Nakusalimu katika jina la Bwana wetu Yesu Kristo aliye hai, siku nyingine tena mpya kabisa Bwana ametupa kibali cha kuweza kuiona. Nafasi kwetu kwenda kumzalia Bwana matunda yaliyo mema, pia ni nafasi kwetu kwenda kutubu pale tuliporudi nyuma kwa matendo maovu.

Juhudi zako ni njema sana mbele za Mungu, pamoja na unakutana na changamoto ngumu sana. Usikubali kurudi nyuma kamwe, bali songa mbele zaidi kuhakikisha unafikia viwango ulivyopenda kuvifikia.

Wengi wetu tumeanza kuelewa kuhusu umhimu wa kusoma Neno la Mungu, lakini pamoja na kuelewa hili jambo lina umhimu mkubwa sana. Bado wengi wetu tunajaribu kusoma lakini hatuchukui muda tunakuwa tumeishia njiani.

Tukiulizwa sababu hasa iliyotufanya tushindwe kuendelea kusoma Neno la Mungu, tunakuwa hatuna sababu ya msingi sana inayotufanya tuonekane hatuwezi tena kusoma Neno la Mungu. Sana mtu akikupa sababu ni ile ya kusema sina muda wa kutosha kusoma Neno la Mungu, wakati huo unamkuta anafanya vitu ambavyo vinampotezea muda wake mwingi.

Kuna maeneo huwa tunaacha mlango wazi ndio maana tunajikuta tunarudishwa nyuma sana, yapo maneno mengi sana ya kuvunja moyo. Utasikia kila neno la kukufanya unachofanya hukupaswa kukifanya, mwingine atakuambia, wa kusoma Neno la Mungu ukaelewa utakuwa wewe!!

Uwe na uhakika kama hukujipanga vizuri kiufahamu, utaanza kuona ile bidii yako ya mwanzo inazidi kutoweka taratibu. Maana ile sauti itakuwa inaimba ndani mwako, hasa pale unapojisikia kuchoka, utaisikia zaidi ikinong’ona ndani yako.

Unaweza kufika maeneo fulani, na yenyewe yakawa kikwazo kwako. Ambapo hayo maeneo yatapaswa utumie akili yako ili yasiwe kikwazo kwako cha kukuzuia usisome Neno la Mungu. Hapa pia inategemea sana ile kiu yako ya kusoma Neno la Mungu, kiu yako ina nguvu ya kupangua vikwazo vilivyosimama mbele yako kukuzuia usisome Neno la Mungu.

Kwa kuwa wewe umekuwa na utaratibu wa kusoma Neno la Mungu ama umeanza utaratibu wa kusoma Neno la Mungu siku za karibuni. Nakuomba usikubali mtu yeyote kukuvuta nyuma, hata kama ulikuwa na rafiki yako mnaenda naye kwa pamoja ila yeye akaacha. Usikubali na wewe kuacha, zaidi endelea kuweka bidii yako katika kusoma Neno la Mungu.

Huenda huyo aliyeacha kusoma Neno la Mungu alikuwa ni mtu wako wa muhimu, aliyekushawishi kuwa na utaratibu wa kusoma Neno la Mungu. Hilo lisikupe shida, alitumika kama daraja kwako sawa ila kama ameamua kuacha na wewe umejaribu kumrejesha hataki. Wakati mwingine amekuambia maneno ya kukufanya na wewe uache mpango wako wa kusoma Neno la Mungu, huyo sio mtu mwema tena kwako.

Atabaki kuwa Mungu alimtumia kukufanya uwe karibu naye kwa njia ya kusoma Neno la Mungu, ila kama shetani amemtawala na kuona haifai tena kuendelea kusoma Neno la Mungu. Kazi yako ni kumwombea kwa Mungu aondoe roho mbaya ya uvivu iliyomwingia ndani yake.

Nasema usikubali kuvunjwa moyo, utakutana na vikwazo vingi sana katika usomaji wako wa Neno la Mungu. Ila iwe funzo kwako kuwa bora zaidi, changamoto unazokutana nazo hakikisha unaziona kama daraja lako la kusogea ng’ambo zaidi.

Zipo sehemu unapaswa kuzifikia ila zina mito mikubwa na ili uvuke unapaswa kupata kifaa cha kukuvushia. Katika kuhangaika huko na kule kupata kifaa cha kukuvushia, unaweza kukutana na changamoto ngumu sana. Ila usije ukakata tamaa, bidii yako ya kusoma Neno la Mungu ni ya maana kubwa sana.

Mungu akubariki sana kwa kutoa muda wako kusoma ujumbe huu, endelea kutembelea mtandao wetu wa www.chapeotz.com kupata masomo mengine mazuri zaidi ya kukusaidia kukua zaidi katika usomaji wako wa Neno la Mungu.

Unaweza kutupata pia kwa;

Facebook: Chapeo Ya Wokovu

Email: chapeo@chapeotz.com

Blog: www.chapeotz.com

WhatsApp: +255759808081.