Nakusalimu katika jina la Bwana wetu Yesu Kristo aliye hai, siku nyingine tena mpya kabisa Bwana ametupa kibali cha kuiona. Sifa na utukufu tumrudishie yeye Bwana mwenza wa yote, atupaye uzima kila siku.

Mkulima mara nyingi anapolima, huwa hana asilimia mia moja kama kile alicholima kinaweza kufikishwa na mvua mpaka mwisho au kinaweza kisifikishwe na mvua mpaka mwisho. Yote mawili yanaweza kutokea kutokana na hali ya hewa itakavyokua msimu huo, lakini pamoja na kutokuwa na asilimia zote bado mkulima yule atakuwa na bidii ya kulima.

Ana imani hata kama mvua itamkwamisha, bado kuna kitu atakipata kupitia kazi yake aliyofanya. Huyu ni mkulima anayelima mazao akitegemea kuvuna zaidi kwa kile alichokipanda shambani.

Yapo mashamba mengine hayaonekani sanaa kama mashamba ila huwa tunapanda tukitengemea kuvuna kitu. Tunaposoma Neno la Mungu kila siku maana yake kuna kitu tunategemea kukivuna kupitia usomaji wetu. Hutosomi ilimradi tunasoma, tunasoma tukiwa na malengo mazuri kabisa.

Ukisoma ilimradi tu unasoma, hutokuwa na kitu unacholenga kukipata kupitia usomaji wako wa Neno la Mungu. Lakini mtu anayesoma Neno la Mungu kwa kutegemea kuvuna vitu vya kumjenga kiroho na kimwili, lazima atakuwa makini na anachokifanya.

Unaposoma Neno la Mungu tegemea kuvuna kama utakuwa unamaanisha kwa kile unafanya, huu sio utani ni ukweli mtupu. Neno la Mungu sio kama mkulima anayelima huku anakumbuka mwaka jana nililima lakini mazao yote yaliungua kwa jua. Neno la Mungu kadri unavyozidi kujifunza ndivyo unavyozidi kupanda vitu ndani yako. Ambavyo unaweza usione matokeo yake wakati unaanza, ila kuna siku utaona kwa uwazi kabisa matunda yalivyo mengi.

Ndio maana hili jambo unapaswa kulifanya kwa bidii sana, wakati wa kuandaa shamba mpaka kufikia kiwango cha kupanda mazao alafu urudi upalilie, ni wakati wa maumivu makubwa. Ila wakati unavuna matunda/mazao ya kile ulichopanda, ni wakati wa furaha kubwa sana.

Hupotezi muda wako unaposoma Neno la Mungu, unaweza kuona hivyo kutokana labda umeanza kufanya hili zoezi muda sio mrefu. Lakini kwa yule aliyeng’ang’ana kila siku kuhakikisha anaulisha moyo wake Neno la Mungu. Mtu wa namna ile huwezi kumsukuma wala huwezi kuanza kumsihi asome Neno la Mungu, yeye mwenyewe anajua wajibu wake na atatekeleza hilo mara moja.

Mwanzo nimesema hakuna kusema kuna kupata na kukosa, kusoma Neno la Mungu kupo kupata tu. Labda wewe uamue tu kuacha ila ipo faida kubwa sana kwa mtu aliyetoa muda wake kujisomea Neno la Mungu. Hasara itakuja pale unapolifanya suala la kusoma Neno la Mungu ni jambo la ziada sana, na shida ya kulifanya jambo la ziada ni kupuuza hata usiposoma utaona ni sawa tu.

Nategemea kukuona ukiongeza umakini zaidi kuliko jana, hakikisha usomaji wako wa Neno la Mungu unakuzalia matunda mema. Ifike wakati ukiri kwa kinywa chako mwenyewe kuwa Neno la Mungu limekuondoa hatua fulani ya uchanga wa kiroho na kukufikisha hatua fulani ya ukuaji wa kiroho.

Mavuno ni mengi sana na mazuri kwa mtu anayewekeza kwenye kusoma Neno la Mungu, mengine unaweza kuyaona ni akili zako kumbe ni matunda ya kazi unayoifanya. Uzuri wa mtu aliyekomaa kiroho, na anayependa kujifunza zaidi, kuna vitu vingi sana anavifanya mpaka unabaki unashangaa hii akili anaitoa wapi.

Usifike hatua fulani ukaacha kusoma Neno la Mungu, mkulima hata akivuna mazao mengi sana. Msimu wa kulima ukifika utamwona shambani tena, na wewe usianze kuhesabu ulilima sana kipindi kilichopita haina haja tena kuendelea kulima. Nakwambia utaanza kulia njaa muda sio mrefu.

Mavuno ni mengi yanakusubiri wewe uchukue hatua.

Chapeo Ya Wokovu

chapeo@chapeotz.com

www.chapeotz.com

+255759808081.