Nakusalimu katika jina la Bwana wetu Yesu Kristo aliye hai, siku nyingine tena mpya kabisa Bwana ametupa kibali cha kuweza kuiona. Sifa na utukufu tumrudishie yeye Bwana mwenza wa yote, atupaye kushinda kila siku kwa wale wanaomcha na kumtegemea yeye.
Ukingia kusoma Neno la Mungu bila kujitoa wewe kama wewe, ni rahisi sana kurushindishwa nyuma na maneno ya watu wasiopenda kusoma Neno la Mungu. Yapo maneno mengi sana ya kuvunja moyo pale unapoanza kusoma Neno la Mungu hasa pale unapogundulika na marafiki zako wasiofanya hilo zoezi.
Haina tofauti sana na mtu anayeanza wokovu, kama hakuchukua maamzi yaliyo sahihi labda alisukumwa na jambo fulani lililomfanya amwamini Yesu Kristo. Mtu huyu ni rahisi sana kurudi nyuma kama hatapata mwalimu mzuri wa kumsaidia, maana kuna wapo wanaokoka ili wapate waume/wake wazuri wa kuishi nao, kuna wameongozwa sala ya toba walivyokuwa wameshikiliwa na pepo wachafu.
Maisha ya mtu wa namna hii awe kweli aliamua kuokoka baada ya kuona uweza wa Mungu ndani yake, vinginevyo atapona na hali yake ya awali hapo hapo atakutana na ugumu wa yeye kuwambia watu nimeokoka. Hasahasa kama alikuwa imani tofauti na ya ukristo, anapotishwa kidogo na kuambiwa tutakutenga katika familia yetu anaona bora aendelee na imani yake ya kumkataa Yesu Kristo.
Ndivyo ilivyo katika usomaji wako wa Neno la Mungu, kama hukufikiri vizuri ukaanza kusoma Neno la Mungu kwa nguvu zote. Nakwambia kuna watu wana maneno hujawahi kufikiri, utasikia Biblia huwezi kuelewa kama hujaenda chuo cha biblia, utasikia biblia ukiisoma sana utachanganyikiwa.
Mtu anakwambia ukisoma sana biblia utachanganyikiwa, alafu anayekuambia hivyo ni mtu unayemwamini ameanza wokovu siku nyingi. Uwe na uhakika kama utakuwa umempa nafasi moyoni mwako, ukienda sana labda siku mbili au wiki, unaanza kujiona unabanwa sana na kazi, na ile hamu ya kusoma inapotea kabisa. Kumbe kuna maneno mabaya yalipandwa ndani ya moyo wako na wewe ukayaruhusu yafanye kazi.
Mimi nina miaka miwili sasa inaenda mitatu nikiwa nasoma biblia sura hadi sura, na hili zoezi nimechagua kulifanya maisha yangu yote nikiwa hai. Lakini sijawahi kuchanganyikiwa zaidi sana naona nazidi kukua kiroho, nazidi kumjua Mungu kwa kiwango cha tofauti siku hadi siku.
Anayekuambia biblia inaharibu akili za mtu atakuwa amekuingiza kwenye uongo, ambao huo uongo utakushikilia maisha yako yote na kuusambaza hata kwa kizazi chako. Hakuna sehemu imeandikwa ukisoma sana biblia utachanganyikia, na inayokuambia epuka kusoma sana biblia. Hiyo sehemu sijaona nimesoma Mathayo mpaka ufunuo na nimeanza Mwanzo mpaka leo nipo kitabu cha Zaburi.
Nakusihi uanze kusoma Neno la Mungu kwa picha mpya ndani yako, kama ulikuwa unasoma biblia ili siku ziende badilisha haraka hiyo picha. Soma kwa lengo la kutafuta kumjua Mungu wako vizuri, anasema nini juu ya maisha yako.
Nakwambia kusoma Neno la Mungu hakutakuwa tena mzingo kwako badala yake usiposoma utaona umepoteza kitu cha msingi sana katika siku yako. Huhitaji kutafuta mchawi ni nani, ni wewe kuamua kusoma Neno la Mungu wewe kama wewe bila kutazama watu wanakuambia maneno gani ya kukuvunja moyo.
Ikiwa walisema hutofikisha mwaka ukiwa ndani ya wokovu, na leo umefikisha mwaka na bado Yesu Kristo anatukuzwa moyoni mwako. Kwanini upandiwe dhana potofu moyoni mwako, kataa hiyo hali kwa kuanza kusoma Neno la Mungu kwa picha nzuri ya kumjua Mungu wako.
Jiunge na marafiki wanaopenda kusoma Neno la Mungu, hii ni njia niliyoitumia mimi kutokurudi nyuma pale nilipojisikia kuvunjwa moyo. Njia hiyo ni kuwa na marafiki mliopatana pamoja kusoma Neno la Mungu, na marafiki hao ninao whatsApp group.
Mungu akubariki sana kwa kutoa muda wako kusoma ujumbe huu, endelea kutembelea mtandao wetu wa Chapeo Ya Wokovu.
Fb: Chapeo Ya Wokovu
Email: chapeo@chapeotz.com
Blog: www.chapeotz.com
WhatsApp: +255759808081.