Nakusalimu katika jina la Bwana wetu Yesu Kristo aliye hai, jina tunalojivua, jina litupalo kushinda, jina ambalo pepo wakilisikia likitajwa humtoka mtu. Fursa kwetu kwenda kumzalia Bwana wetu Yesu Kristo matunda yaliyo mema kupitia jina lake takatifu.
Unaweza kukwazika na kuumia kwa kukuambia maneno haya ila nina imani mpaka kumaliza kusoma ujumbe huu, utakuwa umepona mahali. Nia yangu sio nikuumize, nia yangu uone mahali unapokosea ili uweze kujirekebisha kama utapenda kufanya hivyo.
Najua utakuwa sio mgeni sana na hali hii ya kuhamasika kwa baadhi ya vitu/mambo, ila huwa unaishia hapo na huwa huchukui hatua yeyote ile ya kukufanya uwe vile kama ulivyotamani kuwa.
Kweli sio kila jambo utakalolisikia na likagusa moyo wako, linaweza kuwa kwako, mambo mengine Mungu amempa zawadi kila mmoja wetu kutokana na jinsi alivyopenda yeye. Lakini yapo mambo inakulazimu utumie uwezo aliokupa Mungu ili uweze kufanikiwa katika hayo.
Chukulia wokovu ni wa kila mtu, ila ni wachache sana wanaodumu ndani ya wokovu, ni wachache sana wanamaliza safari yao hapa duniani wakiwa ndani ya Yesu Kristo. Hapa unaweza kuona ni jinsi gani sio kila jambo la bure, kila mmoja anaweza kusimama nalo mpaka mwisho.
Kuokoka huhitaji uwe na mali nyingi sana wala huhitaji uwe mzee ndio uokoke, kuokoka ni sasa. Kama ni sasa, ni wangapi leo walianza safari hii ya wokovu ila wamerudi nyuma wengi? Safari hii sio rahisi japo ni bure kuokoka. Unapaswa kupambana kuhakikisha unamaliza salama safari uliyoanzisha.
Leo hii ukimweleza mkristo habari ya kusoma Neno la Mungu, atahamasika sana, tena mwingine anaweza kubadilika na sura kabisa kuonyesha ameguswa na hili jambo. Ila ataanza hili zoezi kwa muda mfupi sana, baada ya muda huo mfupi anapoteana kabisa.
Siku nyingine akisikia mtumishi wa Mungu anaongelea habari ya kusoma Neno la Mungu, atainuka tena kwa kuhamasika sana. Ukimwangalia utasema hakika huyu mtu anaye kiu ya kusoma Neno la Mungu bila kuacha, cha kushangaza hali hiyo inadumu ndani ya wiki tu au akienda sana labda mwezi.
Mungu wetu ni mwaminifu sana kwetu wanadamu, huwa haachi kutukumbusha hili kupitia watumishi wake. Sasa utakuta kila mara umekuwa mtu wa kuhamasika tu bila kuchukua hatua inayokupasa ili uweze kufanikiwa katika hilo.
Leo unaweza kusikia somo kama hili la kukuhimiza usome Neno la Mungu, utainuka kwa nguvu kubwa. Na wakati mwingine utaanza kujuta kwanini hukuendelea kusoma Neno la Mungu tangu kipindi kile umeanza hili zoezi. Badala hayo maumivu uliyonayo ya kuachia njiani kusoma Neno la Mungu, unaanza kidogo na kuacha tena.
Labda nikuulize tu rafiki yangu, ndugu yangu, mama yangu, baba yangu, mdogo wangu. Umewahi kukaa chini na kujihoji kwanini huna hamu ya kusoma Neno la Mungu? Utasema hamu ipo, hamu gani isiyokupelekea kusoma Neno la Mungu?
Unasema umeokoka miaka mingi, huu wokovu ni wa namna gani usiokusukuma uwe na kiu ya Neno la Mungu? Maana chakula chako cha kiroho ni Neno la Mungu, sasa wewe huwa umeshiba chakula gani?
Unasingizia huna muda, Mungu akusamehe ndugu kwa hilo, maana kuna mahali unapoteza muda mwingi sana na wewe unaona unachofanya. Yapo maeneo yanakula sana muda wako, na hayana sababu yeyote kabisa kula muda wako.
Ungekuwa hujaokoka tungesema umeshikiliwa na nguvu za giza, zinazokuzuia kusoma Neno la Mungu. Lakini unakiri mwenyewe umeokoka na Yesu Kristo ni Bwana na Mwokozi wa maisha yako, na kweli unajiona humtendi Mungu dhambi.
Kinachokufanya usisome Neno la Mungu ni pepo gani hilo? Yaani wewe unaishiaga kuhamasika tu. Yaani umekuwa kama wale watu ambao wanasikiaga moyoni kuokoka kwenye matatizo, ila wakishatoka kwenye hayo matatizo. Na wokovu wanaacha.
Ondoka kwenye eneo la kuhamasika bila vitendo, ingia kwenye eneo la kuhamasika huku ukiendelea kufanya vizuri zaidi kwa vitendo. Yaani sikia kiu ikiongezeka zaidi siku hadi siku kadri unavyozidi kujifunza Neno la Mungu, acha mhamasiko hewa usio na hatua zozote unazochukua.
Mwaka unaisha, na mwaka huu ulivyokuwa unaanza ulisema utasoma sana Neno la Mungu. Hili halihitaji uwe na mtaji, wala halihitaji uwe na pesa, labda ingekuwa vitabu vingine ungesema hujaweza kununua kutokana na hali ya uchumi. Biblia unayo, na kama huna ya kununua dukani, ila hapo ulipo una kifaa chako cha smartphone, tablet au laptop. Kitumie hicho kusoma Neno la Mungu.
Chukulia hili kwa uzito mkubwa ili uweze kufanikiwa katika eneo hili la usomaji wa Neno la Mungu. Pia unakaribishwa kwenye group la whatsApp la kusoma Neno la Mungu kama bado hujajiunga nalo, tumia namba hii0759808081 kuwasiliana nasi whatsApp ili uweze kuungana na wenzako.
Mungu akubariki sana kwa muda wako.
Facebook: Chapeo Ya Wokovu
Email: chapeo@chapeotz.com
Blog: www.chapeotz.com
WhatsApp: +255759808081