Haleluya,

Yapo mazingira yanayoweza kutufanya tukawa na bidii kwa mambo ya Mungu, na yapo mazingira usipokuwa makini unaacha kabisa kuhusiana na mambo ya Mungu. Unaweza kuwa ulikuwa msomaji mzuri sana wa Neno la Mungu ila ukafika mahali ukashindwa kufanya hivyo kutokana na mazingira.

Mazingira yana mchango mkubwa sana kumfanya mtu awe na uhusiano mzuri na Mungu wake, na mazingira yale yale yanaweza kumfanya mtu asiwe na uhusiano mzuri na Mungu.

Mtu anaweza kuwa mahali ambapo hayupo huru kumwabudu Mungu wake, ukashangaa akafanya vizuri zaidi kuliko yule ambaye yupo huru kumwabudu Mungu wake.

Wakati mwingine unaweza kuona mtu ameacha ile bidii yake kutokana na mazingira aliyopo, ila ukichunguza kwa umakini unaweza kuona sio mazingira. Maana kama kigezo ni mazingira mbona wakati yupo maeneo yasiyo mhuruhusu kulitaja jina la Yesu Kristo alikuwa vizuri, mbona wakati yupo huru kumwabudu Mungu wake hakufanya hivyo.

Sikatai kabisa mazingira yanaweza kudhofisha ile kasi yako ya vitendo, ila moyo wa mtu hauwezi kufunikwa na mazingira, wala huwezi kunyamazishwa na mazingira yeyote yale. Ukitaka kujua soma habari za Daniel, kwenye kitabu cha Daniel, utaona maisha yake yalivyomcha Mungu wa kweli na kukataa kuabudu miungu mingine.

Wengi wanakuwa hivi; mtu akiwa na kazi ya kufanya anasema hana muda wa kuomba Mungu, hana muda wa kusoma Neno la Mungu, hana muda wa kwenda ibadani. Akiikosa hiyo kazi ndio anapotea zaidi, anabadilisha na msemo kabisa, na mwingine anarudi kweli kwenye bidii yake.

Mtu mwingine akiwa hana kazi kabisa, anakuwa anafikiri akiwa na kazi nzuri ndio ataanza kuwa na bidii kwa mambo ya Mungu. Anapata hiyo kazi aliyokuwa anaitafuta, anabadilisha tena msemo ule wa mpaka apate kazi sasa unageuzwa na kuwa nimebanwa sana na majukum ya kazi.

Unaweza kuona unafuu hakuna mahali popote kama mtu mwenyewe hatoamua kutenga muda. Kila hatua ya maisha yetu ina changamoto zake ngumu zaidi, unaweza kusema leo umebanwa sana ikafika kesho ukaona jana ilikuwa nafuu.

Nataka kusema nini hapa, nikirudi kwenye moyo wa somo hili ni kwamba. Usionyeshe unamtumikia/unampenda Mungu ukiwa mazingira fulani tu. Na ukiwa mazingira tofauti na hayo uliyozoea, hata ile bidii yako kwa mambo ya Mungu inapoa.

Ni mbaya sana kuonekana upo vizuri kiroho ukiwa kwenye hali fulani ya kukosa pesa, ni mbaya kuonekana upo vizuri kiroho ukiwa kwenye hali fulani ya kuwa na pesa.

Ni mbaya sana kuonekana upo sana kiroho ukiwa na uhitaji wa kupata mke/mume, ukishampata huyo mume/mke na ile bidii yako inazimika. Na mbaya sana ukiwa na mke/mume ndio unaonekana upo vizuri kiroho, akiondoka au akisafiri unaonekana umechoka sana.

Unanielewa ninachokisema hapa? Nasema hivi; usionekane unampenda Mungu na kuwa na bidii kwa mambo ya Mungu ukiwa kwenye mazingira/hali fulani tu. Kwanini usiwe hivyo, maisha yanabadilika, leo upo hapo, kesho ukawa sehemu nyingine kabisa mpya.

Shetani anaweza kukushitakia/kukusemea kwa Mungu kama alivyofanya kwa Ayubu;

Rejea;BWANA akamwuliza Shetani, Je! Umemwangalia huyo mtumishi wangu Ayubu? Kwa kuwa hapana mmoja aliye kama yeye duniani, mtu mkamilifu na mwelekevu, mwenye kumcha Mungu na kuepukana na uovu; naye hata sasa anashikamana na utimilifu wake, ujapokuwa ulinichochea juu yake, ili nimwangamize pasipokuwa na sababu. Shetani akamjibu BWANA, na kusema, Ngozi kwa ngozi, naam, yote aliyo nayo mtu atayatoa kwa ajili ya uhai wake. Lakini sasa nyosha mkono wako, uuguse mfupa wake na nyama yake, naye atakukufuru mbele za uso wako. BWANA akamwambia Shetani, Tazama, yeye yumo mkononi mwako; lakini tunza tu uhai wake. AYU. 2:3‭-‬6 SUV

Hebu ona hapo, wakati Mungu anajivunia Ayubu kwa uaminifu wake kwake, shetani alimwona Ayubu anampenda Mungu kwa sababu ya watoto wazuri, mali nyingi, na afya ya kutosha. Lakini Mungu aliona Ayubu sio mwaminifu mbele zake kwa hivyo vitu, ndio maana ukiendelea kusoma utakuja kuona pamoja na kupoteza hivyo vyote bado alikuwa anampenda Mungu.

Wangapi Leo baada ya kuumwa sana waliendeelea na kumpenda Mungu bila kupata vishawishi vya kwenda kwa miungu mingine, wangapi leo walivyopoteza mali zao waliendelea kumpenda Mungu, na wangapi leo waliopoteza watoto wao wote waliendelea kulitaja jina la Yesu Kristo.

Bila shaka umeanza kunielewa, usikubali jambo lolote lile likutoe kwenye mstari wako, ulivyokuwa na vitu ulikuwa unampenda Mungu katika roho na kweli. Na ulivyokosa au ulivyopoteza hivyo vitu upendo wako ulibaki palepale.

Usionyeshe ulikuwa unampenda Mungu kwa sababu ya mazingira fulani, yawe mazuri au mabaya, usikubali kuonyesha udhaifu huo. Pambana kuhakikisha moto hauzimiki ndani yako, usikubali kusema bado tupo pamoja na wakati kwenye matendo umekufa kabisa. Maneno na vitendo viendane.

Usomaji wako wa biblia usibadilishwa na mazingira yeyote yale, ilimradi hujakatazwa kusoma Neno la Mungu. Uwe sehemu gani mbaya/nzuri soma Neno la Mungu, uwe unafuraha/huzuni soma Neno la Mungu, uwe mjini/kijijini soma Neno la Mungu, uwe tajiri/masikini soma Neno la Mungu, uwe mchungaji/mshirika soma Neno la Mungu, uwe una au hauna mke/mume soma Neno la Mungu.

Mungu akubariki sana kwa muda wako.

Chapeo Ya Wokovu

chapeo@chapeotz.com

www.chapeotz.com

+255759808081.