Haleluya,
Unajua binadamu kuambiwa ajifunze kwa mdudu, inaonyesha kwamba tabia tulizonazo hazimpendezi Mungu kiasi kwamba tumezidiwa akili na mdudu. Na Kitu pekee kilichoumbwa kwa mfano wa Mungu ni mwanadamu, vyote unavyoviona havijaumbwa kwa mfano wa Mungu.
Pamoja na sisi kuwa wana wa Mungu, lakini bado hatutaki kujenga ushirika wetu na Mungu. Yapo maeneo hatuwajibiki ipasavyo, kinachotufanya tusiwajibike ni kuwa wavivu wa kupindukia.
Uvivu sio wa kushindwa kufanya kazi ngumu za mikono, hata kutojishughulisha na mambo ya Mungu huku ukisema tupo pamoja kwa maneno matupu. Huo ni uvivu, uvivu ambao unakufanya usichukue hatua, na ukichukua hatua humalizi siku nyingi unaacha kufanya.
Leo tunaenda kujifunza kwa mdudu, ndio tunaenda kujifunza kwa CHUNGU, ni moja ya wadudu mashuhuri aliyepata kibali cha kusifiwa kutokana na akili na bidii aliyonayo. Mpaka mwanadamu anashauriwa kujifunza kwake, mpaka tunahimizwa kuzitafakari njia zake tupate hekima.
Chungu ni mdudu asiye na mikono ya kulima, ila kazi yake ni moja tu, wakati wa mavuno ya shamba la mkulima yeye hukusanya yale masalia ya mbengu zinazoanguka chini. Hizo mbengu anajiwekea akiba ya chakula, na wakati wake sahihi wa kujiwekea akiba, ni ule wakati wa kiangazi wanapovuna wakulima mazao yao.
Mdudu yule anajua mazao yale hayatakuwepo kila siku, utafika wakati yatakosekana, anajua upo wakati wa masika, wakati ambao sio rahisi kuona kile chakula. Anachofanya ni kukusanya kidogo kidogo mpaka anajaza ghala zake.
Huyu mdudu chungu hana msimamizi anayemsimamia nyuma yake ili akusanye chakula, wala hana mkuu anayemwongoza kufanya hili zoezi la ukusanyaji wa chakula ila yeye tu na akili yake. Ambapo ni tofauti na watu wengine hawawezi kujiwekea akiba ya chakula mpaka serikali itoe tangazo la kutouza chakula.
Rejea:Ewe mvivu, mwendee chungu, Zitafakari njia zake ukapate hekima. Kwa maana yeye hana akida, Wala msimamizi, wala mkuu, Lakini hujiwekea akiba ya chakula wakati wa jua; Hukusanya chakula chake wakati wa mavuno. MIT. 6:6-8 SUV
Leo hii una muda wa kutosha tena sio muda tu, unazo nguvu. Una uwezo wa kusoma Neno la Mungu ila husomi, una macho mawili yanayoona ila huyatumii kusoma, akili zako zina uwezo wa kuhifadhi mambo mengi ila hutaki kuzishughulisha kwa chochote.
Unasubiri wakati upi utakaokufaa wewe kujiwekea akiba ya Neno la Mungu, Neno la Mungu ni chakula chako cha kiroho. Unahitaji kujiwekea akiba ya kutosha ndani ya moyo wako, moyo wako ni ghala la kuhifadhia chakula ambacho ni Neno la Mungu.
Pamoja na una akili kuliko hata mdudu chungu, bado anakushinda kuhifadhi chakula. Ambapo chakula chako ni Neno la Mungu, ndio ni Neno la Mungu, umekuwa mvivu kiasi kwamba unaambiwa ujifunze kupitia chungu ili upate hekima.
Itafika siku hutoweza kusoma Neno la Mungu, akiba yako uliyoijaza wakati una uwezo wa kusoma Neno la Mungu ndio itaweza kutumika kukusaidia kushinda mahali pagumu unapopitia. Wakati ambao huwezi kulima ukapata mazao, ni wakati mwafaka wa kutumia akiba zako ulizojiwekea siku za mavuno.
Wakati wa mavuno kwako ni pale unapokuwa na nafasi ya kusoma Neno la Mungu, ni wakati ambao unaweza kutenga dakika zako chache za kusoma Neno la Mungu. Bila kusukumwa na mtu, bila kusimamiwa na yeyote yule, kwa hiari yako mwenyewe unakuwa na ratiba ya kulijaza Neno la Mungu moyoni mwako.
Wakati unajiwekea akiba moyoni mwako, watu wengine wanaweza kukutolea maneno ya kejeli, wanaweza kukuona vile wanaona wao. Watu wale wale ndio watakaokuja kukuomba msaada wa chakula wakati wa njaa, wakati wanapita kwenye changamoto ngumu na hawana uwezo wa kukabiliana nazo. Wataanza kutafuta watu wenye ushauri mzuri wa kuwasaidia, watu wenye hekima ya kung’amua mambo mazito.
Watu hao ni wale waliotoa muda wao kujaza maarifa sahihi ya Neno la Mungu, watu wanaojua kung’amua mambo mazito. Maana ndani yao wamejaa maarifa sahihi na ya kutosha ndani yao, kwa lugha nyingine hawana njaa, njaa kwao wanaisikia kwa majirani ila kwao ghala zimejaa.
Usishindwe akili na chungu, asiyehitaji akida, wala msimamizi, wala mkuu yeyote wa kumsimamia mbele yake ndio akusanye chakula. Yeye anajituma kivyake, hasubiri aonekane, asubiri siku maalum kama unavyosubiri wewe, yeye anajua wakati wa mavuno ndio wakati wake sahihi wa kukusanya akiba yake.
Jiwekee akiba ya chakula cha kiroho, wakati sahihi ni sasa, usiwe mtu wa kusimamiwa sana ndio uwe na hamu ya kusoma Neno la Mungu. Jiwekee utaratibu wako wa kusoma Neno la Mungu bila kuangalia nani atakuona, hata kama hawakuoni litakusaidia mwenyewe. Nasema sio lazima watu wengine wajue unajiwekea akiba ya chakula, wakati wa njaa ukifika watajua tu una akiba na watakuja kwako kukuomba msaada wa chakula.
Bila shaka hutokubali tena kushindwa akili na bidii aliyonayo mdudu huyu chungu, huenda kwa macho unamwona ni mdudu aliye dhaifu sana. Pamoja na udhaifu wake biblia inamtaja kama mdudu wa kujifunza mazuri kutoka kwake.
Mungu akubariki sana kwa muda wako.
Facebook: Chapeo Ya Wokovu
Email: chapeo@chapeotz.com
Tovuti: www.chapeotz.com
WhatsApp: +255759808081