Haleluya,

Zipo nyakati tunakuwa huru sana kufanya mambo yetu mengi kwa wakati mmoja, na zipo nyakati tunakuwa tumebanwa sana. Hata ule muda wa kufanya mambo yetu kwa uhuru tunakuwa hatuwezi tena.

Usipokuwa makini pale unapojikuta kwenye kubanwa sana, unaweza kuacha kufanya vitu vya msingi. Badala yake ukawa unafanya vitu ambavyo havikuletei msaada wowote kwenye maisha yako.

Hasa kwenye eneo la kusoma Neno la Mungu, unaweza kuwa mwanzo ulikuwa unapata nafasi ya kusoma Neno la Mungu kutokana na uhuru uliokuwa nao kazini. Ikatokea ghafla huo huru ukawa huna tena, je utaacha kusoma Neno la Mungu? La hasha lazima uendelee ila kwa mpangilio mpya.

Angalia ni mahali gani huwa unaacha muda wako unamwagika ovyo, huenda ni kwenye magroup ya kuchati ambayo hayakuongezei kitu chochote, huenda unazunguka sana kwenye mitandao ya kijamii. Na Huenda kuna mahali huwa unaenda kuongea tu na rafiki/marafiki zako.

Wakati unalalamika huna muda kabisa, angalia hivyo vitu, ukiona hata hivyo huwa huna hiyo nafasi ya kuvifanya. Rudi tena uangalie ratiba yako kuanzia unaamka mpaka unaenda kulala, ni vitu gani huwa unavifanya.

Orodhesha ratiba yako kwa siku, angalia vitu vyote unavyovifanya kwa siku, ukishavipata anza kupitia moja baada ya lingine. Lipo utaliona huwa unalifanya ila sio muhimu sana kulifanya kwa wakati huo, kwa mfano ulikuwa na groups tano za whatsApp unazozifuatilia na kabiria zote zina mambo ya Muhimu. Katika hayo makundi matano angalia ambayo sio lazima uingie, anza na moja Kupunguza kuingia ili zile dakika ulizokuwa unazitumia kwenye hilo group zihamishie kusoma Neno la Mungu.

Unapunguza kuyatembelea kwa sababu unaona huwezi kujiondoa, ila kama unaweza kujiondoa ili uwe huru zaidi, nakusihi fanya hivyo. Huenda usiwe na nidhamu yako binafsi ya kuweza kuacha kuangalia nini kinaendelea, jitoe kabisa kama sio Makundi uliyolipia au kama sio makundi ya kazi yako.

Jambo Lingine ni hili, punguza kabisa kuongea na simu muda mrefu bila sababu za msingi, wapo watu kwenye na simu ni kama ulevi wao. Anaongea na simu mpaka inapata moto, anachokiongelea cha muhimu hakuna ila unakuta ni stori tu.

Kwanini nasema hivi, wengi wetu tunalia hatuna muda kabisa wa kusoma Neno la Mungu kutokana na majukum au kutokana na mazingira tuliopo. Unakuta ule muda ambao tupo huru ndio tunautumia sana kwenye mambo ambayo sio ya msingi sana kama kusoma Neno la Mungu.

Huenda hujui vizuri umhimu wa Neno la Mungu, ila nikueleze kwamba Neno la Mungu ni muhimu sana katika maisha yako ya kiroho na kimwili. Unapaswa kuhakikisha ratiba zako zingine zinakuwa za mwisho, ila ratiba ya kusoma Neno la Mungu inakuwa ya kwanza.

Tenga nusu saa au saa moja ya kusoma Neno la Mungu, hili zoezi lifanye kila siku ndani ya siku husika. Usisome kwa kulipuka siku moja na kupotea, ufanye ndio mpango wako wa maisha yako.

Nakwambia ukweli hutokwama, utabanwa sana ila haiwezi kumaliza wiki bado hujapata mbinu ya kuweza kukabiliana na kubanwa kwako. Maana wakati mwingine tunalia hatuna muda kumbe tunasumbuliwa na uvivu wetu wenyewe, ila muda kama muda tunao mwingi, mwingine huwa tunauacha unamwagika tu ovyo bila sababu yeyote.

Usipuuze hili kwa wewe ambaye upo wakati unaona huna kabisa muda wa kusoma Neno la Mungu, nimekuambia pitia upya ratiba yako. Kuna vitu utaviona ulikuwa unavifanya ila sio muhimu sana kwako, unaweza kukuta umhimu upo ila sio sana.

Labda tuseme huwa unapenda sana kusikiliza nyimbo mbalimbali za watumishi wa Mungu, na mahali pa kuzipata huwa unaenda YouTube. Muda unaotumia YouTube ukiuhamishia kwenye kusoma Neno la Mungu, ni heri zaidi kuliko kusema huna muda ila unashindia YouTube. Kwanza utakuwa umepata faida nyingine ya kusevu bando lako la MB/GB, kwa Kupunguza kuingia mara kwa mara YouTube.

Hadi hapo utakuwa umegundua makosa uliyokuwa unafanya huko nyuma, japo sijataja yote ila naamini kupitia mifano hii michache utakuwa umeona mahali ulikuwa unakosea. Usibaki kusikitika, chukua hatua nyingine ya kuanza kufanya kwa vitendo.

Mungu akubariki sana kwa muda wako.

Facebook: Chapeo Ya Wokovu

Tovuti: www.chapeotz.com

Email: chapeo@chapeotz.com

WhatsApp: +255759808081.