Nakusalimu katika jina la Bwana wetu Yesu Kristo aliye hai, siku nyingine tena mpya kabisa Bwana ametupa kibali cha kuifikia. Sifa na utukufu tumrudishie yeye Bwana mwenza wa yote kutupa fursa ya kuifikia siku hii.

Tunaweza kuharibika masikio yetu kwa kusikiliza vitu ambavyo vingine havina faida kubwa sana kwetu, vinaweza kuonekana ni vizuri lakini uzuri wake unaweza usiwe na maana kama tutakuwa tunapuuzia mambo mengine ya msingi.

Mtu anaweza kumaliza siku nzima ameweka head phone masikioni mwake, kitu anachofuatilia ni vipindi vya radio station. Anaweza kuwa anafuatilia kitu kizuri kabisa, ila hakiwezi kuwa kizuri kiasi kwamba kikamaliza masaa yote kwa siku. Basi tunaweza kusema huenda kuna jambo fulani lilimfanya siku hiyo asikilize radio station siku nzima, lakini haiwezi kuwa kila siku.

Labda awe amejiariwa kwa kazi hiyo ya kusikiliza kila kipindi kinachorushwa hewani. Vinginevyo kama haujaajiriwa alafu unafanya hivyo, tutakuona umekosa kiasi.

Mwingine anakuwa anasikiliza nyimbo, anaweza kuweka head phone kuanzia mkoa mmoja mpaka anafika mkoa mwingine. Yeye ni kusikiliza nyimbo tu, inawezekana ikawa tabia yake ya kila siku, akiwa huru kidogo utamwona amechomeka nyaya kwenye masikio yake.

Watu hawa ukiwagusa siku zote watakuambia hawana muda wa kusoma Neno la Mungu, wanazo audio bible kwenye smartphones zao. Lakini hawana muda wa kusoma Neno la Mungu kwa njia ya kusikiliza, ila wanao muda wa kusikiliza mengine. Ila Neno la Mungu kwao wanakuwa hawana muda kabisa.

Huenda ni kwa sababu ya kukosa maarifa ndio maana wengi wanangamizwa, wakati mwingine tunashindwa kupata mawazo kama haya kutokana na kutoruhusu mawazo yetu yafikiri namna ya kutumia vifaa tulivyo navyo kumtukuza Mungu.

Mungu ameweka hazina kubwa sana ndani yetu ya akili, lakini cha ajabu hatuzitumii hizo akili. Badala yake tunazitumia kwenye vitu vingine bila kuwa na kiasi katika matumizi yake, kusikiliza nyimbo za injili au kusikiliza audio za mafundisho mbalimbali ya watumishi wa Mungu. Sio kosa kabisa kufanya hivyo, ila uwe na kiasi katika matumizi ya muda wako.

Unalalamika kila siku huna muda wa kusoma Neno la Mungu, wakati unatumia masikio yako kusikiliza mambo mengine. Ambapo ungeweza kutumia kifaa chako hicho hicho kusikiliza na kusoma Neno la Mungu kwa njia ileile.

Hata kama upo jikoni unapika, unaweza kusoma Neno la Mungu kwa njia ya sauti na ukapata kitu. Huku unaendelea na shughuli zako, tena unaweza kurudia mara nyingi uwezavyo, ukitoka hapo una kitu umekijaza ndani ya moyo wako.

Siku unakuwa na muda wa kushika biblia yako, fanya hivyo kwa uaminifu mkubwa kabisa. Maana kwenye biblia yako napo kuna faida zake unapoisoma tofauti na ile ya kusikiliza tu usichokiona, unaposoma kuna maeneo unaweza kuweka alama za kukusaidia siku nyingine iwe rahisi kuona mistari ile uliyoona itakufaa kuitumia.

Nakusihi sana, upo kwenye foleni kama za jiji la Dar es Salaam, Tanzania. Unapaswa kuzitumia hizo foleni za masaa mengi barabarani kusoma Neno la Mungu, wakati watu wanalalamika foleni kubwa wewe unaendelea kupata chakula cha kiroho. Mpaka unashuka kwenye gari, unakuwa umevuna mambo mengi sana mazuri ya kukufanya uendelee kuona uwezo wa Mungu juu ya maisha yako.

Huenda huko nyuma hukujua haya yote, ila sasa umejua kupitia mafundisho haya. Hakuna kusingizia tena upo bize, huwezi kushika biblia yako, kuanzia leo unaweza kuishika kwa masikio yako mwenyewe. Ukasoma mistari ya kutosha, na ukapata muda wa kutosha wa kutafakari yale uliyojifunza.

Mungu akubariki sana kwa kutoa muda wako kusoma ujumbe huu, endelea kutembelea mtandao wetu wa chapeotz.com kwa masomo mengine mazuri zaidi.

Ahadi yangu kwako ni kuhakikisha unaelewa umhimu wa kusoma Neno la Mungu, maana ukielewa hili unajiweka salama zaidi kutompa nafasi shetani akulaghai. Pia unakuwa na ujasiri zaidi mbele za Mungu kumwomba jambo lolote akusaidie maana tayari unakuwa unayo imani thabiti.

Nakutakia siku njema.

Facebook: Chapeo Ya Wokovu

Email: chapeo@chapeotz.com

Blog: www.chapeotz.com

WhatsApp: +255759808081.