Haleluya, tunapaswa kujua kinachokuja kuangusha watu ni kipi, kitu ambacho mwanzo hakikuwangusha ila walivyoendelea na safari yao ghafla kikawaangusha.
Tusipoelewa hili jambo mapema ni rahisi sana hata kwako linaweza kukutokea ukashangaa ule moyo wa kufanya mambo ya kiMungu unatoweka kabisa. Unaweza kufikiri kuna mahali umekwamishwa kumbe umejikwamisha mwenyewe kutokana na matarajio fulani ambayo uliyapanga katika utendaji wako.
Ni ukweli kabisa ulio wazi, kila mmoja anapenda kuvuna matunda kwenye eneo alipo, lakini pamoja na hilo wengi wetu tumegeuza hili vibaya zaidi. Kwanini nasema vibaya, ni kwa sababu mtu anakuwa na bidii kwa mambo ya Mungu kwa kutarajia kupata faida fulani.
Wengine wanaomwona wanaweza kufikiri huyu mtu ameamua kumtumikia Mungu kisawasawa, kumbe yupo kwenye msimu wa kupanda mbegu ili aje avune mazao ya kile alipanda. Hajui kwamba baada ya mavuno anaweza kupotea kabisa kwenye eneo alilosimama mpaka watu wakasema huyu kijana/mzee yupo vizuri.
Moja ya vitu vinavyoturudisha nyuma ni sisi wenyewe, mtu anaweza kujitoa sana kwa mambo ya Mungu, kumbe nia yake anataka kuonekana kwa washirika wenzake ili iwe rahisi kupitisha jambo lake. Kumbe huo ni mtego ambao unampa hamu ya kumtafuta Mungu kwa bidii, akishafanikiwa tu na ile bidii yake inamwondoka moja kwa moja.
Muda mwingine tunaweza kumtafuta mchawi kumbe sisi wenyewe ndio tumejiloga pasipo kujijua, kama mtu anakuwa na bidii kipindi anahitaji kitu fulani. Unafikiri akija kukipata hicho kitu kutakuwa na bidii tena? Ni wachache sana huwa wanaendeleza hizo bidii.
Huenda hujanipata vizuri, ipo hivi si unaonaga kikundi cha kwaya wakiwa wanaenda kurekodi mkanda wao wa sauti au picha. Jinsi wanavyokuwa na bidii ya mazoezi na maombi ya kufunga, hata wakipanda madhabahuni/jukwani unaona kabisa Roho Mtakatifu yupo katikati yao kwa jinsi wanavyoiba na kugusa wale wanaowasikiliza.
Kikundi hichihichi kikishamaliza kazi ya kurekodi mkanda wao wa sauti au picha, ile nguvu ya kuhudumu madhabahuni/jukwani inatoweka kabisa. Unaweza kufikiri wamevamiwa na nini, kumbe wanafanya mambo ya kiMungu kwa matukio.
Leo unamwona kijana ambaye hajaolewa/hajaoa alivyo na bidii kwa mambo ya Mungu, yaani wakati mwingine unaweza kufikiri huyu kijana ana moyo gani kiasi kwamba anaweza kujitoa kiasi kile. Lakini baada ya kuoa/kuolewa humwoni tena na ile bidii yake, kumbe kufanya hivyo ilikuwa kutaka kuonekana na mchumba wake au na kanisa au na jamii.
Nimeona tabia hii ikienda katika usomaji wa Neno la Mungu, vijana wengi sana wanakuwa na bidii kusoma Neno la Mungu ili kuonekana kwa wenzao kuwa wapo vizuri. Pia wanakuwa na bidii ili kutaka kuonekana na wenzao, ili ikifika kipindi cha kuchangisha michango iwe rahisi kwao kufanya hilo zoezi.
Kuna kijana mmoja kanisani, nilimwona anakuwa na bidii sana kanisani, akafika kipindi akaniomba namba yangu, akawa ananitumia sms kila siku. Nikasema huyu ndugu ana moto kweli wa utumishi ndani yake, ila nikajipa tahadhari kutokana na ile kasi yake.
Unafikiri ilichukua muda, kweli bwana zile fujo zote ilikuwa kutaka kujulikana kwa viongozi ili aje aingize jambo lake. Baada ya hapo sikumwonaga tena, na zile sms zake sizioni tena hadi leo.
Sio huyo tu, nimeona hili hata kwenye group la whatsApp la Chapeo Ya Wokovu, wengi wanaingia kwa mtindo huu huu. Baada ya kuoa/kuolewa humwoni tena akishirikiana na wenzake katika kusoma Neno la Mungu.
Hizi njia tunazofikiri zinatuweka vizuri katika maisha yetu ya wokovu, ni njia mbaya sana. Maana tunakuwa hatufanyi kwa msukumo wa kiMungu ndani yetu, ila tunafanya kwa sababu tunataka kuonekana kwa wengine. Badala yake tunajikuta hatufanyi tena kama ilivyokuwa mwanzo.
Mambo mengine yawe ziada tu, ila hakikisha unamtumikia Mungu siku zote, yaani kasi yako iwe ile ile, isiwe ya matukio fulani tu. Ukishavuka hapo unarudi kwenye udhaifu wako, unakuwa mzembe wa vipindi kanisani, unakuwa mzembe wa maombi, unakuwa mzembe wa kusoma Neno la Mungu, unakuwa mzembe wa kutumika kwenye eneo ulilokuwa unatumika.
Nakusisitiza tena na tena, usiwe na bidii kwa mambo ya Mungu ukiwa unahitaji jambo fulani tu. Bidii yako ionekane siku zote za maisha yako, najua sio kila siku utaamka upo vizuri, hilo linajulikana ila hakikisha kasi yako ipo palepale.
Usijiingize kwenye kikundi cha kusoma Neno la Mungu ili wakuoneone, siku ukija kuwaambia naomba mnichagie mchango iwe rahisi kwako. Huo ni ujinga uliojaza kichwani, unapaswa kufuta kabisa hiyo dhana potofu, wanaweza wasitimize haja ya moyo wako ukaacha na kusoma Neno la Mungu. Pia wanaweza kutimiza haja ya moyo wako ukaona sasa huna hitaji tena ukaacha na kusoma Neno la Mungu.
Fanya kwa sababu unampenda Mungu na unasikia msukumo ndani yako, usifanye kwa sababu ya kutaka kuonekana kwa watu wengine. Utakwama vibaya sana kwenye mambo yako mengi, utafanikiwa kweli kwa muda huo mfupi ila utarudi nyuma tena.
Mungu akubariki sana kwa muda wako.
Facebook: Chapeo Ya Wokovu
Email: chapeo@chapeotz.com
Blog: www.chapeotz.com
WhatsApp: +255759808081