Haleluya, zipo baraka za Mungu tunazikosa kwa kutokuwa na muda wa kupata mafundisho ya Neno la Mungu. Mafundisho yanayoweza kutupa mwanga zaidi kadri tunavyozidi kwenda mbele katika safari ya wokovu wetu.

Mafundisho ya Neno la Mungu tunaweza kuyapata, kwa kusoma wenyewe Neno la Mungu ndani ya biblia, au kwa kuhudhuria ibada za mafundisho kanisani, au kwa kusikiliza kwa njia ya mitandao ya kijamii au radio zinazorusha ibada za semina.

Hizi njia zinaweza kukusaidia kuwa na uelewa mzuri baadhi ya mambo mengi ambayo hukuwa unayajua, pia unaweza kuona jinsi gani Mungu alivyo mwema kwako. Kutokana tu na vile umesikia habari njema zinazogusa maisha yako moja kwa moja.

Pamoja na njia zote hizo, bado utalazimika kuwekeza nguvu katika kusoma mwenyewe Neno la Mungu. Unaposoma Neno la Mungu alafu ukaenda kusikiliza mafundisho kanisani au kwenye mikutano ya nje, inakupa Mwanga zaidi wa kuendelea kuelewa kwa mapana zaidi.

Unapata nafasi ya kupanua zaidi uelewa wako, kama ulikuwa unatafakari ukaishia mahali ukaona ndio mwisho, unapopata mafundisho zaidi uelewa wako unapanuka/unakua zaidi ya mwanzo.

Haya yote tunayakosa kwa sababu hatuna muda wa kutulia tusome Neno la Mungu, tunakosa mema mengi sana ya Mungu juu ya maisha yetu kwa uzembe wetu wenyewe. Wakati tulikuwa na uwezo wa kusoma Neno la Mungu tukapata cha kutembea nacho ndani ya mioyo yetu.

Imani yetu kwa Mungu wakati mwingine imeonekana ya mashaka, kwa sababu hatuna Neno la Mungu ndani yetu. Na kwa sababu hatuna mafundisho sahihi yanayotusaidia kujua uwezo wa Mungu juu yetu.

Uaminifu wetu kwa Mungu hauna nguvu kubwa kutokana na kukosa maarifa sahihi, unaweza kukataa na kujiona upo sahihi. Lakini yapo mengi sana ambayo haupo sahihi sana pamoja na unajiona upo sahihi.

Hebu tuone maandiko matakatifu yanasemaje kuhusu hili ninalolizungumza hapa;

Rejea: Atakayelitafakari neno atapata mema; Na kila amwaminiye BWANA ana heri. MIT. 16:20 SUV

Kama anayelitafakari neno atapata mema, je asiyelitafakari Neno atapata nini? Bila shaka kuna vitu vingi sana atavikosa kwa Kutotafakari kwake Neno la Mungu. Pia huwezi kumwamini sana usiyejua uwezo wake juu ya maisha yako, wanaomwamini Mungu kisawasawa ni wale wanaolijua vizuri Neno lake.

Vitu vingine vinahitaji uchukue hatua, kama ilivyo kupata haya mema, bila kulitafakari Neno la Mungu ni vigumu kupata hayo mema. Wakati mwingine umejifungia ndani kwa kukosa tumaini la maisha yako, ni kutokana tu na kukosa neno moyoni mwako.

Walio na Neno la Mungu mioyoni mwao, wana tumaini jipya kabisa juu ya maisha yao ya sasa na ya baadaye. Wanao ujasiri mkubwa sana hata wanapopita kwenye mazingira ambayo kila mtu analia, wao wanakuwa na tumaini kwa Mungu wao.

Nasi ili tuweze kufika mahali tuwe tunamwamini Mungu hata katikati ya Changamoto ngumu, tunapaswa kutenga muda wa kutosha wa kusoma na kulitafakari Neno la Mungu. Haitoshi tu kusoma peke yetu, tunapaswa kupata muda pia wa kwenda kusikiliza mafundisho ya Neno la Mungu, iwe kanisani au mahali popote pale ilimradi ni mafundisho sahihi ya Neno la Mungu.

Jitume katika hili jambo, usione ninachokueleza hapa sio cha lazima sana. Ni cha lazima sana kwa sababu kinakusaidia kuimarika katika imani yako mbele za Mungu, japo kufanya hivyo inaanzia kwanza na hiari ya moyo wako.

Hiari bila kusukumwa na chochote ni nzuri ila unapaswa kuitengenezea mazingira mazuri ya kujitambua unachofanya hakipaswi kuishia njiani. Ishi na hili katika maisha yako yote, hakikisha hupungukiwi na Neno la Mungu, umekwama leo hakikisha kesho hukosi neno.

Mungu akubariki sana kwa muda wako.

Facebook: Chapeo Ya Wokovu

Email: chapeo@chapeotz.com

Tovuti: www.chapeotz.com

WhatsApp: +255759808081