Nakusalimu katika jina la Bwana wetu Yesu Kristo aliye hai, siku nyingine tena mpya kabisa Bwana ametupa kibali cha kuiona. Hatutaacha kumrudishia Mungu wetu sifa na utukufu kwa neema hii ya uhai anayoendelea kutupa watu wake.

Kuna mawazo tunakuwa nayo ndani ya fahamu zetu, mawazo hayo yanatufanya tuendelee kulea uzembe tulionao ndani mwetu. Lakini sisi kama sisi tunajiona tupo sahihi, na kujiona tunavyofikiri na kuenenda tupo sawa.

Yapo mambo mtu wa rika fulani yakiyafanya lazima tumshangae kwanini anafanya, na yapo mambo akifanya mtu wa rika hilohilo tulilomshangaa tunaweza tusimshangae kutokana na umri wake na kile anafanya.

Pamoja na hayo elewa pia kuna mambo hayahitaji kufanywa na watu wa umri fulani, wote tunapaswa kuyafanya hata kama sio kwa kiwango cha rika la ujana na rika la uzee.

Tunapaswa kuelewa pia kuishi maisha ya kumpenda Mungu hakuangalii umri mkubwa na mdogo, pia tunapaswa kuelewa kumpenda Mungu kwa kumaanisha sio kundi fulani la watu waliochokachoka au wenye duni za maisha.

Tunapaswa kuelewa kuwa siriaz na mambo ya Mungu sio kwa kundi fulani lisilo na kazi/shughuli za kufanya. Na kujiona sisi tulio na shughuli za kufanya hatuwezi kumpendeza Mungu kwa viwango fulani, kwa kufikiri fedha/mali zetu zinaweza kutusaidia kila kitu.

Wengine wamefika mbali zaidi, mfano mama/dada akijitambua yeye ni mzuri wa sura na umbo. Anaona hawezi kujihangaisha hangaisha na mambo ya Mungu, anachoona yeye wenye kuweza kufanya hivyo ni wale wenye sura zisizo na uzuri kama wake.

Mitazamo hii hasi imepelekea mpaka kwenye Neno la Mungu, wengi wanaona kusoma Neno la Mungu ni mambo ya vijana, na wengine wanaona ni mambo ya wazee, na wengine wanaona ni mambo ya wachungaji, na wengine wanaona ni mambo ya watu wasio na kazi za kufanya.

Wengine wanaona ni mambo ya watu walio na nafasi za kutosha kwa siku, yaani kila mmoja anatafuta pa kujifichia ili tu asiweze kusoma Neno la Mungu. Kama kuna mahali pameandikwa, kwa kuwa vijana wana changamoto nyingi wakifia kwenye dhambi hawatahukumiwa siku ya mwisho. Basi unaweza kuwaza hivyo na ukaendelea na uzembe wako, ila kama hakuna andiko la namna hiyo unapaswa kufuta dhana potofu akilini mwako.

Kusoma Neno la Mungu sio kazi ya kundi fulani lisilo na mambo mengi ya kufanya, kusoma Neno la Mungu ni wajibu wa kila mtu. Labda uwe hujui kabisa kusoma, lakini bado una nafasi ya kutumia masikio yako kusoma kwa njia ya kusikiliza sauti.

Huna sababu yeyote ya kujikinga nayo ili uweze kukwepa hili, kama bado una nguvu na unaweza kufanya shughuli zako zingine. Unapaswa kuwa na ratiba ya kusoma Neno la Mungu, bila kujiona wewe ni mtu rasmi sana katika jamii/taifa.

Unapokuwa ofisini kwako na una cheo kikubwa na kila mtu anakupigia magoti, unapaswa kuelewa kwa Mungu wewe ni mtu mdogo sana unayepaswa kumpa muda na heshima yake. Fedha na mali zako vina nafasi yake, hakikisha biblia inakuwa rafiki yako wa damu damu.

Una gari lako mwenyewe hakikisha biblia ipo ndani ya gari, una ofisi yako hakikisha biblia hakosekani kwenye droo zako, hii ni kuonyesha mambo yako yote pasipo Mungu huwezi chochote. Usimalize siku bila sababu yeyote alafu usisome Neno la Mungu, utasema nabanwa sana kazini, mbona unapata muda wa kuingia facebook, whatsApp na instagram, inakuwaje muda wa kuingia mtandao wa biblia unaukosa?

Kusoma Neno la Mungu sio kwa kundi fulani rasmi, wote tunapaswa kuwa na ratiba ya kusoma Neno la Mungu. Tuwaache wale wazee ambao tayari hawana uwezo wa kusikia wala kuona, maana miili yao imechoka wanachosubiri ni Mungu awaondolee uhai wao.

Kuanzia sasa futa dhana potofu kuhusu usomaji wa Neno la Mungu, usijione wewe ni wa kundi fulani hutoweza kusoma Neno la Mungu. Ukajiona wewe ni wa kusoma magazeti ila Neno la Mungu unaona sio hadhi yako, utakuwa umeamua kujipotosha mwenyewe.

Bila shaka umepata kitu cha kukusaidia kuboresha usomaji wako wa Neno la Mungu, na kama ulikuwa unasitasita kusoma Neno la Mungu naamini unaenda kuanza kwa nguvu mpya.

Mungu akubariki sana kwa kutoa muda wako kusoma ujumbe huu, endelea kutafakari zaidi kuhusu yale umesoma hapa.

Chapeo Ya Wokovu.

Email: chapeo@chapeotz.com

Blog: www.chapeotz.com

WhatsApp: +255759808081.