Nakusalimu katika jina la Bwana wetu Yesu Kristo aliye hai, siku nyingine tena mpya kabisa Bwana ametupa kibali cha kuweza kuiona. Lipo kusudi maalum la mimi na wewe kumzalia Bwana matunda yaliyo mema siku ya leo.

Wote najua tumekutwa na hali hii mara nyingi, huenda hujawahi kujua kama huwa unapatwa na hali hii. Ila leo naenda kukumbusha ujue huwa unaipotezea wapi hiyo hali unayoipata ndani yako. Ili ujue cha kufanya, kuepuka kujipa maneno alafu baada ya hapo unasahau.

Umewahi kuona upo kanisani, mchungaji akahubiri ujumbe unaogusa maisha yako moja kwa moja. Yaani moyoni unashuhudiwa ujumbe ule ni wa kwako moja kwa moja, unajiahidi kubadilika kabisa.

Unaweka mipango mizuri ya kuanza kuchukua hatua kwa kile ulichopanga uanze nacho, lakini unapotoka nje ya kanisa. Unasahau yote na kama hujasahau unaona ile hamasa imefutika kabisa, hujui kimetokea nini ila unajikuta huna hamu tena ya kuchukua hatua.

Wakati mwingine sio kanisani tu, unaweza kukutana na ujumbe wa kusoma kama huu au ukakutana na kitabu chenye mafunzo mazuri, ukaguswa kweli kweli. Ukajiambia unabadilika na kuanza kuchukua hatua kwa yale uliyoona una mapungufu nayo.

Ukija kuacha kusoma kile ulikuwa unasoma, utashangaa humalizi hata siku nzima. Ile nguvu ya uthubutu iliyokujia kwako inakupotea kabisa, au inabakia kwa mbali sana, ambapo haichukui hata wiki moja inakuwa imepotea kabisa.

Mwingine anaweza kumwona mwenzake anavyofanya, akapata mwamko/hamasa ndani yake. Anashindwa kujizuia anaamua kumuuliza anafanyaje mpaka kufikia hatua ile, na yule mtu anakuwa sio mchoyo anamwambia kila hatua anayopaswa kupitia. Wakati mwingine anapewa na angalizo kubwa ambalo litamsaidia asikate tamaa atakapokutana na changamoto ngumu.

Lakini pamoja na hayo yote, watu hujikuta wamerudia maisha yao ya kale. Na wengine wanakuwa hawajaribu kabisa, yaani huwa wanaishia kuhamasika na kubaki nayo moyoni bila kuchukua hatua yeyote. Tunaweza kusema wanahamasika na kuchukua hatua ndani yao, na kujikatisha tamaa humohumo ndani kabla hata hawajathubutu kufanya.

Umewahi kukaa ukafikiri hili? Hili linakujaje? Najua utakuwa umekumbuka mengi uliyowahi kuhamasika nayo. Ila hukumbuki yaliishia wapi, au mara nyingi ukienda kanisani mchungaji akisimama huwa anakugusa sana kwenye masomo anayotoa. Kinachokupelekea ushangae ni kwanini huwa mtu wa kuhamasika tu ila kwenye matendo/vitendo huwa unafeli kabisa.

Chukulia umeonywa kuhusu dhambi fulani, na unajua kabisa hiyo dhambi unaitenda. Unatubu na wakati mwingine unatoka mbele kwenda kuombewa, ila ukishatoka nje ya kanisa. Zile ahadi na mikakati uliyojiwekea ya kutorudia hilo kosa, unajikuta unalirudia tena.

Labda unajiwekea kuanzia leo naacha uvivu wa kutohudhuria kanisani, kuanzia leo naacha kunywa pombe kwa siri, kuanzia leo naacha kutembea na wake/waume za watu, kuanzia leo naacha tabia mbaya ya kujichua sehemu za siri, kuanzia leo naacha tabia ya kutokusoma Neno la Mungu, kuanzia leo naacha kabisa kuchelewa kanisani, kuanzia leo naacha kabisa tabia kutokuomba, kuanzia leo naacha kabisa tabia ya kusema uongo, na kuanzia leo naacha kabisa tabia ya kutazama picha/video za ngono.

Unajiwekea mikakati hiyo ya kuacha tabia hizo baada ya kuguswa na ujumbe uliokutana nao siku hiyo. Lakini baada ya muda fulani unajishangaa umerudi pale pale kwenye tabia yako uliyojiwekea mikakati na mchungaji alikuombea siku hiyo, ukatoka umejiapia hutorudia tena.

Lakini pamoja na kujiapia, unarudia yale yale. Unajua ni nini kinakufanya urudie yale yale au ubakie pale pale? huna nidhamu binafsi. Unapohamasika siku ya kwanza unakuja kukosa ule mwendelezo wake, ambapo ungekuwa na nidhamu binafsi ingekusaidia kujipa hamasa mwenyewe. Hata pale unapovunjwa moyo, utahakikisha unaendelea na kile uliamua kukiishi.

Kama ulijiwekea kuanzia leo utakuwa unasoma Neno la Mungu, huhitaji kusimamiwa tena kukumbushwa hili. Unakuwa wewe mwenyewe unajisukuma na kujihamasisha mwenyewe bila kutegemea mtu mwingine aje akuhimize kufanya. Unabaki unatafuta maarifa ya kukuwedhesha kuimarisha usomaji wako, ila tayari ndani yako una nidhamu binafsi inayokusaidia kukusukuma kufanya au kutokufanya kile kisichokustahili.

Kuna vitu huwezi kusimamiwa kila unapoenda, unahitaji nidhamu yako binafsi. Ukishakuwa na nidhamu yako, ni rahisi kwako kujihamasisha kwa kile ulichoamua kukiishi au kukifanya au kutokifanya.

Unaweza kutafuta wahamasishaji wa kila aina, unaweza kutafuta manabii, mtume, maaskofu, wachungaji na waalimu wakuombee na wakusaidie kutoka kwenye udhaifu ulionao. Hutotoka Kamwe kwenye kifungo hicho kama hutoamua mwenyewe, unahitajika wewe kama wewe kudhamiria toka moyoni mwako.

Unao uwezo mkubwa sana ndani yako, hamasa iliyo ndani yako inakutosha kabisa. Sema hujajiua uwezo ulio ndani yako, kwa kuwa umejifunza hapa, anza kujitafuta mwenyewe, hakikisha yale unayopenda yawe kwako. Unachukua hatua kweli, acha maneno, kuwa mtu wa vitendo ukiamua jambo fulani liwe kwako amua kweli. Hata kama watu watasimama watakuambia huwezi, sema kimoyomoyo unaweza na baada ya muda fulani waone kweli umeweza.

Mungu akubariki sana kwa muda wako, naamini kusoma kwako hapa kumekuletea faida kubwa. Hayo ndio matunda ya mtu anayependa kujifunza, ninachokusihi usiache kusoma Neno la Mungu.

Nakutakia wakati mwema.
Facebook: Chapeo Ya Wokovu
Email: chapeo@chapeotz.com
Tovuti: www.chapeotz.com
WhatsApp: +255759808081.