Nakusalimu katika jina la Bwana wetu Yesu Kristo aliye hai, siku nyingine tena mpya na njema kabisa machoni pa Bwana ameona vyema kutupa kibali cha kuiona leo. Sifa na utukufu tumrudishie yeye Bwana mwenza wa yote, maana anatupa kutengeneza pale tulipokosea jana alafu hatukutubu. Na tunaoishi maisha matakatifu ametupa kibali kingine cha kwenda kumzalia matunda yaliyo mema mbele zake.

Sio wote tunaoenda mbele za Mungu kumwomba jambo fulani atusaidie au atutendee, huwa tunaenda tukiwa na uhakika Mungu anaweza kujibu mahitaji yetu. Muda mwingine tumeenda tu kwa kuona wengine wakifanya hivyo, ila ule uhakika kabisa wa kusema Mungu anaweza kutusaidia kwa lile tunalomwomba tunakuwa hatuna imani kabisa.

Wote tunajua tunamwamini Mungu yupo kwa imani, imani zetu zinakuja kwa kuwa na picha fulani halisi. Ambapo hiyo picha inakuwa ndani mwetu, huwezi kuwa na imani iliyosimama kama huna kitu kinachokufanya uwe na imani hiyo.

Unapoenda mbele za Mungu kumwomba jambo fulani akusaidie, kwanza kabisa unapaswa kuwa na uhakika Mungu anaweza kukujibu hicho unachomwomba. Ujasiri wetu unapaswa kuwa mkubwa ndani mwetu kwa kumjua Mungu wetu.

Ujasiri huo tunaupata wapi sasa, swali zuri kabisa, ujasiri huo tunaupata tunapojifunza Neno la Mungu. Neno la Mungu linatupa ujasiri mkubwa wa kwenda mbele Mungu kumwomba vile vitu tunapoona tumeahidiwa alafu hatuvioni maishani mwetu.

Tunakuwa na mahitaji mengi mbele za Mungu kwa kujua kwanza Neno lake linatuambia nini, hapo ndipo tunakuwa na sura ya kiMungu ndani mwetu kwa imani. Pia tunakuwa na uhakika tukiomba kwa mapenzi ya Mungu, Mungu anaweza kutusaidia kile tunaomba kwake.

Ili uweze kuelewa haya na uwe na ujasiri wa kumwendea Mungu kumweleza shida zako, lazima utoe gharama kufikia viwango hivi. Huwezi kufika kwenye hatua ya kumwamini Yesu Kristo kama huna Neno la Mungu la kutosha.

Nasema hivi Daniel kuwa jasiri kuendelea kushikilia imani yake, hata pale alipoonywa juu ya mwenendo wake wa kukataa kuabudu mungu mwingine. Haukuwa ujasiri wa hivi hivi, alikuwa anajua uwezo wa Mungu wake, alikuwa anajua Baba ana nguvu na utiisho zaidi ya mfalme.

Kutupiwa kwa Daniel kwenye zinzi la simba wakali usifikiri alitupiwa tu bila kuwa na uhakika wale simba walikuwa wanakula watu. Lazima kuna watu wamewahi kutupiwa humo wakaliwa na simba wale, usifikiri Daniel mwenyewe hakuwahi kuona wale simba wanavyokula watu. Nina uhakika kabisa wale simba hawakuanza kwa Daniel, lazima kuna watu wamewahi kupoteza maisha yao humo.

Ujasiri wa Daniel ulitokana na kuelewa ukuu wa Mungu, kwa leo tungeweza kusema Daniel alikuwa jeuri haswa. Hivi unaletewa agizo kutoka kwa rais wako wa nchi usifanye kitu fulani, alafu wewe unaendelea kufanya, tena Daniel aliongeza dozi ya maombi kwa siku mara tatu tena anaacha na madirisha wazi.

Huo kama sio ujeuri ni nini? Lazima huyu Daniel alikuwa anamwelewa Mungu vizuri, hakuwa mtu wa kumkana Mungu wake. Hebu fikiri vijana wangapi wanaweza kusimama na imani zao katikati ya matisho ya kuwataka wamwabudu mungu mwingine.

Ujasiri wetu unatokana na kumjua Mungu wetu, njia ya kumjua ni kusoma Neno lake. Hakuna mkato katika hili lazima ujitoe haswa, ili kuwa na maarifa ya kutosha ndio uweze kusimama na Mungu wako.

Mungu anaweza kukutendea muujiza mkubwa ukajenga imani naye vizuri, akaja mtu anakuambia jambo la kukuondoa kwenye imani yako. Kwa kuwa na wewe ni mchanga wa kiroho, unarudi nyuma kirahisi sana.

Unatamani uwe na imani iliyo na mizizi imara, hakikisha Neno la Mungu linakuwa rafiki yako. Tena rafiki wa damu ambaye haupo tayari kumpoteza kwa lolote lile.

Mungu akubariki sana kwa kutoa muda wako kusoma ujumbe huu, nikusihi uendelee kutembelea mtandao wetu wa Chapeo Ya Wokovu kwa masomo mengine mazuri zaidi.

Chapeo Ya Wokovu.

Email: chapeo@chapeotz.com

Blog: www.chapeotz.com

WhatsApp: +255759808081.