Nakusalimu katika jina la Bwana wetu Yesu Kristo aliye hai, Mungu wetu ni mwema sana ameendelea kutupa pumzi ya uhai wake. Haijalishi jana ulilala na hali gani mbaya, na hajalishi jana ulilala ukiwa na hali gani nzuri sana, wote tumeamka na tumeiona siku ya leo.

Unaweza kufikiri wale wanaopuuza sana mambo ni watu wasiojua kabisa hasara za kufanya hivyo. Unakuta ni watu wanaojua kabisa hasara ya kupuuza jambo, na wanaojua faida ya kutopuuza hilo jambo.

Tofauti kabisa na yule aliyekuwa hajui chochote kuhusu kutofanya jambo fulani, anapokuja kugundua alikuwa anakosea na akapata maelekezo ya namna ya kufanya hilo alilokuwa halifanyi. Inakuwa rahisi sana kwake na mara nyingi wanakuwa ni watu wazuri sana wanapoamua kubadilika.

Tofauti na anayejua alafu hafanyi, anabaki anajivunia kujua kwake umhimu wa jambo huku hathubutu kulifanya kabisa. Unashindwa kuelewa kama ni jambo la muhimu sana, mbona yeye halifanyi alafu anawahimiza wengine walifanye.

Wengine hawana nafasi za kuhimiza wengine wafanye, ila anapopata nafasi ya kuzungumza na wenzake anaonekana ni mtu anayeelewa mambo mengi sana. Unakuja kuchoka pale utakapomwona pamoja na kuelewa mengi kuhusu hilo jambo, yeye mwenyewe ndio anakuwa mvivu kuliko yule asiyejua chochote.

Ikiwa tunajua umhimu wa jambo alafu tukawa hatuchukii hatua yeyote, itakuwa haina maana yeyote kwetu kujua. Kujifariji na uelewe tulionao kuhusu jambo fulani, haiwezi kutufanya tuonekane tunajua sana. Bali inaweza kutusaidia kubishana na watu, ila ukweli unabaki mioyoni mwetu kuwa tunachokifanya hakina faida yeyote.

Tabia hii ndio imevaa sana wakristo walio wengi, wanahimizwa kila siku umhimu wa kusoma Neno la Mungu lakini pamoja na kuhimizwa huko hawathubutu. Na wengine wanaamua kuchukua hatua za kusoma Neno la Mungu baada ya muda fulani wanaacha kabisa, wanabaki na ile harufu ya kusimlia waliwahi kujaribu miaka ya nyuma ila wakaacha.

Kitu kama unajua umhimu wake alafu ukawa hukifanyi kama yule asiyejua umhimu wowote kuhusu hilo jambo. Huna tofauti yeyote na asiyejua, ila shida ipo kubwa kwako unayejua alafu hutaki kufanya kabisa.

Ni sawa na mtu anayejua kufanya jambo fulani ni dhambi na maandiko matakatifu yanakataza, lakini yeye akawa anaendelea kufanya pamoja na kujua kwake ni dhambi. Mtu wa namna ile neema ya Mungu isipoingiliana kati, umauti unaweza kumkuta akiwa kwenye dimbwi la dhambi maana ni mgumu kuambilika.

Asiyejua chochote kuhusu umhimu wa kusoma Neno la Mungu, siku akikutana na somo linaloeleza vizuri umhimu wa kusoma Neno la Mungu. Mtu yule akisema kuanzia sasa nakuwa msomaji wa Neno la Mungu kweli anakuwa vile vile, maana alichokitamka kinatoka ndani ya moyo wake.

Changamoto inapokuja kwa huyu aliyekuwa hajui chochote kuhusu umhimu wa kusoma Neno la Mungu, ni kurudi kwake nyuma pale anapoingiza mazoea kwa kile alichoanza kukifanya. Huyu anakuwa kwenye lile kundi la anayejua umhimu/faida za kufanya jambo fulani Lakini akawa halifanyi.

Kujua sana faida za kusoma Neno la Mungu, alafu ukawa sio msomaji wa Neno la Mungu, huna unachopata kwenye kujua kwako kama hutaki kuchukua hatua ya kufanya kwa vitendo.

Acha maneno mengi, soma Neno la Mungu ili likae kwa wingi moyoni mwako. Kujifanya mjuaji sana, hakuwezi kukusaidia chochote kama hutokuwa msomaji wa Neno la Mungu. Neno la Mungu liwe chakula chako cha kila siku, usikie njaa ya kiroho kila siku, hakuna siku utakinai kula chakula cha tumbo, iwe pia kwenye Neno la Mungu.

Mungu akubariki sana kwa kutoa muda wako kusoma ujumbe huu, endelea kutembelea mtandao wetu www.chapeotz.com kupata masomo mengine mazuri zaidi.

Nakutakia siku njema.

Facebook: Chapeo Ya Wokovu

Email: chapeo@chapeotz.com

Tovuti: www.chapeotz.com

WhatsApp: +255759808081.