Haleluya,

Kila mmoja wetu anapitishwa kwenye changamoto ngumu sana ambayo inaweza isifanane na ya mwingine, lakini pamoja na kutofanana. Bado ni changamoto, wakati mwingine analia hili, yupo mwingine analia zaidi na lingine.

Wakati mwingine unaweza kujiona wewe umezidiwa sana na matatizo, ukija kusikia mwenzako anayokusimlia ya kwake. Unaanza kujiona wewe mbona unaafadhali kubwa kuliko mwenzako, badala ya kuendelea kuhuzunika, unapata huruma ya kumtia moyo mwenzako.

Wakati wewe unalalamika umepoteza sh. 10,000 na moyoni mwako unajisikia vibaya sana, kwa sababu ndio hiyo hiyo ilikuwa imebakia kwenye pochi/mkoba wako. Yupo mwingine anaumia amepoteza sh. 500,000, unaweza kuona mbona ya kwangu ndogo sana alafu nakosa usingizi.

Maisha yana mambo mengi, yapo ya kufurahisha sana, na yapo ya kuhuzunisha sana. Ukiona furaha imezidi sana kwenye maisha yako, jiandae huzuni I karibu sana, na ukiona huzuni imezidi sana kwako, jua furaha I karibu sana.

Ukiona njia/barabara ina mteremko mkali sana, jua mlima u karibu sana mbele yako, na ukiona mlima u mkali sana, ukafika mahali ukachoka sana kupandisha juu. Uwe na uhakika kilele chake ki karibu, utaanza kuteremka kwa furaha sana.

Ukiona jua limezidi sana na unaona joto sana, jua jioni imekaribia sana, utafurahia sana kivuli chake. Na ukiona usiku umekuwa mrefu sana, jua asubuhi imekaribia sana.

Ukiona kiangazi kimekuwa kirefu sana, jua masika yamekaribia sana. Utaanza kufurahia mvua ikitiririsha maji sehemu mbalimbali, ndio wakati wa kula matunda mbalimbali ya miti.

Usifanye vitu vya msingi kwenye maisha yako ukiwa kwenye wakati fulani tu, usifanye mambo ya kiMungu ukiwa kwenye furaha tu. Ukishakutana na changamoto ngumu unaachana na mambo ya Mungu, na Usifanye mambo ya kiMungu ukiwa kwenye changamoto ngumu inayohitaji msaada wa Mungu. Baada ya Mungu kukusaidia, unaona haina haja ya kuendelea kumtumikia/kumtafuta Mungu kwa bidii.

Wengi wetu tumechoka mambo ya kiMungu, waliokuwa wana bidii sana ya kumpa Mungu muda wao, leo hii hawana tena muda huo. Wapo bize, ukiwauliza nini haswa inayowakwamisha wasifanye mambo ya kiMungu, wanabaki wanajikanyaga bila majibu ya kueleweka.

Kumbe ndani yao wamechoka, hawana hamu tena ya kutenga muda wao wa kumwomba Mungu, hawana tena hamu ya kuhubiri, hawana tena hamu ya kuimba, hawana tena hamu ya kusoma Neno la Mungu. Kazi iliyobaki ni kulalamika muda mfupi, muda upi ambao wanautaka sasa na zamani haukuwepo, unakuta ni kelele tu za mtu aliyekandamizwa mahali.

Leo tunazungumza sana habari ya kusoma Neno la Mungu, sio kwamba wengi hawajawahi kusoma kabisa Neno la Mungu. Wamewahi kusoma ila walivyokutana na changamoto ngumu wameamua kuacha, sababu wanayoitumia ni ngoja wapumzike kwanza wataanza kesho.

Hiyo kesho haijawahi kufika kwao, toka January hadi leo September, bado wanasubiri waje waanze, wamechoka, tena wamechoka kweli kweli. Maana wameruhusu udhaifu ndani yao uwe kikwazo, wakati walikuwa wana uwezo wa kuendelea na utaratibu wao wa kila siku, huku wakiendelea kupambana na changamoto zilizo mbele yao.

Pamoja na unapita mahali pagumu sana, usije ukaruhusu udhaifu wa aina yeyote ukakwamisha kusoma Neno la Mungu. Fanya kila namna, usikubali maumivu makali unayopitia yakufanye ushindwe kusoma Neno la Mungu. Itokee tu upo kitandani alafu hujitambui kabisa, ila kama bado u mzima wa afya njema hakikisha huachi kusoma Neno la Mungu.

Wakati unapanda mlima na wakati utakaposhuka mlimani, ukutwe bado unaendelea na ratiba yako ile ile ya kusoma Neno la Mungu, labda kitakachobadilika kwako ni muda wako wa kusoma Neno la Mungu. Ila siku ni ile ile, nikiwa namanisha kwamba kila siku umehakikisha haipiti bila kusoma Neno la Mungu.

Kumbuka haya siku zote, utajinua mwenyewe mahali popote pale utakapojiona kuanguka. Hutahitaji msaada wa wengine kukuinua, maana tayari unajua unayopitia ni ya muda tu hayawezi kukufanya wewe usimamishe ratiba yako ya kusoma Neno la Mungu.

Ufike mahali watu washindwe kukuelewa kabisa, wakati wanakuona umeanguka wakitegemea utaendelea kulala palepale na kuacha mambo yako mengine. Wakuone ukiinuka tena na kuendelea na safari yako ile ile hata kama wewe unajisikia sio mwepesi kama awali.

Mungu akubariki sana, nakutakia siku njema.

Facebook: Chapeo Ya Wokovu

Email: chapeo@chapeotz.com

Tovuti: www.chapeotz.com

WhatsApp: +255759808081.