ya Neno la Mungu? Nakwambia utaendelea kuona Neno la Mungu ni adhabu kwako, hutolisoma kama mtu anayejua thamani anayoipata humo ni kubwa mno na haipatikani sehemu yeyote.
Uliahidi utakuwa siriaz katika hili, uliahidi kuweka bidii mwaka huu, lakini mbona mwendo wako ni ule ule. Unasoma Neno la Mungu kwa kulipua lipua, hakuna siku wewe una nafasi ya kusoma Neno la Mungu, siku zako zote huwa upo bize. Ila muda wa kuchati na marafiki zako unao, ila muda wa kuzunguka kwenye mitandao ya kijamii unao, ila muda wa kukaa na marafiki zako unao. Cha ajabu muda wa kusoma Neno la Mungu ndio huna na unakuwa bize sana.
Utarekebisha lini hili ndugu yangu, utapunguza kukaa na marafiki zako lini, utapunguza makundi ya kuchati lini, utapunguza uzembe wako lini. Maana umeahidi kubadilika ila bado una tabia zile zile, nakukumbusha tena kuwa unaelekea mwisho wa mwaka Lakini bado una tabia zako zilezile.
Tabia yako ya kupuuzia Neno la Mungu bado inaendelea, utachukulia hili kwa uzito lini ikiwa miaka inazidi kukatika ila bado mwendo ni ule ule wa kupuuza. Bila shaka una hamu ya kubadilika, ila unapaswa kujua kwamba gharama inahitajika kutoka hapo.
Vizuri ukadhamiria kutoka ndani ya moyo wako kusoma Neno la Mungu, vinginevyo utaendelea kubaki na udhaifu wako ule ule. Wewe ni mtumishi wa Mungu, unapaswa kumzalia Bwana matunda yaliyo mema mbele zake. Hivi mti utawezaje kukua na kuanza kutoa matunda ikiwa mti huo hutanyeshewa na mvua au hutomwangiliwa maji, na hutowekewa mbolea? Ni kitu ambacho hakiwezekani.
Hatupaswi kuwa wakristo wa jumla jumla, lazima tujitofautishe kwa matunda ya kazi zetu. Mungu ana kitu ameweka ndani yangu ambacho wewe huna, na wewe kuna kitu Mungu amekiweka kwako ambacho mimi sina. Mimi nikikaa kwenye eneo langu na wewe ukakaa eneo lako, lazima jina la Yesu Kristo litukuzwe kupitia sisi.
Shida inakuja pale ambapo hutaki kuusoma mwongozo wa maisha yako unaokusaidia kulifanya/kulitenda kusudi la maisha yako. Ambalo hilo kusudi ndilo ameliweka Mungu ndani yako, litawezaje kuimarishwa zaidi wakati unaona Neno la Mungu ni mzigo kwako.
Hebu amua leo kuchukua hatua za kuweza kusimama katika usomaji wako wa Neno la Mungu, achana na ahadi hewa, chukua hatua za kuweza kukujenga kiroho.
Mungu akubariki sana kwa kutoa muda wako kusoma ujumbe huu.
Chapeo Ya Wokovu.
Email: chapeo@chapeotz.com
Blog: www.chapeotz.com
WhatsApp: +255759808081.