Nakusalimu katika jina la Bwana wetu Yesu Kristo aliye hai, karibu sana tujifunze pamoja somo hili ili tuweze kufika mahali tuwe na uwezo wa kufanya mambo yetu kwa bidii, na si kwa mkono mlegevu.
Mtu mvivu ndiye anayeongoza kwa sababu nyingi za kushindwa kupita yule asiye mvivu, mvivu ana maneno mengi sana lakini ukimpeleka kwenye matendo hayupo kabisa.
Mtu aliye mvivu anaweza kufanya kazi moja akajiona amechoka sana na akawa hataki kufanya chochote, kazi moja yenyewe aliyokuwa anafanya wala haikumaliza hata saa moja. Ila ukimgusa atasema amechoka sana, ukifuatilia kilichomfanya achoke unaona hakuna kabisa.
Mtu mvivu huwaza kupumzika kuliko kufanya kazi, wakati wengine wanafanya kazi yeye hutaka akae tu. Na wakati wa kuvuna matunda ya kazi zao, yeye hujikuta amefanya vibaya na wenzake wamefanya vizuri.
Tabia hii ya uvivu huenda mbali zaidi katika maisha ya wakristo walio wengi, wapo wavivu wa kuomba Mungu, hapa mtu hawezi kuomba hata nusu saa wala hawezi kukesha nusu saa akiwa anaomba Mungu.
Wapo wavivu wa kuamka asubuhi, kuna mtu analala saa mbili usiku anataka kuamka saa mbili tena ya asubuhi. Yaani analala masaa 12 ukiacha yale ya jioni aliyolala, huyu ni mvivu kazi anazofanya mpaka kumpelekea kuchoka kiasi kile unaweza usizione.
Tukisoma katika maandiko matakatifu, tunaweza kuona uvivu unavyozungumzwa, na hasara anazopata mtu mvivu.
Rejea:Uvivu humtia mtu katika usingizi mzito; Na nafsi yake mvivu itaona njaa. MIT. 19:15 SUV
Ukishaona una viashiria vya kupenda kulala sana kuliko kufanya kazi uwe na uhakika tabia ya uvivu imekuvamia, ukishajiona unapenda kupumzika sana kuliko kufanya kazi uwe na uhakika umevamiwa na tabia ya uvivu. Na mavuno ya mvivu ni hasara.
Wengi wetu tumeshindwa kujua hili, ndio maana wengi wanaendelea kushindwa kusoma Neno la Mungu. Mtu ametoka kwenye kazi zake, anaona bora kuzurura kwenye mitandao ya kijamii kuliko kusoma Neno la Mungu. Anachowaza kwenye kichwa chake ni amechoka sana, amechoka sana huku amemaliza lisaa limoja akiwa anaongea na simu au akiwa anachati.
Unakuta wale wanaobanwa sana na shughuli, na wasio wavivu, ndio hao hao wanaopata muda wa kufanya mambo mengi sana yenye faida katika maisha yao. Lakini wale wavivu wakishafanya jambo moja wanaona wamemaliza kila kitu, wala hawataki kujisumbua tena, ndipo inazaliwa misemo mbalimbali ya kulinda uvivu wao.
Mvivu ataona biblia ni kubwa sana, mvivu ataona kubeba Biblia kwake ni shida, mvivu ataona kusoma Neno na kutafakari Neno ni adhabu kwake. Lakini ukimpeleka kwenye habari zingine nje na Neno, anasoma hadi nukta ya mwisho kabisa.
Kama tunataka kufanikiwa tuache uvivu, uvivu ni sumu mbaya sana kwa mtu anayetamani kufanikiwa, ukiwa mvivu sana alafu ukawa unatamani vitu vizuri. Lazima utajiingiza kwenye vitendo viovu, hili linaingia pande zote mbili, maisha ya kimwili na kiroho.
Ili uwe na mafanikio kwenye jambo lolote unalofanya, epuka uvivu, hata kama unajisikia kuchoka sana, jisukume kwa nguvu kufanya hata kama kuna maumivu makali. Fanya tu, utaona ukizidi kwenda mbele badala ya kurudi nyuma.
Wakati mwingine unaweza usione ile raha katika usomaji wako wa Neno la Mungu, kutokana labda na uchovu wa mwili. Hilo lisikupe tabu, mwili wako unaujua vizuri, unaweza kujisukuma ukafanya jambo ulilopaswa kulifanya na mambo yakaendelea vizuri.
Hakikisha unaondoka kwenye eneo la uvivu, acha kujitengenezea sababu za kukufanya uonekane upo bize sana. Huko ni kujiundia sababu ya kujiangamiza mwenyewe, maana mwisho wa siku utajikuta huna akiba yeyote ya Neno la Mungu ndani ya moyo wako.
Epuka kuingia kwenye njaa ya kiroho, na hii imewashika wengi waliowavivu wa mambo ya Mungu. Unaweza kujiondoa kwenye eneo hilo la uvivu kwa kuanza kufanya mambo yako kwa ratiba na mpangilio mzuri.
Umefanikiwa kusoma ujumbe huu hadi hapa, wewe sio mvivu, hamishia nguvu hii hii kwenye Neno la Mungu. Hakikisha unakuwa na msimamo wa kujisimamia wewe mwenyewe katika hili la kusoma Neno la Mungu.
Mungu akubariki sana kwa muda wako.
Facebook: Chapeo Ya Wokovu
Email: chapeo@chapeotz.com
Blog: www.chapeotz.com
WhatsApp: +255759808081