Nakusalimu katika jina la Bwana wetu Yesu Kristo aliye hai, siku nyingine tena mpya kabisa Bwana ametupa kibali cha kuiona. Hatutaacha wala hatutachoka kumrudishia sifa na utukufu Mungu wetu kwa neema hii ya uzima.
Kuna maamzi unaweza kuyafanya ukiwa kwenye uchanga fulani wa kiroho, baadaye ukija kuwa vizuri kiroho yaani namaanisha ukija kukua kiroho. Unakuja kujiona maamzi uliyofanya wakati mchanga wa kiroho, hayakuwa maamzi sahihi kwako.
Wakati mwingine unaweza kusemeshwa na Roho Mtakatifu kuhusu hilo jambo unalotaka kuchukua maamzi, ukaona moyoni uendelee na mipango yako. Roho Mtakatifu anaweza kukusemesha kwa kukuondolea furaha moyoni mwako kwa hilo unalotaka kufanya maamzi, ukaona ni hali ya kawaida na ukaendelea nacho.
Mungu wakati mwingine hutuacha kwanza kutokana na ugumu wa mioyo yetu, ili tukapoumizwa tujifunze na kuelewa kwanini tulipata huzuni kabla ya kufanya kile tulichokuwa tunataka kufanya.
Hebu fikiri uliingia kwenye mahusiano ya ndoa na mwanamke/mwanaume ambaye hakuwa ndoto yako. Ila kwa sababu ulikuwa mchanga wa kiroho, ulishindwa kujisikiliza na hata Mungu alipojaribu kukunasua ulikuwa mbishi. Badala yake ulivyoona anakuzungusha na kukuletea vituko vya ajabu ajabu, uliamua kutegesha mimba ili akose cha kujitetea.
Umetamani upate mke/mume sahihi alafu unakuwa unafanya naye uasherati huyo mchumba wako kabla ya ndoa, ukifikiri ni jambo la siri kati yenu na halina madhara kwako. Hapo unashindwa kujua unaondoa uwepo wa Mungu kabisa kuhusika katika kukusaidia.
Hayo yote unaweza kuwa unayafanya kwa sababu ya uchanga wa kiroho, bahati mbaya ukawa umeingia tayari Kwenye jambo ambalo hukujua madhara yake baadaye. Ndio maana unakuta wengi wapo ndani ya ndoa lakini hawana furaha na waume zao na wake zao, ukimhoji labda mke/mume wako kuna jambo baya anakufanyia mpaka ukamchukia, anakuwa hana sababu.
Sipo kukufundisha somo la ndoa ila nataka upate picha ya madhara ya kufanya maamzi ukiwa mchanga wa kiroho, mchanga wa kiroho ana matakataka mengi sana katika ubongo wake. Tena hatari zaidi Mungu anaweza kuwatumia watumishi wake kwenda kumshauri kuhusu jambo fulani akaona anafuatiliwa.
Mchanga wa kiroho anaweza kuwa kanisani, lakini akawa anafanya vitu ambavyo ukikaa chini unamwona huyu anahitaji msaada mkubwa, ila yeye mwenyewe anakuwa hajui kama anahitaji msaada. Maana anajiona ana kiwango fulani kikubwa cha elimu ya darasani, anasahau mambo ya kiroho hayaletwi na kumaliza chuo kikuu.
Ipo faida kubwa sana kukomaa kiroho, hata kama sio kwa kiwango kikubwa sana lakini kuna tofauti kubwa na yule ambaye ni mchanga kabisa. Mara nyingi maamzi yao huwa sio ya kujutia, mara nyingi huwa wanaweza kujisimamia katika kuamua mambo yao, mara nyingi ni watu wa kupenda kusikiliza watu wengine wanaowashauri na kukaa chini kuchambua ushauri waliopata unafaa au haufai.
Ukomavu wa kiroho hauji tu hivi hivi, lazima ujue kuna gharama yake, na gharama yake ni kulijaza Neno la Mungu moyoni mwako. Huu ndio ukweli wenyewe huwezi sema naomba sana Mungu, wakati mwingine unafunga na kuomba. Napata wasiwasi unaombaje ikiwa hujui ahadi zako zilizo ndani ya Neno la Mungu, unajuaje hicho unachoomba unapaswa uombe?
Unaweza kushangaa unaomba kitu ambacho kinahitaji tu uwe na maarifa ndipo ukipokee, kwa kuwa hujui unaendelea kukazana kuomba. Wakati ungekuwa na maarifa ungeweza kuvuka haraka.
Hebu ondoka kwenye uchanga wa kiroho na uje katika faida ya kukua kiroho, hii itakufanya ufurahie kuokoka kwako. Muda mwingine umekuwa mtu wa kurudi nyuma kila wakati kutokana na uchanga wako wa kiroho, kutokana na huna maarifa ya kutosha ndio maana unajikuta umemtenda Mungu dhambi.
Wekeza nguvu zako zote katika kutafuta Mungu anasema nini kupitia Neno lake, utaona kiwango chako cha kiroho kikipanda siku hadi siku. Bora kuomba Mungu akufungue ufahamu wako uweze kuelewa Neno lake, kuliko kuomba Mungu akukuze kiroho huku hujishughulishi na chochote kinachoitwa kusoma Neno la Mungu.
Mungu akubariki sana kwa kutoa muda wako kusoma ujumbe huu, endelea kutembelea mtandao wetu wa Chapeo Ya Wokovu ili uendelee kupokea mafundisho ya kukujenga kiroho.
Chapeo Ya Wokovu.
Email: chapeo@chapeotz.com
Blog: www.chapeotz.com
WhatsApp: +255759808081.