Nakusalimu katika jina la Bwana wetu Yesu Kristo aliye hai, unaweza kuhuzunika sana vile vile unaweza kulia sana. Lakini jua maisha bado yanaendelea mbele, dunia haiwezi kuacha kuzunguka katika mhimili wake kwa sababu wewe unapitia wakati mgumu. Maisha yanaendelea mbele na unapaswa kulielewa hili, ili usiwe mtu wa kuvunjwa moyo haraka na vitu vidogo vidogo vya kupita.
Wakati mwingine huwa tunaonekana waoga wa kufanya mambo kutokana na kutochukua hatua kwa vitu fulani, ama kutokana na kukaa kimya, ama kutokana na kujifanya wajinga kwa mambo fulani kuyaacha yapite wakati yanaonekana ya msingi kwa wengine.
Kweli kabisa inaweza kuwa ni tabia ya uoga/hofu imemvaa mtu ndani yake, anajua kabisa hawezi kuchukua hatua fulani kutokana na sababu anazoona yeye. Mwingine anaweza kujitutumua kwa maneno ya mdomoni ila moyoni mwake amejaa hofu na mashaka makubwa.
Ukweli halisi mara nyingi anaujua mhusika mwenyewe, japo anaweza kujulikana kwa kumtazama usoni. Jinsi anavyozungumza unaweza kujua huyu amejaa uoga/hofu, jinsi anavyotenda unaona kabisa hofu/uoga umemtawala mtu huyu/yule.
Hofu na uoga, vyote vipo ndani ya mwanadamu kwa kazi maalum. Mungu alitengeneza hivi vyote kwa kazi maalum, ila usipokuwa makini vinaweza kutumika kwa matumizi yasiyo halali. Matumizi yasiyo halali ni kuogopa kufanya vitu vya msingi visivyomchukiza Mungu, kuogopa kufanya vitu vitakavyokusaidia miaka 5 au 10 au 20 ijayo.
Wengi wetu inapofika eneo hili, huwa tunachanganya hofu/uoga kutokana na mtu kushindwa kufanya kama tulivyotegemea sisi afanye. Tunamwona hajiamini yeye mwenyewe kabisa kwa jinsi tunavyomtazama au tunavyomchukulia sisi.
Inawezekana kabisa anayeonekana hajiamini, ila anawashinda ujasiri wa kuthubutu mambo makubwa wale wanaomwona ni mwoga. Uwezakano upo wale wanaomwona mwenzao ni mwoga, wao wenyewe ndio waoga ila hawajijui kuwa ni waoga kutokana na ujuaji wao.
Nataka kusema nini hapa, ninachotaka kusema ni kwamba, kadri unavyozidi kukomaa kiroho. Hata kufikiri kwako mambo kubadilika kabisa, hata uchukuaji wako wa hatua unakuwa umejaa umakini mkubwa. Hutochukua hatua kuwafurahisha watu, utachukua hatua kuangalia faida na madhara ya kutochukua hatua.
Unakuwa unajua matokeo ya jambo kwa kiasi fulani, kutokana na kanuni za kiasili, mfano hai; unajua kabisa kukanyaga waya wa umeme ulioaguka kunakupelekea kifo. Wewe unajitoa ufahamu kwa sababu huwa sio mwoga, unakanyaga huo waya unakutana na shoti ya umeme unakufa, wakati ulikuwa na uwezo wa kukwepa huo waya ukaendelea na safari yako.
Wachanga wa kiroho wanaweza kuwa na tabu kubwa sana kutokana na kuwa ngumu kwao kujitambua kama wana shida ndani yao. Wanaweza kuwaona wengine wanakosea kumbe wao ndio wanakosea, wanaangalia sana matokeo ya upande mmoja bila kuangalia matokeo ya upande wa pili.
Neno la Mungu linasaidia sana, linakupa stamina za kuweza kukabiliana na changamoto ngumu. Ambazo watu wengine walijua hutoweza kuzinasua, ila kutokana na maarifa uliyoyajaza moyoni mwako. Unakuwa na uwezo wa kuyachuja mambo kwa kina, na yale yasiyofaa kwa wakati huo yanamezwa na maarifa yaliyomo ndani yako.
Vile vile Neno la Mungu linakupa uwezo wa kuwa na maamzi yanayojitegemea pasipo kusubiri watu wengine wakuamlie jambo. Wote tunajua ni vizuri kusikiliza ushauri wa wengine, ila sio kila jambo litahitaji muda wa wengine. Litakuhitaji wewe kama wewe ulitolee maamzi muda ule ule.
Vizuri ukajenga tabia imara zaidi ya kupenda kusoma Neno la Mungu bila kukoma, maana kadri unavyozidi kukomaa kiroho ndivyo unavyozidi kukaa mbali na mitego ya mwovu shetani. Uchanga wetu wa kiroho mara nyingi umetuingiza kwenye mitego ya mwovu shetani bila kujijua, tukijua tupo sahihi kumbe tunamkosea Mungu wetu.
Vizuri ukayajua haya ili unaposoma Neno la Mungu, ujue kuna vitu vingi utaepukana navyo kwa sababu ya usalama wako. Na kuna vitu utajitoa kwa ajili ya usalama wa wengine, bila kuangalia matokeo ya upande mmoja.
Usalama wetu upo katika kulijua Neno la Mungu, unaweza kuona kama vile hujui unachofanya, au unaweza kuona unachofanya hakina faida yeyote. Ila nakwambia leo, Neno la Mungu limekuepusha na mambo mengi sana pasipo wewe kujua kama ndio lenyewe limekusaidia hayo.
Ukomavu wa kiroho unaletwa na Neno la Mungu, jisukume zaidi katika usomaji wako wa Neno la Mungu. Siku zote utakuwa mtu wa faida kwako na kwa wengine wanaokuzunguka.
Mungu akubariki sana kwa kutoa muda wako kusoma ujumbe huu, endelea kutembelea mtandao wetu www.chapeotz.com kupata masomo mengine mazuri zaidi ya kukujenga kiroho.
Nakutakia siku njema.
Facebook: Chapeo Ya Wokovu
Tovuti: www.chapeotz.com
Email: chapeo@chapeotz.com
WhatsApp: +255759808081.