Haleluya,

Kuna vitu vimeuteka ufahamu wetu kiasi kwamba tumevipa kipaumbele kikubwa sana, mtu yupo tayari kukosa kula chakula ila asikose habari fulani inayorushwa hewani. Mwingine yupo tayari kukosa ibada kanisani kwa sababu tu alikuwa anafuatilia habari fulani ambayo kwa namna moja haimwongezei chochote.

Tunaweza kulalamika kila siku hatuna muda, kumbe muda wetu mwingi tumeuweka mahali, unatumika vibaya pasipo faida yeyote. Hapa leo ndio tunapaswa kukumbushana hili, ili uweze kujua huwa unamwaga masaa yako eneo gani.

Hebu kaa chini ujifuatilie mwenyewe, ni habari gani huwa humalizi siku bila kuifutilia, ni hadithi/riwaya gani haipiti siku bila kuisoma bila kujalisha ina maneno mengi kiasi gani.

Rudi kwenye akaunti unazofuatilia kwenye instagram, Facebook, YouTube na blog. Hizo zote zina zinahusiana na mambo ya Mungu? Zina mchango wowote katika kukujenga kiroho? Au ni matukio tu ya kusisimua na wakati mwingine kukuvuruga akili yako.

Sisemi hupaswi kufuatilia mambo ya dunia inavyoenda, ninachozungumza hapa, ni vitu gani vimeutawala moyo wako kiasi kwamba huwezi kufurahia kumaliza siku yako bila kujua kinachoendelea… Nakutafakarisha hili ili ujue kosa unalolifanyaga kila siku pasipo wewe kujua kama unakosea.

Kusoma riwaya/hadithi zenye maadili na mafunzo mazuri sio vibaya, kufuatilia habari mbalimbali duniani sio vibaya, kufuatilia ukurasa unaorusha matukio ya kutisha na kusisimua sio vibaya kama hayakufanyi umkosee Mungu, na kufuatilia vichekesho mbalimbali vyenye mafunzo ya kukujenga sio vibaya.

Je moja wapo kati ya hayo, lipo lililoukamata moyo wako kiasi kwamba huwezi kufanya chochote mpaka umelitimiza? Kati ya hayo lipo linalochukua nafasi ya kuomba Mungu? Kati ya hayo lipo linalochukua nafasi ya kutohudhuria kanisani? Kati ya hayo lipo linalochukua nafasi ya kusoma Neno la Mungu? Kama lipo na limekufanya huwezi kufanya chochote, ujue unachokifanya ni kosa kubwa sana kuliko unavyofikiri.

Je unaweza kusoma vitabu vingine lakini Biblia yenye Neno la Mungu ndani yake huwezi kuisoma? Kama ni ndio, kuna mahali una shida, vitabu vingine haviwezi kuwa bora kwako kupita Biblia. Unaweza kujitetea kwa namna yeyote ile, ila kama wewe ni mkristo na unaona vitabu vingine vinafaa sana kusomwa kuliko Biblia. Nikuambie tu ukweli umetoka kwenye msingi mkuu wa maisha, kwa jinsi unavyofikiri.

Unalalamika huna muda wa kutosha lakini hukosi kufuatilia habari mbalimbali tena zenye kurasa ndefu, kubali una shida ya kiroho. Ambayo inapaswa kutatuliwa mapema iwezekanavyo, huwezi kujisikia kila siku kwenda kupunga upepo baharini wakati wa ibada.

Wewe ikifika muda wa ibada unaona heri uende ziwani kupunga upepo, ikifika muda uliojipangia kusoma Neno la Mungu unaona bora ukaangalie kinachoendelea kwenye mitandao ya kijamii. Unaona bora uingie YouTube uangalie videos mbalimbali, au unaona bora uende kijiweni.

Kila jambo linapaswa kufanyika kwa kiasi, kama kila siku unapiga kelele za huna muda wa kutosha kusoma Neno la Mungu. Alafu kwenye mambo mengine kama hayo niliyokutajia, unapatikana muda wote na unafuatilia kwa umakini. Unapaswa kufahamu umevamiwa na hali isiyo taka usogee kiroho.

Wakati mwingine tunapenda kusingizia tunabanwa sana na kazi, ila ukija kufuatilia kwa umakini. Unakuja kuona sio kazi zinawabana watu, ni vile kuna mahali wameacha muda wao mwingi ukimwagika ovyo kwenye maeneo mengine kabisa nje na kazi/huduma zao.

Funguka ufahamu wako, fika mahali jihoji inakuwaje unapenda kufuatilia habari zingine, ila ikija kwenye Neno la Mungu unakosa kabisa hamu ya kulisoma. Kaa chini ujihoji, ni kitu gani kinakufanya ukose Hamu ya Neno ambayo wewe unakuja kuiita, huna muda wa kutosha.

Omba Mungu akupe moyo wa kupenda Neno la Mungu, chukia hali ya kupenda kufuatilia sana maisha ya watu kuliko habari za Mungu. Fika mahali usikie moyoni mwako kupenda zaidi kufuatilia Neno la Mungu linasemaje juu ya maisha yako ya kiroho na kimwili.

Mungu akubariki sana kwa muda wako.

Facebook: Chapeo Ya Wokovu

Email: chapeo@chapeotz.com

Blog: www.chapeotz.com

WhatsApp: +255759808081