Haleluya,
Jambo kabla ya kulianza unaweza kuliona raisi sana au unaweza kuliona gumu sana, wakati unafikiri hivyo kuna maneno utakuwa unasikia kuhusu hilo unalotaka kulifanya, au kuna maneno utakuwa unajisemea mwenyewe.
Maneno yale unayoyasikiliza yanaweza kukufanya ukaamua kuchukua hatua, au wewe mwenyewe unaweza kuwa unajiahidi kila siku kufanya jambo Lakini ukawa hufanyi vile unaongea.
Kuongea inaweza ikawa rahisi sana, kwenye kuongea unaweza kusema kila kitu, ila ikija kwenye matendo halisi kwa kile ulikuwa unazungumza. Inaweza kuwa tofauti kabisa, tofauti yake ni vile ulikuwa unaongea haiendani kabisa na matendo yako.
Tunapaswa kuelewa vizuri ili tusiwe watu wa kuongea tu kwa maneno ila tukija katika vitendo/matendo, tunakuwa watu wa kushindwa tu. Kweli inaweza isiwe vile tulikuwa tunafikiri, ila tusikubali hata vile vinavyowezekana kufanyika tunakuwa tunavishindwa kuvifanya.
Kushinda ama kushindwa ipo ndani ya mtu mwenyewe, unaweza kudhamiria kufanya jambo fulani ukafika mahali ukavunjika moyo na kuamua kuacha kutokana na mazingira magumu uliyokutana nayo. Pia unaweza kudhamiria na kujiahidi kuwa haijalishi mazingira gani magumu utakutana nayo, lazima ufikie lengo lako.
Ndivyo inavyowarudisha nyuma walio wengi, wanakuwa na maneno mengi mazuri sana kuhusu mpango wao wa kusoma Neno la Mungu. Lakini wakija kwenye matendo halisi, hawachukui muda wanakuwa wamerudi kwenye hali zao za awali.
Tunachopaswa kujua ni kuwa, kuongea ni rahisi sana kuliko matendo, unapaswa kujipanga kisawasawa kifikra. Jambo ukishalianza kulifanya mwenyewe, unakuwa sio mtu wa maneno tena, bali unakuwa mtu wa maneno yaliyoambatana na matendo.
Zile kelele za kuongea tu, unakuwa hauna tena, unakuwa mtu wa matendo, na tabia ya kufanya huwa nayo ina changamoto zake ngumu. Utakutana na maneno mengine ya kukuvunja moyo, hasa kwa wale ambao walikuwa kama wewe ulivyokuwa husomi Neno la Mungu.
Unaweza kuwa fundi mzuri sana wa kuongea, ila kama huweki vitendo kwa unayoongea, utabaki kuwa mkristo asiye na Neno la Mungu la kutosha moyoni mwake. Hili halina kuzunguka sana, kama unaongea tu, kama unaahidi kila siku utaanza kusoma Neno la Mungu kesho ila hufanyi hivyo, wewe ni mtu wa maneno matupu.
Yamkini hayo maneno yameenda mbali zaidi, unasema unamtumikia Mungu katika roho na kweli kumbe kuna njia zisizompendeza Mungu unazifanya kwa siri. Ukifikiri wewe unafanya kwa siri, kumbe watu wanakuona, wanaona kwa sababu Mungu ndiye wa kwanza kukuona.
Unapoamua kuondoka kwenye eneo la maneno matupu, hakikisha unajipanga kisawasawa kifikra usije ukarudi kwenye udhaifu wako. Maana ni rahisi sana kwa mtu wa maneno mengi kushindwa, alafu akabadilisha maneno mengine ya kujifariji katika kushindwa kwake.
Umeamua kuwa msomaji wa Neno la Mungu, hakikisha ndani yako umejipanga, hata kama utakutana na vitu ambavyo hukuvitegemea kuvikuta. Hilo lisiwe shida kwako kwa sababu umedhamiria kweli kutoka moyoni mwako.
Nasema hivi kwa sababu ipo vita kubwa sana katika kusoma Neno la Mungu, ni kama vita ya mtu aliyeokoka kisawasawa. Sasa kama unaweza kukabiliana na vita ngumu ya kuokoka kwako, je hii vita ya kukuzuia usisome Neno la Mungu itaweza kukushinda? La hasha ukiamua haitakushinda.
Usifike mahali watu wakakuchoka kwa maneno yako yaleyale ya kila siku, watu waone kile unakizungumza ndicho unakiishi. Utakuwa mfano bora sana mbele ya jamii inayokuzunguka na hata ile isiyokuzunguka, na utakuwa shuhuda mzuri sana kwa kizazi chako cha sasa na kijacho.
Kiri kutoka katika eneo la maneno mengi pasipo Matendo, na kiri kuingia katika eneo la maneno yanayoambatana na matendo halisi.
Mungu akubariki sana kwa muda wako.
Facebook: Chapeo Ya Wokovu
Email: chapeo@chapeotz.com
Tovuti: www.chapeotz.com
WhatsApp: +255759808081