Nakusalimu katika jina la Bwana wetu Yesu Kristo aliye hai, siku nyingine tena mpya kabisa Bwana ametupa kibali cha kuiona. Ikiwa jana tulilala na changamoto zetu ngumu, na leo Mungu ametupa pumzi ya uhai tena anayo sababu njema kwetu.

Unapotafuta kusogea hatua nyingine kihuduma au kibiashara au kimasomo, lazima kuna watu watatumika kama daraja kukusogeza hiyo hatua. Kweli Mungu anaweza kutusaidia kusogea hatua moja kwenda nyingine, ila mara nyingi sana ametumia wengine kutusogeza mahali tunapostahili kufika.

Unaonekana huduma yako ipo vizuri ni kwa sababu Mungu anaweka mizigo ndani ya watu wengine waweze kuibeba kimaombi na kifedha. Hata wakati Mariam amebeba ujauzito wa Yesu Kristo, kuna mama alipewa mzigo wa kuombea ujazito ule kwa miezi yote tisa mpaka akajifungua salama.

Unafikiri Mungu anashindwa kufanya mambo moja kwa moja bila kuwaambia wengine wakubebe? Mungu anaweza kabisa kufanya hivyo. Ila utaratibu wake ndivyo ulivyo. Ndio maana tuliona kunguru alitumika kumlisha mtumishi Elia.

Unafikiri Yesu Kristo alikuwa hawezi kushuka mzima mzima bila kupitia tumbo la Mariam, alitumia binadamu wa kawaida kabisa anayemcha yeye kuja kutukomboa wanadamu. Jambo lingine unaweza kufikiri alikuwa hawezi kutukomboa akiwa huko huko mbinguni, tunarudi kule kule kuwa mawazo yetu wanadamu sio mawazo yake Mungu.

Unafikiri yule mwanamke Kahaba aliyejulikana kwa ukahaba wake, Mungu alishindwa kuwaongoza watumishi wake wakahifadhiwe mahali pengine? Rahabu ndiye aliyetumika kuwahifadhi watumishi wale, akapata nafasi ya kuokoa maisha yake na familia yake. Kwa yale maangamizo ya Mungu.

Mungu hutumia mtu mwingine aliye juu au aliye na kidogo kumnyanyua aliye chini, hata kama unamwona mtu ni dhaifu kwa macho ya mwili. Kile kidogo alichonacho kinaweza kutumika kumsaidia mwingine asiye nacho kabisa.

Unapojifunza kwa kusikiliza mawazo ya walioshindwa kile unataka kukiendea/kukuishi. Uwe na uhakika utavunjwa moyo kwa kujazwa sumu nyingi sana, ambazo zinaweza kukuondoa kwenye mpango wako wa kuanza hicho ulichopanga kukifanya.

Wengi wanaoanza kusoma Neno la Mungu wanakuwa wamezungukwa sana na walioshindwa kusoma Neno la Mungu. Marafiki zao wengi hawasomi Neno la Mungu, wala hawana mpango kabisa kuhusu hilo jambo la kusoma Neno la Mungu.

Wanapozungukwa na kundi la namna ile, wanajikuta wanaomba ushauri kwao walioshindwa, wanajikuta wanaiga jinsi wanavyoishi. Wanasahau aliye chini kumnyanyua mwenzake aliye kaa chini kama yeye, ni ngumu sana wasipoamua kutoka kwenye udhaifu wao.

Ukitaka kufanikiwa kwenye eneo lolote lile katika maisha yako, unapaswa kupata waliokuzidi nguvu kidogo ili waweza kukubeba wewe uliye dhaifu. Lazima atokee mmoja wapo aliyejaa ujasiri mkubwa ndani yake kuwasaidia wengine.

Unapoendelea kung’ang’ana na marafiki wanaoendelea kukufanya uwe chini, ni wewe umeamua kuwa hivyo. Lakini kama u mhitaji wa kusogea hatua fulani kiroho, lazima Mungu angeshakupa marafiki wazuri na ungekuwa tayari kuwapokea.

Ili ukue na uone mafanikio kwenye eneo la usomaji wa Neno la Mungu, hakikisha unajifunza kwa waliofaulu katika eneo hilo. Tafuta mtu mmoja wa kumwangalia mbinu anazotumia kusoma Neno la Mungu, ikiwezekana uliza, ukiona kuuliza itakuwa ngumu fuatilia mafundisho yake.

Usiendelee kujifariji na walioshindwa, tafuta walioshinda au wale walio na kiu ya kushinda. Usitafute ambao hawana mpango wa kushinda, wala usitafute wale waliojaribu wakashindwa. Waachie watafiti wa mambo waje wajue nini kiliwafanya washindwe au subiri ufanikiwe kwanza na ukomae vizuri, ndipo uje kujifunza vitu kwao walioshindwa.

Ambatana na wasomaji wa Neno la Mungu, kuwa karibu nao muda mwingi kadri unapopata nafasi ya kufanya hivyo. Chukua mazuri yao yanayoweza kukuimarisha kwenye usomaji wako wa Neno la Mungu.

Mungu akubariki sana kwa kutoa muda wako kusoma ujumbe huu, endelea kutembelea mtandao wetu wa chapeotz.com kwa masomo mengine mazuri zaidi.

Unaweza kutupata kupitia;
Fb: Chapeo Ya Wokovu
Email: chapeo@chapeotz.com
Blog: www.chapeotz.com
WhatsApp: +255759808081