Nakusalimu katika jina la Bwana wetu Yesu Kristo aliye hai, siku nyingine tena mpya kabisa Bwana ametupa kibali cha kuiona. Karibu tujifunze kwa pamoja yale yanayoweza kutusaidia katika usomaji wako wa biblia.
Sio kila neno unaweza kulisikiliza na kulibeba, sio kila mtu unaweza kumsikiliza anayoyazungumza na ukafuata kile anakuelekeza, sio kila mtu anayekuja mbele yako kutaka umpe muda wako umsikilize utakuwa una muda wa kutosha wa kumsikiliza.
Kuna muda unapaswa kusikiliza ukiona haifai unaweza kuachana nayo, lakini isifike wakati ukaona kila mtu hana cha maana anachoweza kuzungumza kwako. Yapo mambo mengi sana tunajifunza kwa kusikiliza mawazo ya wengine, na yapo mambo tunaweza kujifunza kwa kusoma mawazo ya wengine waliyoandika kwenye vitabu vyao, blog zao na majarida yao mbalimbali.
Unachopaswa kujua ni vitu gani unapaswa kuvisikiliza, na unapaswa kujua vitu gani unapaswa kuvifuatilia katika maisha yako. Kama umeamua kufuatilia mambo yanayohusu habari za Mungu, utapaswa kuwasikiliza watumishi wa Mungu mbalimbali, upaswa kusoma mafunzo yao mbalimbali ili ujifunze zaidi.
Wengi wamezama kwenye shimo la kutosikiliza wengine, anachoamini yeye au alichomezeshwa ndani yake hana muda wa kujua wengine wanasema nini juu ya kile anaamini. Wote tunajua Neno la Mungu ndio huwezi kusema linasema uongo hata kama litaenda kinyume na vile unaamini wewe, itakubidi ujilazimishe kuliamini na kuacha imani potofu uliyokuwa nayo.
Katika Neno la Mungu unaloliamini, wapo watu Mungu amewapa neema ya mawazo mapana zaidi juu ya Neno lake. Upana huu wa mawazo umekuja kwa kutafakari zaidi kuhusu yale wanayojifunza kwenye Neno la Mungu. Kwenye kutafakari kunazalisha vitu vingi sana kwa undani zaidi, na kuwa na uwezo wa kuletewa lile Neno la Mungu katika mazingira halisi tunayoishi sasa.
Tofauti na mtu anayesoma biblia alafu hana muda wa kutosha wa kutafakari yale aliyojifunza siku husika, sio siku husika tu hata pale anapokuwa kwenye mizunguko yake ya kawaida. Kumtafakari Mungu kupitia Neno lake kwake ni kawaida kabisa, na imekuwa kama maisha yake.
Ukifuatilia pia wote wanaotumia Muda mwingi kumtafakari Mungu mioyoni mwao, mara nyingi huwa hawalemewi na majaribu mazito katika maisha yao, mara nyingi huwa hawarudishwi nyuma kiimani na changamoto wanazopitia.
Siku zote wanapofika mahali pagumu, kimbilio lao huwa kwa Mungu wala hawana muda wa kusumbuana na watu wengine. Kilio chao huwa kwa BABA yao aliye mbinguni, maana wanajua yeye pekee anaweza kuwasaidia hata kama wengine watashindwa kuwapa msaada.
Siku ya leo nazungumza kuhusu kusikiliza wengine, ipo faida kubwa sana kuruhusu kuwasikiliza wengine. Vyema ukasikiliza hata kwa dakika chache anachosema aliye mbele yako, ukiona anachosema sio sahihi kwako, hapo ndio una uwezo wa kumweleza kwa nini huwezi kuendelea kumsikiliza ama ukaondoka bila kumwambia.
Hapo utakuwa umejua yeye ni mtu wa namna gani kuliko kujiwekea mipaka ya kutomsikiliza yeyote anayetaka kusema na wewe. Kwanza ukimsikiliza inakupa nafasi zaidi kujua hupaswi kumpa nafasi nyingineya kumsikiliza kutokana na upotofu alionao. Pia inakupa nafasi zaidi ya kujua mtu yule ana vitu vizuri vya kukusaidia kukua katika eneo unalohitaji kukua.
Leo wengi wanakataa kusikiliza kuhusu habari za kusoma Neno la Mungu, wakisikia mtu anazungumza kuhusu biblia. Wanasema waachie hiyo kazi walioenda vyuo vya biblia, waachie wachungaji/maaskofu, walimu, wainjilisti, mitume na manabii. Mshirika wa kawaida kama wanavyojiita wao, wanaona hawezi kuisoma biblia na akaielewa. Bila kujua Roho Mtakatifu yupo ndani yake kumsaidia hayo yote.
Ikiwa yote niliyokueleza hapa yamekupa changamoto kuyaelewa, naomba uondoke na hili moja tu, na naomba unisikilize hata kama huwa huna hiyo tabia ya kusikiliza wengine. Ujumbe wangu kwako ni kukuomba hili, Neno la Mungu liwe chakula chako cha kila siku, iwe asubuhi, iwe mchana, iwe jioni, iwe usiku, iwe kiangazi na iwe masika. Hakikisha hili halitoki moyoni mwako, Neno la Mungu ni chakula chako cha kiroho na kimwili.
Narudia tena kwa kusema, nisikilize hili, Neno la Mungu liwe chakula chako cha kila siku. Ni moja ya chakula chenye kila ladha unayoijua na usiyoijua wewe, hakichoshi wala hakikinai siku zako zote utakazokuwa unakitumia.
Bila shaka umepata kitu cha kukusaidia kuboresha baadhi ya maeneo ambayo uliyachukulia kawaida. Pale umeona unahitaji kuparekebisha, hebu jitahidi kufanya hivyo, ili uondoke kwenye huo uchanga.
Mungu akubariki sana kwa kutoa muda wako kusoma ujumbe huu, endelea kutembelea mtandao wetu wa chapeotz.com kwa masomo mengine mazuri zaidi.
Fb: Chapeo Ya Wokovu,
Email: chapeo@chapeotz.com,
Blog: www.chapeotz.com
WhatsApp: +255759808081.