Nakusalimu katika jina la Bwana wetu Yesu Kristo aliye hai, siku nyingine tena mpya kabisa Bwana ametupa kibali cha kuweza kuiona tena. Sifa na utukufu tumrudishie yeye Bwana mwenza wa yote, anayeweza kutupa kushinda siku zote za maisha yetu.

Kwanza kabisa napenda kukushukuru kwa uvumilivu wako wa kutoonekana kwa muda, nimekuwa mapumziko kwa muda wa wiki moja sasa. Namshukuru Mungu kile kilinifanya niwe kwenye mapumziko kimeisha salama na sasa tutakuwa pamoja.

Leo tujifunze jambo hili la msingi sana, wengi wetu huwa tunajiingiza kwenye mambo ya Mungu kwa kutegemea kupata kitu fulani kwa wenzetu. Mfano ulio hai ni huu, tuna utaratibu wa kusoma biblia kila siku group la whatsApp la Chapeo Ya Wokovu. Wapo watu wanajiunga sio kwa lengo la kujifunza Neno la Mungu, lengo lao ni kuja kuvuna kitu fulani nje na kujijengea nidhamu ya kusoma Neno la Mungu.

Mtu akisikia Chapeo Ya Wokovu whatsApp group, huwa wanatiana moyo mtu anapokuwa na jambo lake kama harusi/sendoff/msiba. Anaona bora kujiunga ili akifika zamu yake ya kuoa/kuolewa, watu waweze kumchangia chochote. Anakuwa na bidii sana ili aweze kuonekana kwa wenzake, kweli baada ya kufika muda wake wa kuoa/kuolewa hata ile bidii yake inaondoka kabisa baada ya kutimiza lengo lake.

Hatuwezi kupeleka moja kwa moja mtu aliyeoana naye sio sahihi wala hatuwezi kusema baada ya kuoa/kuoelewa majukum yameongezeka. Hii utaiona mapema akikaribia kuoa/kuolewa bidii yake inabadilika kabisa, kama alikuwa mzembe wa kusoma Neno la Mungu na kutoa tafakari yake. Hiyo hali ya uzembe haitakuwepo mpaka pale watu wengine wamefanya jambo kwake, na baada ya hapo anapotea moja kwa moja.

Wengine hawafikii kigezo cha watu kushirikiana nao kwa michango ya fedha, wanapoona malengo yao hayakutimia. Unaona wanakata kamba njiani, yaani anapotea kabisa kwenye kusoma Neno la Mungu, anarudi kwenye maisha yake ya mwanzo aliyokuwa hasomi Neno la Mungu.

Huku ni kujidanganya mwenyewe unapoanza kusoma Neno la Mungu ili kuja kuvuna kitu fulani kutoka kwa wenzako, wasipotimiza kile ulikuwa unataka. Utapoteana vibaya sana na hutoonekana tena ukifanya bidii ya kusoma Neno la Mungu, jiwekee mtazamo hasi unaposoma Neno la Mungu.

Acha kutanguliza faida za kimwili unapoanza kusoma Neno la Mungu, wengine waanzisha magroup ya kusoma Neno la Mungu kwa kusudi la kuja kukusanya michango. Huu ni ujinga mbaya sana, maana wanaweza wasifikie lengo lao, na wasipofikia lengo lao lazima magroup yale yavunjwe au wakitimiza malengo yao na bidii yao ya kusoma Neno la Mungu inapotea kabisa.

Unapoamua kufanya mambo ya kiMungu, amua kutoka ndani ya moyo wako, fanya bila kutazama kupata faida fulani za kimwili. Hizo zitakuja zenyewe maana Mungu anajua wewe ni mhitaji, unaweza kufanya mambo kwa matarajio fulani ukaja kuangukia pua. Maana haitakuwa vile ulitaka iwe badala yake inakuja kugeuka kinyume kabisa.

Hii unaweza kuitumia mahali popote pale, usifanye kitu kwa kutazamia kuvuna faida kubwa kwa uliowafanyia. Utashangaa unajiumiza kwa sababu ulikuwa hufanyi kwa moyo wa kupenda, na matokeo yake watu hawatakuja kufanya vile ulitarajia wakufanyie. Hapo ndipo utapoanza kuona watu walivyo wabaya na kuanza kujenga chuki nao, maana sio wote unaojitoa kwao na wao watajitoa kwako.

Nakusihi sana ndugu yangu, kama umeanza kusoma Neno la Mungu kwa kutegemea faida fulani ya kimwili kabisa. Nakushauri uachane na hayo mawazo potofu, maana hutofika mbali itakuja kubaki simulizi ya uliwahi kujenga utaratibu wa kusoma Neno la Mungu.

Chochote unachoamua kufanya leo au chochote unachosikia moyoni mwako kuanza kumtumikia Mungu wako, hakikisha hutawaliwi na tamaa ya vitu vya mwili. Ukitanguliza kuvuna matunda ya nje, badala ya matunda ya ndani kwanza, utayakosa hayo matunda ya nje na hapo utakuwa mwisho wako wa bidii yako au utavuna yale ulitegemea kuvuna na hapo ndio utakuwa mwisho wako kufanya. Maana yale matarajio yako yatakuwa yameshatimia na ukija kuangalia mbele huwezi kufanya hilo jambo tena.

Lengo lako kuu liwe kumjua Mungu anasema nini kwenye maisha yako ya kiroho na kimwili kupitia Neno lake. Unapotafuta kujua kusudi la maisha yako kupitia Neno la Mungu, na unapotafuta kujua Mungu anakuelekeza nini juu ya maisha yako kupitia Neno lake. Kusoma kwako Neno la Mungu kutakuzalia matunda mengi sana, na hutokaa uache Kusoma Neno la Mungu. Maana utakuwa unapata mambo mengi mazuri usiyotamani kuyakosa katika maisha yako ya kila siku.

Uliingia Kusoma Neno la Mungu kwa picha ya kupata kitu fulani, badili leo mtazamo wako hasi. Anza kusoma Neno la Mungu kwa kutegemea kuvuna hekima za kiMungu zitakazoweza kukusaidia kukaa mbali na dhambi, na kuishi na watu vizuri.

Mungu akubariki sana kwa muda wako.

Facebook: Chapeo Ya Wokovu

Blog: www.chapeotz.com

Email: chapeo@chapeotz.com

WhatsApp: +255759808081