Nakusalimu katika jina la Bwana wetu Yesu Kristo aliye hai, Mungu ni mwema ametupa kibali kingine tena cha kuweza kuiona siku ya leo. Sifa na utukufu tumrudishie yeye Bwana mwenza wa yote.

Kuna rafiki yangu mmoja nikawa namuuliza hivi, vipi ndugu mbona siku hizi sioni zile bidii zako za kumfuta Bwana kwa bidii. Maana wakati wa nyuma alikuwa yupo vizuri sana, sasa nikawa namkumbusha mambo ya nyuma alivyokuwa mtu wa maombi sana, alivyokuwa mtu wa kutulia muda mwingi akimtafakari Bwana, alivyokuwa mfuatiliaji mzuri wa mafundisho mbalimbali ya Neno la Mungu na vitabu mbalimbali walivyoandika watumishi wa Mungu.

Alichoniambia huyu rafiki, nisubiri atarudi tena upya. Nimerudia kumwambia zaidi ya mara moja kumtaka aone alipo sasa sio pazuri sana. Sikutaka kukaa na kitu moyoni mwangu, nilijua hata kama ninamuuliza kiutani utani kuna kitu namkumbusha ndani yake.

Huyo ndugu niliyemtolea mfano, alikuwa yupo vizuri kweli, ila sasa kapoa sana. Ukimuuliza anakuambia subiri nitarudi tu, atarudi lini! hilo siwezi kujua zaidi ya kumwombea tu. Maana kama ni muda unazidi kwenda huku hakuna dalili zozote zinaonyesha ameona umhimu wa kuyafanyia kazi yale niliyomweleza.

Wengi ndio wanavyojidanganya nitaanza kusoma Neno la Mungu siku sio nyingi, tangu mwaka unaanza alijaribu kidogo kusoma akaacha kwa kujiahidi atarudi muda sio mrefu. Mpaka leo tupo mwezi huu hakuna dalili zozote zinazoonyesha kuanza kusoma Neno la Mungu.

Wapo walijiahidi wakimaliza masoma yao, watakuwa na muda wa kutosha kusoma Neno la Mungu. Walivyomaliza shule/chuo wakabadilisha kauli, wakasema wakipata kazi watakuwa na utulivu na wataanza kusoma Neno la Mungu.

Wamepata hiyo kazi waliyokuwa wanaitafuta, wamebadilisha tena kauli na kuanza kusema wanabanwa sana kazini hawawezi kabisa kupata muda wa kutulia wasome Neno la Mungu.

Kumbuka hatua zote hizo zinaenda na muda, inaweza ikawa miezi, mwaka mpaka miaka. Alikuwa shule/chuo, akawa anasubiri apate kazi, na kazi akapata, na hapo kwa kila hatua kuna muda wake unapita yaani kuna muda wa kukaa shule/chuo, kuna muda wa kutafuta kazi. Na kuna muda wa kuwa kazini na kujiona amebanwa sana na shughuli hawezi kuwa na muda wa kusoma Neno la Mungu.

Wengine walikuwa wanalalamika kazi zinawabana, wamefukuzwa kazi hata ile hamu ya kusoma Neno la Mungu haipo wala kukumbuka washike biblia haipo kabisa. Wanarudi mtindo ule ule wa mwanzo wa kusubiri wapate kitu fulani kwanza ndio waanze.

Nataka ujifunze jambo hapo kwa hayo Makundi hapo juu, huenda ukawa ni wewe au huenda akawa rafiki/ndugu yako. Unafikiri ni muda upi sahihi kwako wa kuanza kusoma Neno la Mungu ikiwa umepita hatua zote hizo lakini bado unaendelea kuongeza muda mbele.

Mwingine anasema kwa sasa sina utulivu kabisa, ngoja nimalize mipango ya kuoa/kuolewa ndipo nitakuwa huru kusoma Neno la Mungu. Ameingia kwenye ndoa, kwanza akageuza na kibao kinachosema, amebanwa na majukumu ya ndoa.

Hebu fikiri mwenyewe ni muda gani sahihi kwa watu wa namna hii, kama ni wewe hebu jaribu kufikiri tangu uanze kujiahidi kuanza kusoma Neno la Mungu. Hizo ahadi zimekufanikisha lolote? Maana badala ya kutekeleza kile ulisema utafanya, unazidi kusogeza siku mbele kadri Mungu anavyokufanikisha mambo yako.

Ombi langu kwako, hupaswi kumpuzika kwa kisingizio chochote kile, patwa na jambo la kukuzuia kushindwa kusoma Neno la Mungu siku moja. Alafu kesho yake hakikisha umeondoka na somo ili usirudie tena kosa la kushindwa kusoma Neno la Mungu, hata kama utakutwa ukiwa kwenye changamoto ile ile iliyokuzuia usisome siku iliyopita.

Labda ukutwe upo hoi hospital au ukawa nyumbani lakini unaumwa kiasi kwamba ukishika biblia unaona pichapicha tu badala ya maandishi. Hapo inaeleweka kabisa huyu ana shida ila sio hizi changamoto zingine nilizokueleza hapo juu.

Acha kujidanganya muda fulani ndio utakuwa huru sana kufanya mambo yako, kama ulikuwa hujui unapaswa kujua hivi sasa; kila kukicha kuna changamoto yake ngumu, linatoka hilo ulilokuwa unaona limekubana sana linakuja lingine ngumu zaidi ya hilo uliloona kikwazo kwako.

Maisha ndivyo yanavyoenda, hupaswi kujipa sana muda wa kuanza kusoma Neno la Mungu. Hapo ulipo unao uwezo wa kutenga nusu saa kila siku ya kusoma Neno la Mungu, na ukapata muda wa kutafakari yale uliyojifunza. Usisome mambo mengi, soma sura moja au mbili tu, kesho endelea ulipoishia, fanya hivyo bila kukoma.

Anza sasa na sio kesho.

Chapeo Ya Wokovu

chapeo@chapeotz.com

www.chapeotz.com

+255759808081.