Haleluya, siku nyingine tena mpya na njema kabisa machoni pa Bwana ameona vyema kutupa kibali cha kuweza kuiona. Sifa na utukufu tumrudishie yeye Bwana mwenza wa yote.
Kuna vitu vinashangaza ndugu zangu, mpaka mtu kufikia hatua ya kuanza kufikiri msaada pekee anaoweza kuupata ni kwa mganga wa kienyeji na sio kwa Yesu Kristo. Ujue huyo mtu alikuwa mchanga sana wa kiroho, kwa sababu mtu yeyote mwenye mahusiano mazuri na Mungu wake na aliyeshiba vizuri Neno la Mungu. Hawezi kutamani kwenda kwa waganga wa kienyeji wanaotumia nguvu za giza.
Unapoambiwa unapaswa kukua kiroho ili uweze kukabiliana na changamoto ngumu utakazokutana nazo katika safari yako ya wokovu. Usifikiri ni jambo la kawaida, ni jambo la muhimu sana kwako kama utaamua kweli kulijaza Neno la Mungu.
Mambo mengi tunayapa nafasi mioyoni mwetu kwa sababu hakuna Neno la Mungu, tumeipa mioyo yetu nafasi kubwa ya kuweza kuingiza vitu visivyofaa na vikatengeneza makao yake humo ndani. Tunapokuja kushtuka tayari tumeshazama katika uovu na kurudi mbele za Mungu tunaona aibu.
Nakuhakikishia mkristo yeyote aliyekomaa kiroho, hawezi kutamani kwenda kwa waganga wa kienyeji, wala hilo wazo kwake haliwezi kupata nafasi hata kidogo. Maana anajua kabisa uweza na nguvu alizonazo Mungu huwezi kufananishwa na mchawi yeyote chini ya jua.
Upuuzi mwingi wa kufanya mambo ya kumkosea Mungu, ni kutokana na kupungukiwa mafundisho ya Neno la Mungu. Huwezi kuona pombe inaweza kukuondolea mawazo ikiwa unajua maandiko matakatifu yanasemaje kuhusu pombe, huwezi kutamani kujihusisha na madawa ya kulevya kwa kisingizio cha kukupunguzia mawazo yako.
Uchanga wa kiroho ndio unatufanya vijana wengi tujiingize katika makundi mabaya, ambapo makundi hayo yamechagua kuishi maisha ya ya uasi. Ndio maana wakati wa sodoma na gomora, Lutu na wanaye wawili hawakuishi maisha ya dhambi kama walivyofanya watu wote wa miji ile.
Uhusiano wetu na Mungu huondolewi na changamoto ikiwa tu tutakuwa tunajua uweza wa Baba yetu aliye mbinguni. Kweli changamoto au majaribu yanaweza kutujia ili kutuondoa katika imani yetu, ila ikiwa tutakuwa na Neno la Mungu lililoshibisha mioyo yetu. Hakuna siku utatamani kuacha wokovu, kwanza utaacha wokovu uende wapi na wakati unajua mwenye vyote chini ya dunia na mbinguni ni vyake vyote, na ndiyo huyo uliye naye moyoni mwako.
Tena Bwana anatusihi tuwe na uhusiano naye hata kama tutakutana na mambo magumu, bado yeye ni yeye yule jana leo na hata milele. Tunapaswa kuzitafakari njia zake na kupeleka hoja zetu zenye nguvu ili asikiapo vile tunahitaji kwake anatutendea sawasawa na mapenzi yake.
Rejea: Tieni moyoni boma zake, Yafikirini majumba yake, Mpate kuwaambia kizazi kitakachokuja. Kwa maana ndivyo alivyo MUNGU, Mungu wetu. Milele na milele Yeye ndiye atakayetuongoza.ZABURI 48:13-14 SUV.
Tia Neno la Mungu moyoni mwako ili uweze kutangaza ukuu wa Bwana vizazi na vizazi, yatafakari matendo makuu ya Mungu ili uweze kuwaeleza kizazi chako ukuu wa Mungu ulivyo. Huwezi kumweleza mtu uweza wa Mungu wako ikiwa wewe mwenyewe ukibanwa kidogo unachomokea kwa waganga wa kienyeji.
Utazitangaza habari za Yesu Kristo kwa ujasiri kwa sababu unajua ulipopatwa na shida fulani hakukuacha, utakuwa na shuhuda zenye nguvu kuliko yule aliyeenda kutafuta msaada kwa miungu mingine.
Utazitangaza vipi habari za Yesu Kristo wakati marafiki zako wanakuona ulishindwa kuvumilia wakati huna mtoto ukaenda kwa waganga wa kienyeji. Marafiki/ndugu zako watakuelewaje kuwa Yesu Kristo anaweza wakati unatafuta wa kukuoa uliamua kwenda kutafuta msaada kwa miungu mingine ya mababu zako.
Ukomavu wako wa kiroho ndio utakaokuepusha na kuliebisha jina la Yesu Kristo kwa matendo yako maovu, hakikisha Neno la Mungu lijaa kwa wingi moyoni mwako. Usijione sasa hivi una amani sana, usijione huna muda wa kusoma Neno la Mungu, tafuta nafasi kwa njia yeyote ile kupata nafasi ya kusoma Neno la Mungu na kutafakari yale unayojifunza.
Hakuna siku utaweza kuepukana na changamoto mbalimbali za maisha, hutaishi siku zote bila kujarabiwa, hajalishi umejaa nguvu za Mungu kiasi gani. Utafika kipindi imani yako lazima ipimwe kama kweli umesimama na Mungu wako wa kweli, kama hujajizamisha kwenye Neno la Mungu, ni rahisi sana kuiacha imani yako.
Ili kesho usijikute unatafuta msaada wa miungu mingine, hakikisha Neno la Mungu linakaa kwa wingi moyoni mwako. Sio kwa faida yangu wala sio kwa ajili ya baba, mama, shangazi, mjomba, dada au kaka. Ni kwa ajili yako wewe, hao ndugu zako watajifunza wenyewe kwa matendo yako mema jinsi unavyomtegemea Mungu wako.
Bila shaka umepata mwanga zaidi kuhusu umhimu wa kusoma Neno la Mungu na kuliweka moyoni mwako. Furaha yangu ulichukulie hili suala la kusoma Neno la Mungu kwa uzito mkubwa na ulifanyie kazi kwa vitendo. Ninakuhakikishia hutokaa ujute maisha yako yote, Neno la Mungu ni mwongozo sahihi wa mkristo, popote alipo kwenye jambo lolote lile gumu Neno la Mungu linaweza kumwongoza.
Mungu akubariki sana kwa kutoa muda wako kusoma ujumbe huu, endelea kutafakari niliyokueleza huku ukiweka mikakati imara ya kuimarisha usomaji wako wa Neno la Mungu.
Chapeo Ya Wokovu.
chapeo@chapeotz.com
www.chapeotz.com
+255759808081.