Bwana Yesu asifiwe sana, siku nyingine tena mpya kabisa Bwana ametupa kibali cha kuweza kuiona siku ya leo. Kwa akili ya kawaida na mazoea ya kila siku, unaweza kuona ni jambo la kawaida kulala na kuamka. Lakini sio jambo la kawaida kabisa, sio wote wanaolala wanaamka wakiwa wazima, ni neema ya Mungu tu kutupa uhai huu tulionao leo.
Nimekuwa nikisisitiza sana umhimu wa kusoma Neno la Mungu pamoja na wenzako/mwenzako mliyepatana kwa jambo hili. Mtu mliyewekeana ratiba ya kukutana pamoja kila siku kwa ajili ya kusoma Neno la Mungu. Naenda kusisitiza tena hili kwa namna hii;
Kama ilivyo kanuni ya mkristo yeyote kuhimizwa na Mungu kukutana/kukusanyika pamoja katika ibada za kanisani/vikundi. Katika kufundishana, kuonyana, na kuelekezana namna ya kuenenda katika njia sahihi zimpendezayo Mungu wetu.
Ipo faida kubwa sana katika kukusanyika pamoja kwa lengo moja la kusikia Mungu anasema nini juu ya maisha yenu, kupitia mtumishi wake aliyemwandaa kwa ajili ya kusema nanyi. Tofauti na mtu aliyekaa nyumbani huku akifikiri moyoni mwake kuwa hata asipoenda ibada za kanisani haina shida.
Ukitaka kufanikiwa kwenye baadhi ya maeneo, unapaswa kuwa na mtu mwingine anayeweza kukusaidia pale unaposikia kuchoka na kuacha. Unapofika mahali unasikia kurudi nyuma au kuacha kile ulichokuwa unafanya, ni rahisi mwenzako au wenzako kukushika mkono mkaendelea mbele.
Kuna wakati hupaswi kufa na mzigo peke yako, unapaswa kuwashirikisha wenzako mlionao pamoja na unaowaamini wanaweza kukusaidia kwa namna unayoona moyoni itakufaa. Tofauti na kuwa peke yako, huku ukiendelea kuumia na mzigo ambao ungekuwa na wenzako wangekusaidia kukubeba.
Unaweza kubebwa kwa namna nyingi sana, unaweza kubebwa kwa namna ya kutiwa moyo kwa maneno ya faraja pale unapokata tamaa, unaweza kubebwa kwa maombi ya wenzako, unaweza kubebwa kwa namna ya kupewa hitaji lako. Inaweza ikawa fedha au kitu chochote kile ulichokuwa mhitaji lakini ukawa umekosa msaada kutokana na hali yako.
Usomaji wa Neno la Mungu, watu wengi sana wanashindwa kuzoea zoezi hili yaani wakalifanya jambo wanalopaswa kulifanya kila siku. Bila kusukumwa na mtu yeyote yule, ila badala yake wamejikuta wanaanza vizuri na kuishia njiani.
Kumbuka hili jambo la kusoma Neno la Mungu, tunajifunza tukiwa wakubwa, tofauti na tungejizoeza tukiwa watoto wadogo. Tunapojifunza tabia mpya ukubwani, kuna changamoto zake ngumu ambazo unapaswa kutafuta namna ya kukabiliana nazo ili usije ukarudi nyuma kizembe.
Kwa kuwa tunajifunza hili jambo ukubwani, ni vizuri ukawa na rafiki anayeweza kukusaidia pale unaposikia kuchoka. Akaweza kukuhimiza na wewe ukawa na uwezo wa kumsikiliza, yaani mtu unayeheshimiana naye, akikuambia fanya hili unaweza kufanya bila kusitasita.
Unapokuwa huna rafiki wala kikundi chenye kufanya kile unataka kufanikiwa nacho, mara nyingi sana ni rahisi kuanza vizuri na kuishia njiani. Maana hakuna mtu anayekufuatilia, na kupitia nafasi hiyo unaweza kuacha kabisa kusoma Neno la Mungu.
Angalia marafiki walioshibana, tabia zao zinafanana sana, matendo yao na ongea zao mara nyingi zinafanana sana. Hata mitazamo yao ya kimaisha inafanana sana, akitokea mmoja anataka kwenda kinyume chao, ni rahisi mno kupingwa na kurejeshwa kwenye mstari mmoja.
Unapokuwa na marafiki wengi ambao hawapendi kusoma Neno la Mungu, na wewe ukawa unaanza kujifunza kujenga nidhamu ya kusoma Neno la Mungu kila siku. Uwe na uhakika wa kukuvunja moyo wa kushindwa kuendelea mbele ni hao hao marafiki zako.
Ukiwa na mke/mume asiyependa kusoma Neno la Mungu, alafu ukawa huna marafiki wengine wanaokuhimiza pale unapokatishwa tamaa au ukawa nao hao marafiki. Ila ukawa huwasikilizi au ukawa hufuati taratibu mlizojiwekea, ni rahisi sana kuacha kabisa kusoma Neno la Mungu.
Rejea:Afadhali kuwa wawili kuliko mmoja; Maana wapata ijara njema kwa kazi yao. Kwa maana wakianguka, mmoja wao atamwinua mwenzake; lakini ole wake aliye peke yake aangukapo, wala hana mwingine wa kumwinua! MHU. 4:9-10 SUV.
Nimekupitisha kwenye maandiko matakatifu ili uweze kuona uzito wa hili jambo ninalokueleza hapa, kusimama peke yako kwa kila jambo ni ngumu sana. Unapaswa kuwa na mtu/watu wanaoweza kukubeba pale unapochoka, pale unapoanguka unapaswa uwe na mtu wa kuweza kukuinua tena.
Mungu akubariki sana kwa muda wako.
Facebook: Chapeo Ya Wokovu
Blog: www.chapeotz.com
Email: www.chapeotz.com
WhatsApp: +255759808081