Nakusalimu katika jina la Bwana wetu Yesu Kristo aliye hai. Baba yetu ni mwema sana, ametupa kibali kingine tena cha kuiona siku ya leo. Sifa na utukufu tumrudishie yeye Bwana mwenza wa yote.

Huwa nina ratiba ya mazoezi kila siku jioni, nisipobanwa sana na shughuli zangu, huwa najitajidi angalau nipate dk 40 au lisaa limoja la mazoezi ya mwili. Licha ya mazoezi kuwa ni muhimu sana kwa mwili wa binadamu, binafsi ninayapenda kutoka moyoni, nimeanza mazoezi rasmi tangu mwaka 2006/2007.

Pamoja na kuyapenda na kujiwekea ratiba ya jioni, kuna wakati najikuta nimebanwa sana na kuamua kutokwenda. Na kuna wakati sijikii kabisa kufanya mazoezi ila najikuta najisukuma kwa nguvu, nikifika tu kwenye chumba cha mazoezi. Nitafanya tu na nitaondoka nikiwa nina furaha kabisa, nasahau ile hali ya uchovu niliyoingia nayo.

Naweza kujipa sababu za kutokwenda mazoezi, muda mwingine ni uzembe tu nauruhusu, lakini kadri ninavyozidi kujipa sababu unakuta wakati mwingine namaliza mwezi sijaenda kushiriki mazoezi. Kinachokuja kunisaidia kurudi kwenye mazoezi na nisiache moja kwa moja ni ile kupenda mazoezi kutoka moyoni bila kulazimishwa na mtu.

Muda mwingine naweza nisiende sehemu ya mazoezi, nikafanya nyumbani kwa kutumia vifaa vyangu binafsi. Kwa sababu sio sheria mpaka nifanye mazoezi ni lazima niende sehemu maalum, kinachoangaliwa ni mazoezi huwa nafanya tu japo sifanyi kama tungekuwa kundi.

Nikirudi kwenye moyo wa somo hili, unaweza kuona napenda mazoezi ila muda mwingine nafanya kama jambo la ziada sana. Kama umesoma vizuri hayo maelezo, utaona naweza acha muda fulani bila kujali sana alafu baadaye nakuja kurudi tena na kuendelea na ratiba zangu za mazoezi.

Nataka ujifunze kitu hapa ili uweze kudaka kile nimekusudia ukielewe kwa kina, ukiangalia huo mfano hai wa kitu ninachofanya. Unaweza ukahamasika na wewe leo ukaanza mazoezi, alafu baada ya muda mfupi ukaona hilo jambo ni gumu kwako ukaamua kuacha kabisa.

Nimeona wengi sana nikiwambia naelekea kwenye mazoezi, na yeye atakuambia na mimi nitaka kwenda. Atakuja kweli siku mbili tatu. Akija kuona mwili unamuuma siku za mwanzo, si unajua kama hujauzoeza mwili mazoezi ya aina fulani lazima upate maumivu. Baada ya hapo ndio utaona unazoea na kufurahia kile unafanya.

Wengi wetu tunalinganisha usomaji wa Neno la Mungu kama mazoezi fulani anayejisikia kufanye afanye, na asiyejisikia kufanya asifanye. Ndio maana wengi ukiwaambia habari za kusoma Neno la Mungu, wanahamasika sana siku za mwanzo. Akija kukutana na vikwazo viwili vitatu anaona ya nini kuendelea kusoma Neno la Mungu.

Mwingine ameokoka kweli, anaona hana shida kabisa na Neno la Mungu, kama ni kujazwa na Roho Mtakatifu amejazwa vizuri tu, kama ni kuhubiri anaweza akahubiri vizuri tu, kama ni kuimba anaweza kuimba vizuri tu maana anayo sauti nzuri kabisa ya kuimba.

Anachoona yeye kusoma Neno la Mungu ni jambo la muhimu sana ila sio lazima sana kwake, anaweza kusoma leo akaja kusoma wiki ijayo. Au wakati mwingine anamaliza mwezi mmoja au miwili kabisa hasomi, anakuja kushtuka alikuwa na zoezi la kujisomea Neno la Mungu, hapo ndio anaanza tena kusoma.

Sawa na mimi napenda jambo lingine la kujisomea vitabu mbalimbali, napenda sana kusoma vitabu ila sio jambo ambalo nimeliweka sana kipaumbele. Naweza kusoma wiki hii kidogo, wiki ijayo nisisome kabisa, na wala siwezi kujisikia vibaya sana kama nisiposoma Neno la Mungu.

Kinachotutesa wakristo wengi tushindwe kuliweka moyoni suala nzima la kusoma Neno la Mungu, ni kulifananisha hili jambo na mfano wa mazoezi niliokutolea, ni kulifananisha na vitabu vingine nilikutolea mfano wake. Mtu akijiona amechoka na shughuli za kutwa nzima, anaona bora apumzike kusoma Neno la Mungu, bila kujua anapopumzika anapoteza kabisa mwelekeo wake.

Vipo vitu vinaweza visiwe lazima sana katika maisha yako yaani ni sawa na kusema kwamba sio lazima sana ule chakula muda ule ule uliozoea kula. Unaweza kuvusha muda wa kula na isiwe tatizo kwako au unaweza kufunga, ila huwezi kuacha kula pamoja na kutokula muda uliojipangia.

Neno la Mungu ni muhimu sana na lazima kwa mkristo yeyote yule, ni rahisi sana kuanguka dhambini na ukapotelea humo kwenye hiyo dhambi. Kwa sababu utakuwa unaonywa utaona unafuatiliwa, utaona watu wamekosa kazi za kufanya ndio maana wanakufuatilia wewe. Wakati ni tofauti kabisa na mtu anayesoma Neno la Mungu, atakuwa amepikwa kwa namna ambayo anakuwa msikivu sana na mtiifu na mwepesi wa kujirudi.

Wakati mwingine huhitaji kuhuburiwa ndipo ujue jambo fulani ni dhambi kwako kulifanya, Neno la Mungu linakufundisha lenyewe, linakuonya lenyewe, linakukemea lenyewe, linakupa tahadhari lenyewe. Huhitaji kusimamiwa mbele yako uambiwa acha hilo, usifanye hilo ni baya kwako.

Vizuri ukakumbuka hili ninalokuambia hapa, vipo vitu usipovifanya kila siku havina madhara kwako, ila kuna vitu ukivipa mwanya wa kutovifanya. Utajikuta umeacha kabisa, na ile bidii yako utashangaa inapotea kabisa. Maana unachofanya shetani anajua kabisa kina faida na manufaa makubwa kwako na yeye atashindwa kukuingia kirahisi akakupotoshe.

Kusoma Neno la Mungu kwangu ni lazima na wala sisomi kama starehe na siwezi kujihurumia, kuandika ujumbe kama huu wa kukumbusha umhimu wa kusoma Neno la Mungu pia kwangu ni lazima wala siwezi kujihurumia. Haya mambo mawili siyafanyi nikisijikia kufanya, niwe najisikia au niwe sijikiii, lazima nisome Neno la Mungu na lazima niandike. Ikitokea siku sijafanya haya, nitaugua moyoni sana na siku yangu itakuwa na mapungufu makubwa mno.

Tamani na wewe kufikia kiwango kikubwa cha kutokubali kusoma Neno la Mungu kama jambo la ziada sana kwako, weka mkakati wa kukusaidia kuboresha utaratibu wako wa kusoma Neno la Mungu.

Mungu akubariki sana kwa kutoa muda wako kusoma ujumbe huu, kazi yangu ni kuhakikisha unaelewa umhimu wa kusoma Neno la Mungu. Ninachokuomba ni hili, usiache kutembelea mtandao wetu wa chapeotz.com hapa utapata masomo mbalimbali ya kukufanya uone uzito wa Neno la Mungu kwa kina zaidi.

Nakutakia siku njema iliyojaa ulinzi wa Mungu.

Facebook: Chapeo Ya wokovu

Email: chapeo@chapeotz.com

Blog: www.chapeotz.com

WhatsApp: +255759808081.