Nakusalimu katika jina la Bwana wetu Yesu Kristo aliye hai, siku nyingine tena mpya kabisa Bwana ametupa kibali cha kuiona. Tunaendelea kusema Yesu ni Bwana kwa matendo mema na wengine wanaendelea kumkana Yesu Kristo kwa matendo yao mabaya. Vizuri kuhakikisha mahusiano yako na Mungu wako hayapotezwi kizembe na hali yeyote ile.

Uliokoka kwa gharama kubwa mno, usikubali kirahisi kurudishwa nyuma kwenye matendo maovu, kataa kabisa hali hiyo. Utakapokubaliana na udhaifu wa namna hiyo, utajitengenezea ukuta ambao ukija kutaka kuruka ili urudi tena ulipokuwa. Unaweza kujikuta unajisikia aibu badala ya ujasiri wa kumrudia Mungu wako, au unaweza kuona huwezi tena kumwona Mungu akikutumia kama mwanzo katika maisha yako, kutokana na dhambi ulizofanya.

Baada ya kusema hayo, karibu katika somo letu la leo tuweze kujifunza yale muhimu yaliyopaswa tujifunze siku ya leo. Tuliza mawazo yako ili uweze kudaka kile kilipangwa kwako, usipotuliza mawazo yako kwenye somo hili unaweza kutoka mtupu na utakuwa umepoteza muda wako bure. Na mimi sipendi upoteze muda wako kwa kitu ambacho hutovuna chochote, bora usisome kabisa ujumbe huu, unaweza kuishia hapa ukaendelea na shughuli zako zingine.

Nimekaa natafakari hili jambo, nimeona linaimba sana moyoni, nikapata msukumo wa kukushirikisha na wewe. Najua kuna kitu kipya kinaenda kutengenezeka au kuzaliwa kwako kwa upya, baada ya kusoma na kutafakari haya ninayokwenda kukueleza hapa.

Sijui sana kama tunapenda kuendelea kukua zaidi ya jana, ile bidii yetu tuliyokuwa nayo awali iendelee kutuzalia matunda zaidi. Tuone utofauti wa mwezi au mwaka uliopita na sasa tulipo ni tofauti kiasi gani, utofauti wake ni vile tulikuwa na uchanga fulani wa kiroho. Na sasa tulipo tunaona tumekua kwa hatua kubwa sana, ikiwa na maana hatupo tena kwenye ule uchanga.

Tunajua wote, sio mara zote unaweza kujijua una uchanga eneo fulani, huwa mara nyingine tunajiona tupo sawa. Ila tukishatoka kwenye hiyo hali ndio tunajigundua tulikuwa na mapungufu fulani, inakuwa inatufarahisha na kututia moyo kadri tunavyosonga mbele.

Sawa na mtu anayeanza masomo yake ya sekondari, anaona kidato cha kwanza ni kigumu sana. Ila akishasogea kidato cha pili, anaona cha kwanza kilikuwa kirahisi zaidi kuliko cha pili, vivyo hivyo cha tatu, cha nne, cha tano na cha sita. Muda mwingine ugumu tunauona kwenye darasa husika ila tukishasogea tunaona ilikuwa sio gumu sana kama tulipo sasa. Na muda mwingine tunatengeneza ugumu wa kitu ambacho hatujakifikia bado, ukishakifikia unaona zile hadithi nyingi za kushindwa huzioni tena.

Unaweza kujikuta unaingia na bidii kubwa ya kushinda ule ugumu ulioambiwa, kweli kabisa bidii yako inakusaidia kufikia eneo fulani zuri kabisa. Ukija kuona matokeo mazuri yanakuja kutokana na bidii yako, hutokumbuka haraka kilichokufanya ufikie hapo ambapo ilikuwa ni ile kujituma kwako. Badala yake unasahau kufanya kwa bidii, unakuja kujikuta umeporomoka na kurudi chini kabisa.

Wengi walianza wokovu kwa bidii kubwa sana baada ya kuambiwa na kusikia wokovu ni mgumu sana, waliingia na nguvu kubwa. Ile bidii yao iliwafikisha mahali pa kubwa sana bila wao kujua, baadaye wakaanza mazoea na kuacha kuweka bidii.

Matokeo yake wamechoka sana na hawana mpango wa kutoka katika uchovu huo. Kama walikuwa na hamu ya kurudi walipokuwa wangefanya juhudi ya kurudi kama awali. Lakini wamezoea wokovu, pamoja na kuzoea wamechoka sana.

Hawaumii kwanini hawana hamu ya kuomba tena, hawaumii kwanini hawana hamu ya kwenda kwenye vipindi vya kanisani, hawaumii kwanini ule moyo wa kutoa fedha zao kuwepeleka watumishi wa Mungu kuhubiri injili, hawaumii kwanini hawana moyo wa kujitoa kwenye shughuli mbalimbali za kanisa na jamii.

Mbaya zaidi hawaumii kwanini hawana ule moyo wa kusoma Neno la Mungu, wamebaki na kusema hawana muda, wamebanwa na majukum. Wamesahau ile bidii yao ya awali, bidii iliyowaletea matunda mema, bidii iliyowatambulisha kile Mungu ameweka hazina ndani yao. Walikuwa na majukum yale yale ila sasa wanayaona yanawabana.

Wengine wamenyonywa bidii yao na ndoa zao, wengine wamenyonywa bidii yao na kazi zao, wengine wamenyonywa bidii yao na biashara zao, wengine wamenyonywa bidii zao na wachumba/wapenzi wao, wengine wamenyonywa bidii na watoto wao. Na vyote hivyo vipo ndani ya uwezo wa Mungu, nikiwa na maana anaweza kuwaondolea wakabaki weupe.

Pamoja na kujua hayo yote, bado hatuna mpango wa kupambana kurudi kama mwanzo. Maana tungekuwa tunaendelea na bidii yetu, tungejikuta tunasukumwa kwenda mbele zaidi wala tusingekuwa na haja ya kutamani vya nyuma. Tunakuja kujiona nyuma tulikuwa tunafanya vizuri zaidi baada ya kupoteza ile bidii yetu.

Hebu siku ya leo, mwambie Yesu Kristo nirejeshe bidii yangu, kwa kutubu makosa yako. Rudi pale ulipoteleza, kile kilianza kukufanya uache kuweka akili zako kwenye mambo ya Mungu, hakikisha unapaweka sawa. Haiwezekani kazi hiyo hiyo, biashara hiyo hiyo, maisha yale yale ya ndoa wanayoishi wengine na bado wanampa Mungu muda, wewe imekuwa kitanzi kwako.

Lazima ufike mahali ujihoji, bidii yako ya kusoma Neno la Mungu imeenda wapi, sio kusoma tu. Yaani huna hata ile hamu ya kufanya chochote, umebaki mkristo wa jpili/jmosi tena wa kwenda kwa kujisukuma ilimradi uonekane na wewe ulihudhuria ibada. Ukifika hata ile hamu ya kuomba huna, kuimba ndio usiseme.

Chukia sasa hali ya kuchoka, ndio umechoka na umefika wakati umekata tamaa. Ndio maana umekuwa na sababu nyingi za kushindwa kujishughulisha na mambo ya Mungu, sasa imefika wakati wa kusema IMETOSHAAA… piga kelele kwa nguvu zote kutoka ndani ya moyo wako.

Mungu aendelee kukupa haja ya moyo wako, akusimamie mipango yako yote, na ukijiunganisha naye vizuri. Mambo yako hayatakaa yaharibika mpaka ufike mahali upotezee mwelekeo, wewe ni mtoto wa mwenye miliki zote duniani na mbinguni. Ondoa mashaka.

Mungu akubariki sana kwa kutoa muda wako kusoma ujumbe huu, nina imani umepata kitu cha kukusaidia katika maisha yako. Endelea kutembelea mtandao wetu www.chapeotz.com kupata masomo mengine mazuri zaidi kadri Roho Mtakatifu atakavyotuongoza.

Nikutakie wakati mwema.

Facebook: Chapeo Ya Wokovu

Email: chapeo@chapeotz.com

Tovuti: www.chapeotz.com

WhatsApp: +255759808081