Haleluya,
Kitu kama hukifanyi na unaambiwa kila siku ukifanye, na unaelezwa sana umhimu wake ila unaona ni jambo la kawaida. Ni jambo la kushtusha kidogo watu wa Mungu.
Tunahimizwa sana usomaji wa Neno la Mungu, lakini wakristo wengi hatujali hili na tunalipuuza, tunasema tunampenda Mungu ila tunachukia maarifa yake sahihi. Upendo upi ambao tunasema tunampenda Mungu na wakati hatujishughulishi na kusoma Neno lake.
Umeokoka sawa, ni mtumishi wa Mungu sawa, mbona hujishughulishi na kusoma Neno la Mungu. Utapata wapi maarifa ya kukusaidia kushinda dhambi, utapata wapi maarifa ya kusema na wale wasiomjua Kristo.
Hebu tufike wakati tujitathimini kwa upya, kama hatuwezi kusoma Neno la Mungu. Lakini tunashinda vijiweni kuongea mambo mbalimbali kwa muda wa kutosha, kama tunashinda kwenye mitandao ya kijamii kwa muda wa kutosha. Je kipi kinatufanya tushindwe kutenga muda wa kutosha kusoma Neno la Mungu?
Tunakabiliwa na roho gani hiyo isiyopenda kutuona tukisoma Neno la Mungu? Ikiwa hatuna hamu na Neno la Mungu, tunaweza kumthibitisha vipi Mungu wetu kuwa tunampenda ikiwa hatutaki kujishughulisha na kutafuta maarifa yake aliyotuwekea ndani ya biblia yake takatifu.
Tunajaribu kukwepana pembeni na kushindwa kuambiana ukweli, ila mtu yeyote asiyesoma Neno la Mungu ana mapungufu mengi sana ambayo mengine yanamsababishia kuendelea kumkosea Mungu. Na watu wa namna hii ni wagumu kushauriwa waache wanachofanya kwa sababu wanajua wapo sahihi.
Ukristo usiopenda kutafuta maarifa sahihi ya Neno la Mungu, ukristo usiokuwa na kiu ya kusoma Neno la Mungu. Huo ukristo una walakini kwa mkristo huyo, haijalishi unajionaje ndani yako, kama huna hamu ya kusoma Neno la Mungu ujue kuna kitu sio kizuri kimekuvaa ndani yako.
Hujiulizi Kwanini watumishi wa Mungu hawaachi kusema kuhusu umhimu wa kusoma Neno la Mungu. Lakini pamoja na kukueleza hayo yote bado huna mpango wowote wa kusoma Neno la Mungu, ukianza kusoma Neno la Mungu ukikutana na ugumu kidogo unaamua kuacha.
Hatuendi hivyo na hatuwezi kufika, labda kwa yule asiyejua kabisa kusoma, na huyu anapaswa kutafuta njia ya kuweza kusoma Neno la Mungu. Anaweza kujifunza kusoma maana inawezekana, au anaweza kutafuta mtu anayemwamini awe anamsomea mahali anataka, au anaweza kutafuta Biblia ya sauti ambayo inapatikana play store.
Ndugu, umeokoka na huna mpango wowote wa kusoma Neno la Mungu. Kuokoka kwako kunaleta maswali mengi sana, chakula cha mtu aliyeokoka ni Neno la Mungu, ikiwa huwezi kula chakula cha mtu aliyeokoka na wala huna hamu nacho kabisa. Tunao uwezo wa kukuhoji unamwamini Mungu huyu wa kweli au una mungu mwingine nje na huyu?
Acha kujifariji unachofanya ni sahihi, kama husomi Neno la Mungu sio sahihi kabisa kwa mkristo mwenye safari ya kwenda mbinguni. Kusoma Neno la Mungu iwe ni sala yako ya kila siku, na kama huwa husali unahitaji kutafuta kitu ambacho lazima ukifanye kwa siku zaidi ya mara moja.
Tutaendelea kupenda ujinga hadi lini? Watu wasiopenda kujifunza maneno ya Mungu? Watu wanaoenda kama vile wamemaliza safari ya kwenda mbinguni. Tufike mwisho tuseme imetosha kufuga tabia mbaya tuliyonayo, tabia isiyopenda kujifunza Neno la Mungu.
Rejea:Enyi wajinga, hata lini mtapenda ujinga? Na wenye dharau kupenda dharau yao, Na wapumbavu kuchukia maarifa? MIT. 1:22 SUV
Mtu anayepaswa kuwa mstari wa kwanza kupenda maarifa ya Neno la Mungu ni wewe uliyeokoka, kama umeokoka na hupendi kabisa maarifa ya Neno la Mungu. Bila kukwepesha maneno utakuwa kwenye hili kundi;Enyi wajinga, hata lini mtapenda ujinga? Na wenye dharau kupenda dharau yao, Na wapumbavu kuchukia maarifa? MIT. 1:22 SUV
Himiza hili jambo la kusoma Neno la Mungu kwenye moyo wako, himiza hili jambo kwenye familia yako, himiza hili jambo kwa mume/mke/mchumba wako, himiza hili jambo kwenye kikundi chako cha kwaya, na himiza hili jambo kwenye kusanyiko lolote linalomwamini Yesu Kristo. Usinyamaze kimya unapopata nafasi ya kusema, usiache kusema, sema bila kukoma, rudia tena na tena kusema.
Usipende kuendelea kuwa mtumwa wa ujinga, penda maarifa ya Neno la Mungu utaona ukifunguka ufahamu wako, utaona unajiepusha na dhambi nyingi sana zilizojificha kwenye kutokujua kwako.
Mungu akubariki sana kwa muda wako.
Chapeo Ya Wokovu
chapeo@chapeotz.com
www.chapeotz.com
+255759808081.