Nakusalimu katika jina la Bwana wetu Yesu Kristo aliye hai, siku nyingine tena mpya kabisa Bwana ametupa kibali cha kuiona. Sifa na utukufu tumrudishie yeye Bwana mwenza wa yote kutupa fursa hii adimu.
Wengi wetu huwa tunafanya vitu pasipo kuwa na picha ya miaka 5 au 10 au 20 ijayo itakuwaje, kama tutaendelea kufanya au kuishi na kile tulichochagua kukikifanya sehemu ya maisha yetu. Mara nyingi huwa tunaangalia furaha ya muda mfupi kuliko ya muda mrefu, mtu anachagua kitu ambacho moyo wake unakataa kabisa ila kwa sababu anataka kuuridhisha mwili wake, anaamua kufanya.
Mtu anakuwa kama vile amefungwa ufahamu wake asiweze kuona mbele, anakuwa kama anatembea gizani kwa kupapasapapasa. Anakuwa kipofu kabisa asiyejua kuna nini mbele yake, kwa sababu tu hana taa/tochi ya kumlika mahali alipo na anapoelekea.
Giza hili ni kutokuwa na maarifa sahihi ya Neno la Mungu, tunapokosa maarifa ya Neno la Mungu. Tunakuwa kwenye giza kinene sana, ninaposema giza kinene au giza torotoro, ujue ni giza kweli sio utani.
Nikapata nafasi ya kuzungumza na ndugu yangu mmoja katika Kristo, akaniuliza jambo fulani kuhusu maamzi aliyotaka kuyafanya kwenye maisha yake ya ujana. Na mimi sikumkwepesha jibu la swali lake kutokana na jinsi alivyoniuliza, binafsi nilishangaa mno nilivyomweleza akaniambia kwa jinsi ulivyonipa jibu naachana kabisa na haya maamzi niliyotaka kuyafanya. Sababu haswa ya kuacha, ametazama picha ya maisha yake yajayo akaona hatakuwa na furaha kwa maamzi yaliyotaka kuyafanya Leo.
Sikuwa mchoyo kumweleza kile nilikiona ndani yake, nilimwambia moja kwa moja, umeanza kuiva kiroho na hatua uliyonayo weka bidii zaidi kufikia viwango ya juu zaidi. Nilimwambia hivyo kwa sababu kuu tatu, kwanza sijawahi kukutana na kijana wa jinsia yake mwenye ujasiri mkubwa namna hiyo. Ambaye alishafanya makosa akagundua kosa lake akaamua kujirudi upya bila kujali maumivu atakayopata. Pili amekuwa na uwezo kuisikiliza amani ya moyo wake zaidi kuliko kuangalia hali ya mazingira yake ya sasa. Na tatu ameona picha ya miaka 10 au 20 au 30 ijayo hatakuwa na furaha na hicho alichotaka kufanya maamzi leo.
Unaweza kusema alikuwa na uhakika gani kama atafikia miaka yote hiyo, unaweza ukawa sahihi kufikiri hivyo ila hayo sio mawazo ya mtu mwenye imani. Mwenye maono na aliyebeba kusudi la Mungu ndani yake, lazima alitimize kwanza ndipo Mungu aweze kumwondolea uhai wake.
Unaweza kusema hufanyi vitu vikubwa kwa kuhofia kifo, cha ajabu utakutwa na uzee wako hujafanya chochote zaidi utabaki unahangaika na maisha yako. Kile ulichoogopa kufanya kwa kufikiri utakufa kesho, unashangaa hujafa na miaka uliyoiona ipo mbali sana imefika ukiwa mzima kabisa.
Ndugu yangu, Neno la Mungu linaondoa watu kwenye uchanga wa kiroho, Kadri unavyozidi kujifunza Neno la Mungu ndivyo unavyozidi kufunguka zaidi kiufahamu. Unakuwa na akili zinazofikiri sawasawa maana tayari takataka nyingi zimeondolewa ndani yako, na hii haitokei bahati mbaya ni juhudi zako ndio zinakufikisha kiwango hicho.
Nimekutolea mfano wa ndugu huyu, japo sijakuambia ilikuwa ni kitu gani ila elewa hatua aliyonayo huyu ndugu ni kubwa sana. Maana kwa jinsi nilivyomsikiliza ushuhuda wake baada ya kumaliza kumshauri, alikiri mwenyewe kilichomfanye awe hivyo ni Neno la Mungu.
Raha iliyoje kupata picha ya maisha yako, bila shaka ni raha kubwa sana. Hofu na mashaka ya kufikiri itakuwaje nikiacha hili na kuanza lingine, inakuwa haipo kabisa maana walio ndani ya Kristo hawana hofu na kesho yao. Ukiona una hofu sana na kesho yako, ujue uhusiano wako na Mungu upo mbali, umeokoka sawa ila huna Neno la Mungu la kutosha moyoni mwako.
Mpaka hapo umepata kuona jinsi gani Neno la Mungu linavyoweza kumlika maisha yako ya sasa na ya baadaye. Hakuna gharama ya kutoa ili ujifunze Neno la Mungu, gharama yake ni kutenga muda wako kila siku. Tenga muda wa kusoma na kutafakari Neno la Mungu, hakuna njia ya mkato kwa hili.
Mungu akubariki sana kwa kutoa muda wako kusoma ujumbe huu, endelea kutembelea mtandao wetu wa www.chapeotz.com kupata masomo mengine mazuri zaidi. Je unahitaji kujiunga whatsApp group ili kuwa na wenzako wanaosoma Neno la Mungu kila siku? karibu sana uwasiliane nasi kupitia namba +255759808081(tumia whatsApp tu)
Siku yako ya leo ikawe njema.
Chapeo Ya Wokovu
chapeo@chapeotz.com
www.chapeotz.com
+255759808081.