Haleluya, nakusalimu katika jina la Bwana wetu Yesu Kristo aliye hai.
Kuanza kuchoka mambo ya Mungu, unaweza usijue haraka kwa wakati huo. Mwanzo unaweza kujiona umebanwa sana na majukum, ukasahau siku za nyuma ulikuwa umebanwa ila ulikuwa na muda wa kumpa Mungu.
Wachache sana wanajitambua mapema wanavyoenda sio kwa viwango vyao, hawa mara nyingi ni wale wanaopenda kutathimini njia zao. Wanakaa chini kujichunguza mwendo walioanza nao upo vile vile na kuongezeka zaidi au kuna mahali umepungua, na unazidi kupungua zaidi.
Wengi huwa hatuna tabia ya kujitathimini, ndio maana mambo mengi sana tunakuja kushtuka wakati yameharibika au yamepoa kabisa. Ambapo kuja kuyarudisha kama mwanzo, inakuwa kazi kubwa sana.
Kuepukana na hili, vizuri ukajenga tabia ya kujitathimini kila mara. Hakikisha una utaratibu mzuri wa kujitathimini kila mara, utaona mapungufu mengi sana ambayo utakuwa na uwezo wa kuyafanyia kazi kabla hajakupeleka pa baya.
Kuishi bila kujitathimini kwa unalofanya, ni rahisi sana kuangushwa au kurudishwa nyuma au kupoa kabisa au kuleta mazoea zaidi yakakubaribia. Unaposahau ile bidii yako ya mwanzo, ni dalili za mtu aliyepoteza ile kiu iliyokuwa inamsukuma kufanya kila anafanya.
Kuna vitu vinaweza kuonekana ni vilevile, na vinakuja kwa mtindo/muundo uleule, na kweli vinaenda kwa utaratibu ule ule kama ulivyovikariri. Mfano unaweza kujenga utaratibu wa kufanya jambo fulani ifakapo muda fulani, kama utakuwa umeweka nidhamu binafsi. Watu wote wanaokuzunguka watajua tu hata bila kuwaambia, watajua huyu akifika muda fulani anafanya jambo hili.
Labda hujanielewa, hujawahi kusikia mtu akisema mtu fulani akifika muda fulani anakuwa kichaa au anakuwa na homa kali au anaanguka au anapita njia hii. Kwa sababu tu hilo jambo limejirudia kwake muda ule ule zaidi ya mara moja, kujirudia hivyo linazoeleka na watu.
Hata wapita njia/barabara, wanaona njia ni ile ile wanayopita. Mazoea yale yanaweza kuwa mazuri kwa sababu wanajua sehemu fulani huwa kuna shimo na sehemu fulani huwa kuna mlima na mteremko mkali.
Mazoea yale yanaweza kuleta umakini mkubwa kwenye sehemu anazozijua zina shida, pia mazoea yale yanaweza kuleta shida pale anapoondoa umakini kwa kujua kote hakuna shida isipokuwa mahali fulani. Kumbe shida ipo palepale kwenye sehemu aliyoona hakuna tatizo lolote.
Kufahamu jambo fulani ni kuzuri sana, ila kumbuka kuweka mazoea yakazidi kipimo ni hatari kwako. Kufahamu jambo fulani kukusaidie kwenda mbele zaidi, kukusaidie kufika haraka unapoelekea, na kukusaidie kutokosea mahali unaenda.
Tabia hizi za mazoea ya kupitiliza zinawavuta wengi nyuma hadi kwenye huduma zao, mwanzo unamwona mtumishi alikuwa anaenda vizuri sana. Ila baada ya muda fulani anakuwa amepoa kweli, usifikiri amerudi nyuma kiimani. Hajamwasi Mungu ila ameingiza mazoea na wakati mwingine amechoka, na kuchoka kule anaona mambo ya Mungu ni yale yale.
Mazoea haya yameingia hata kwa wasomaji wa Neno la Mungu, mwanzo wanakuwa vizuri sana. Wanakuwa na bidii na kujituma haswa, na ule msemo wa Neno la Mungu ni jipya kila siku, wanakuwa wanaufahamu sana. Ila baadaye wanausahau na kuona maneno ya Mungu ni yale yale hakuna jipya wanalojifunza.
Ukiona umefikia hatua kuona Neno la Mungu ni lilelile wala hakuna jipya unalojifunza, na wakati mwingine umejiona huna tena muda wa kusoma Neno la Mungu. Ujue kuna shida imekuvaa, kubali ukatae, jua umepoteza ile kiu ya neno la Mungu.
Neno la Mungu haliwezi kupoteza hamu, yaani unaweza kulisikia mara nyingi uwezavyo na ukapata mambo mengi mazuri zaidi. Kadri unavyozidi kujifunza ndivyo unavyozidi kufunguka zaidi, hakuna kusema mambo ni yale yale.
Usije ukafika hatua ukaona hakuna jipya unalopata ndani ya biblia, alafu ukaridhika na hiyo hali. Vizuri kuikataa hiyo hali mapema iwezekanavyo maana muda sio mrefu inakupeleka pa baya.
Furahia Neno la Mungu, sikia kujifunza zaidi kadri unavyokutana na habari ile ile iliyoelezewa kitabu kingine. Isiwe kero kwako, maana Mungu kusema na wewe kupitia Neno lake haiwezi kuwa kero bali ni furaha kwako.
Mungu akubariki sana kwa muda wako.
Facebook: Chapeo Ya Wokovu
Tovuti: www.chapeotz.com
Email: chapeo@chapeotz.com
WhatsApp: +255759808081.