Haleluya, siku nyingine tena mpya kabisa Bwana ametupa kibali cha kuweza kuiona, sifa na utukufu tumrudishie yeye Bwana mwenza wa yote.
Tufike mahali tujihoji wenyewe tumetiwa ganzi ya namna gani, kiasi kwamba huwezi kusikia msukumo wa kusoma Neno la Mungu. Wakati mwingine tunaweza kuona ni jambo la kawaida, ila ukweli haliwezi kuwa jambo la kawaida kabisa, ikiwa ndani mwetu hatujisikii hamu ya Neno la Mungu.
Pamoja na kusikia sana faida za Neno la Mungu, bado ndani mwako huna kiashiria chochote kinachoonesha huyu mtu ana kitu alichokiona ndani ya Neno la Mungu.
Unawashangaa wenzako wakiwa wanakimbizana na muda ili wakasome Neno la Mungu, ila wewe huna hata mshtuko ndani mwako wa kuonyesha na wewe u mhitaji kama wenzako.
Hali kama hizi sio za kunyamazia ukiwa kama mkristo aliyeamua kumfuata Yesu Kristo kisawasawa bila kupinda kona yeyote. Lakini ukikaa na kuona kawaida, itaendelea kukugharimu kwa kubaki na hali yako ya kutokusoma Neno la Mungu.
Nimeona mara nyingi, kuna baadhi ya ndugu katika Kristo, wanapata shida sana mioyoni mwao wanapoona wengine wanasoma Neno la Mungu na kulielewa vizuri. Hawa watu wakipata watu wa kuwatia moyo, huwa wanakuwa wanafunzi wazuri sana wa Yesu Kristo.
Tofauti na wale wanaoona kawaida ndani yao na hawaumii yaani hawana msukumo wowote ndani yao, wawe wamesoma Neno la Mungu au wawe hajasoma Neno la Mungu kwao wanaona sawa tu.
Tabia hii imewashika hasa wale waliokoka siku nyingi, wanaona wao sio wahitaji sana, kumbe wao ndio wanapaswa kuwa mstari wa mbele katika hili. Ila utashangaa wanaong’ang’ana na kusoma Neno la Mungu ni wale waliokoka siku sio nyingi.
Moja ya mahitaji muhimu sana ya kumweleza Mungu kwa machozi mengi ni pamoja na hili la kushindwa kusoma Neno la Mungu. Hushindwi kusoma tu, hata ile hamu ya kukusukuma uchukue biblia yako uanze kusoma, huna kabisa ndani yako.
Utafanya jambo la maana sana kama utaanza kujiombea kwa hili, huku ukiendelea kujisukuma kwa nguvu kusoma Neno la Mungu. Hata kama hujisikii ile ladha nzuri unayoisikia kwa wenzako wakiisema, jitahidi kusoma tu. Kadri unavyozidi kuweka juhudi ndivyo na hiyo ladha itaanza kutengenezeka ndani yako.
Tofauti na kuweka juhudi zako na kuwa na nidhamu katika hili la kusoma Neno la Mungu, utajiombea sana ila utashangaa unaanza vizuri sana. Ila ukishafika katikati unaacha kabisa kusoma Neno la Mungu, ukiguswa kwanini husomi Neno la Mungu, sababu ya kwanza utaanza kusema umebanwa sana na majukumu huna muda. Kumbe muda unao wa kutosha sema ndani yako huna msukumo wowote.
Usiwe mkristo asiye na tabia za mtu aliye na safari inayohitaji kujiangalia kila wakati kama yupo vizuri, kipimo chetu cha kutupima afya zetu za kiroho ni Neno la Mungu. Ndilo linatupa uhakika mahali tulipo tupo sahihi ama tumegeuka, maana wakati mwingine tunaweza kujiona tupo vizuri Kumbe tumeshapoteza dira siku nyingi.
Nimekueleza mengi ya kukuonyesha hali uliyonayo ya kutokupenda Neno la Mungu wala kutokusikia msukumo wowote ndani yako, hali hiyo sio nzuri kwako. Cha kufanya ni kuanza kufanyia kazi moja baada ya jingine unapoliona limechangia kukufanya usiwe na msukumo ndani yako.
Kama bado hujaungana nasi katika group la whatsApp, la kusoma Neno la Mungu, unakaribishwa sana kwa kutumia namba hizi 0759808081(tumia whatsApp kuwasiliana nasi).
Na ambao tupo pamoja group la whatsApp la Chapeo Ya Wokovu, tuendelee kuweka juhudi za kusoma Neno la Mungu. Hakikisha unajiona unapanda juu kadri siku zinavyozidi kwenda mbele, epuka kuwa pale pale kila siku.
Mungu akubariki sana kwa muda wako.
Facebook: Chapeo Ya Wokovu
Email: chapeo@chapeotz.com
Blog: www.chapeotz.com
WhatsApp: +255759808081