Nakusalimu katika jina la Bwana wetu Yesu Kristo aliye hai, siku nyingine tena mpya kabisa Bwana ametupa kibali cha kuiona. Tunamrudishia Mungu wetu sifa na utukufu kwa neema yake hii aliyotupa.
Kuna msemo unasema “rizika na ulichonacho au rizika na hali uliyonayo”kauli hii inaweza ikawa sahihi kabisa ila upande mwingine tunaweza kusema wapo watu wengine wakawa wameitafsiri vibaya. Kama utarizika na uzembe ulionao kisa kuna msemo unasema hivyo ujue hayo sio matumizi sahihi ya msemo huo.
Tunasema sio matumizi sahihi kwa sababu ukiendelea na tabia yako hiyo bila kubadilika, hata hicho kidogo kizuri ulichokuwa nacho kinaweza kusinyaa na kupotea kabisa. Kutokana na kutoendelezwa na kukuzwa kila siku.
Vipo vitu pia vina ukomo wa ukuaji wake, mfano mwili wa nyama una ukomo wake kurefuka, mtu akishafika umri fulani hawezi kuongeza urefu tena. Isipokuwa anaweza kuongezeka kilo zake za mwili au anaweza kupungua kilo zake cha mwili, kama alikuwa mwembamba anaweza kuwa mnene na kama alikuwa mnene anaweza kupungua unene wake.
Wakati yupo anapambana kupunguza unene wake, yupo mtu mwingine anatamani kunenepa. Hiyo yote ni kutaka kufikia hatua fulani ambayo mtu alikuwa hana wakati huo.
Unaweza kutamani kuwa na nyumba yako, utapambana utaipata. Utakapoipata hiyo nyumba yenyewe hahitaji uikuze zaidi, kuikuza kwake utapaswa kuongeza nyumba nyingine tena, ukiimaliza na hiyo ukaona bado una nafasi utapaswa kuongeza zaidi. Huo ni ukuaji wa nyumba huwezi kuikuza yenyewe kama yenyewe labda uwe ulijenga msingi wa ghorofa ili uendelee kuipandisha juu au uwe ulijenga ndogo ukataka kubomoa na kuipanua zaidi.
Changamoto ipo katika ukuaji wa kiroho, wengine walivyoweza kutoa pepo ndio wameona mambo yote yameishia hapo. Hawataki tena kujishughulisha na mambo mengine ili waendelee kumjua Mungu zaidi na zaidi.
Wengine walivyoimba nyimbo zikawa baraka kwa watu wengi, waliona imetosha hawahitaji tena kuongeza kitu kingine cha kuwasogeza hatua zingine kiroho. Ndio maana ukifuatilia waimbaji wengi albamu ya kwanza huwa nzuri na ina uwepo wa Mungu ukiisikiliza, ila zinazoendelea zinakuwa kawaida sana.
Wewe kama wewe hapo ulipo unatamani kukua kiroho au umeridhika baada ya kuona umejazwa na Roho Mtakatifu, umeona huhitaji tena mambo mengine. Roho Mtakatifu anataka kukusaidia kukuboresha kwenye baadhi ya maeneo, wewe umeona imetosha.
Unapaswa kujua usomaji wako wa Neno la Mungu una tofauti na mwezi wa kwanza, wa pili, wa tatu, wa nne, wa tano, wa sita, wa saba na leo tupo wa nane. Je unaona unaongezeka au tangu ulivyoanza unajiona upo vile vile na huhitaji tena kuongezeka? Kama upo vile vile unahitaji msaada wa Mungu, hata kama unajiona upo vizuri kiroho.
Unapaswa kusogea viwango vingine, unapaswa kuonekana unakua siku hadi siku, ulivyokuwa mwezi uliopita akija mtu leo kukutazama akuone umesogea hatua nyingine. Hata mtu akikuambia nieleze jinsi unavyoelewa jambo fulani ndani ya biblia, aone utofauti wako ulivyokuwa nyuma na ulipo sasa.
Chochote kizuri unachokifanya tamani kuongezeka, usibaki hivyo hivyo miaka nenda rudi, kuza kiwango chako kwa kuweka bidii katika lile unalifanya. Usomaji wako wa Neno la Mungu uonekane una matunda kwako na kwa wengine, usisome kusukuma siku, soma ukijua kipo kitu unapata na unachokipata kinafungua maeneo fulani.
Unapofunguliwa hutatazamii kukuona unabakia kwenye udhaifu huo, tunatazamia uwe kwenye Kiwango fulani tofauti na ulivyokuwa mwanzo. Unapoendelea kubaki pale pale tunakuwa na mashaka na ukujua wako wa kiroho.
Usiridhike na kiwango chako cha kuhifadhi maandiko mengi kichwani, tamani kuona ulichokihifadhi kinazaa matunda zaidi na kile ambacho huwa unacho unazidi kukijaza zaidi. Usikae unajisifia umesoma sana biblia miaka ya nyuma alafu hapo ulipo husomi, labda uwe na sababu ya msingi kutofanya hivyo.
Bila shaka umepata kitu cha kukusaidia kuboresha mwenendo wako wa usomaji wa Neno la Mungu, endelea kutafakari zaidi kuhusu haya niliyokueleza hapa utapata kuelewa zaidi pale ulipoona hujaelewa.
Mungu akubariki sana kwa kutoa muda wako kusoma ujumbe huu, endelea kutembelea mtandao wetu wa Chapeo Ya Wokovu kwa masomo mengine mazuri zaidi.
Chapeo Ya Wokovu.
Email: chapeo@chapeotz.com
Blog: www.chapeotz.com
WhatsApp: +255759808081.