Nakusalimu katika jina la Bwana wetu Yesu Kristo aliye hai, umeianzaje siku yako. Unaifurahia au unaona kama isingefika siku ya leo, kama huoni kuifurahia nikuombe uifurahie hii siku maana ina maana kubwa kwako. Hata kama imejaa changamoto nyingi na ngumu, hakikisha unaendelea kujiunganisha na uwepo wa Mungu, uhusiano wako na Mungu uendelee kuwa karibu zaidi.
Kuna vitu ambavyo huwa sitamani kuvikisikia siku zote za maisha yangu, vitu hivyo ni pamoja na kuonekana zamani nilikuwa vizuri sana kwa mambo ya Mungu. Ila sasa nimechoka sana na sina ile bidii tena ya mambo ya Mungu.
Naweza kuwa simtendi Mungu dhambi yeyote, ila kujituma kwangu kwa mambo yanayomhusu Mungu. Nakuwa nyuma sana, naweza kujua kwanini nilirudi nyuma ila nikashindwa kurudi tena kama kipindi cha nyuma.
Hii inaweza kuwa imewakuta wakristo wengi sana, wengi walikuwa wamesimama kweli. Huenda miongoni mwao walikufanya na wewe uokoke, au walikufanya uwe na bidii kwa mambo ya Mungu. Badala yake wameacha ile bidii yao ya awali, usipokuwa makini unaweza kupoa kama wao maana moto ulionao ulitokana na kuhamasishwa na wao.
Mambo ni mengi sana na kila kukicha kunaibuka changamoto mpya, hayo yote yasikubadilishe na kukutoa kwenye ile bidii yako. Unaweza kubanwa sana na shughuli ila hakikisha hizo shughuli hazikuondolei bidii yako, kubali umebanwa ila ukipata hata lisaa limoja litumie kisawasawa. Unaweza kujishangaa unafanya vizuri zaidi kuliko hata ukiwa uhuru au ukiwa na nafasi.
Mwendo uliokuwa unaenda nao wa kusoma Neno la Mungu, hakikisha huo mwendo unauboresha zaidi. Na sio uzidi kuchakaa bali uzidi kuwa imara zaidi na bora zaidi, aliyekuona miezi 3 iliyopita akuone leo upo vizuri zaidi ya mwanzo alivyokuona. Sio akuone hicho kipindi ulikuwa vizuri zaidi kuliko sasa, epuka sana hilo.
Wengi wetu tulianza vizuri kabisa, tabia ya kusoma Neno la Mungu ilitukaa vizuri sana ila tumefika mahali tumezoea, na mazoea hayo yametupelekea kuchoka sana. Mazoea yale yametutoa kabisa kwenye sifa ya mtu mwenye bidii, imebaki historia ulikuwa hivi na vile, unaweza kufikiri kipindi kinachoongelewa ulikuwa kijana na sasa u mzee sana. Kumbe bado u kijana au unazo nguvu zilezile za mwanzo.
Hakikisha unazidi kwenda mbele zaidi, ili ufanikiwe hili ni kuithamini sana siku yako. Unapofanya jambo lifanye kwa kumaanisha haswa, haijalishi mazingira uliopo, fanya kutokana na mazingira yako ila iwe kwa bidii sana. Isionekane mazingira yalikupunguzia kasi yako ya usomaji wako wa Neno la Mungu.
Narudia tena, usije ukaonekana zamani ulikuwa umesimama vizuri kuliko sasa, usije ukaonekana zamani ulikuwa siriaz na mambo ya Mungu kuliko sasa. Epuka sana hali hii, sio lazima awepo mtu wa kuja kukuambia sasa hivi umepoa, jipekue mwenyewe kabla wengine hawajaanza kutafuta kilichokumaliza/kilichokurudisha nyuma.
Fika mahali uone ulivyokuwa unafanya mwaka jana, iwe kichekesho kwako maana utajiona ulikuwa unafanya kwa kiwango cha chini sana kutokana uchanga wako. Japo wakati huo ulionekana upo vizuri sana, ila wewe jione ulikuwa upo chini sana ukijilinganisha na sasa ulivyo.
Usikubali udhaifu wa aina yeyote ukuvute nyuma, hakikisha unasonga mbele zaidi bila kujali mambo yanayokupata kwenye safari yako ya wokovu. Nitakushangaa umekutana na changamoto unaacha na kusoma Neno la Mungu, wakati unayo macho na uelewa wa kusoma ukaelewa.
Si unajua wasiopenda kulijaza Neno la Mungu mioyoni mwao, asilimia kubwa tabia zao huwa zipo vilevile. Hata kama ana tabia fulani mbaya, itaendelea kuwepo kwa sababu hana maarifa ya kuibadili hiyo tabia. Lakini wale wanaopenda kulijaza Neno la Mungu mioyoni mwao, hawatabiriki kabisa, leo unaweza usipendezwe na tabia fulani mbaya. Ila kesho ukafurahishwa zaidi na tabia nyingine nzuri, na ile mbaya ikawa haipo tena.
Mungu akubariki sana kwa kutoa muda wako kusoma ujumbe huu, naamini umejifunza mengi ya kukufanya usonge mbele na sio urudi nyuma. Usiache kutembelea mtandao wetu www.chapeotz.com kupata masomo mengine mazuri zaidi.
Nakutakia siku njema.
Facebook: Chapeo Ya Wokovu
Tovuti: www.chapeotz.com
Email: chapeo@chapeotz.com
WhatsApp: +255759808081.