Nakusalimu katika jina la Bwana wetu Yesu Kristo aliye hai, siku nyingine tena mpya kabisa ambayo inatupa fursa ya kwenda kumzalia Bwana matunda yaliyo mema.
Yapo mambo mengi sana huwa tunayaonea haya/aibu kutokana na mapokeo ya mila zetu au jamii inayotuzunguka, kututengeneza kuwa hivyo tulivyo leo.
Wakati mwingine huwa nzuri kuwatengeneza watoto vile, ila ni mbaya kama hawatajulishwa wakiwa wakubwa kuwa walikuwa wanafundishwa hivyo ili kuepuka kupotea. Badala yake mtu anakuwa mkubwa bado anayo ile hali yake ya mafundisho ya utoto aliyokuwa nayo.
Mfano unakutana na wana ndoa wanaoneana aibu hadi leo, pamoja na kuwa mke na mume yaani mwili mmoja. Bado wanaoneana aibu kubwa kiasi kwamba inakuwa kero kwao, maana wanafikiri ni dhambi wakifanya kile kitamfurahisha mwenzake.
Tunaweza kuwalaumu watu hawa ila ukweli upo, malezi waliyolelewa yamewafanya wawe hivyo. Kosa lao labda linaweza kuwa hawakutaka kujifunza zaidi, wamebaki na mapokeo ya mila zao.
Kukosa maarifa sahihi kunawafanya watu wengi waendelee kuona wanachofanya ni sahihi, na wengine waendelee kuona wanachokiogopa kufanya wapo sahihi. Kumbe hawapo sahihi ila kutokana na upeo wao kuwa mdogo wanajinyima vitu vya msingi, ambavyo wangevifanya vingeleta baraka kwao na mbele za Mungu.
Tutawezaje sasa kuondoka kwenye eneo hili la ujinga? Vizuri tukajikita kusoma Neno la Mungu, yapo mambo mengi sana tutayajua yaliyo sahihi kuyafanya. Na yapo mambo mengi sana tutayajua yasiyo sahihi kwetu kuyafanya, hata kama kwa wengine yanaonekana yapo sawa.
Wakati mwingine tumewapa watu majina ya tofauti kutokana na matendo yao, tukiwaona wanafanya mambo ya tamaduni zingine nje na malezi yao. Utasikia huyu ndugu ana mambo ya kizungu sana, kinachomfanya aitwe hivyo ni matendo yake.
Tumefikia mahali tunaona mambo mengine ni tamaduni za kizungu, kumbe sio tamaduni za kizungu. Ila ndivyo inavyopaswa iwe kwa watu wote, ila kutokana na kukosa maarifa sahihi, tunaona hayo ni mambo ya kizungu.
Sikuambii kila jambo la tamaduni zetu ni baya, nataka kukusaidia kuelewa kwamba yapo mambo yamechukua nafasi kubwa. Kiasi kwamba yamekuwa na nguvu kuliko mafundisho sahihi ya Neno la Mungu, yaani mtu anaweza kupingana na maandiko matakatifu kutokana na vile alivyokua akakuta jamii yake inaishi hivyo.
Kuna wakati tunashauriwa kutembelea sehemu mbalimbali, inatusaidia kuondoa baadhi ya misimamo ambayo tuliishikilia kwa kufikiri ndivyo tunapaswa kuishi maisha hayo.
Kuna vitu ni dhambi usipovifanya kwa wakati sahihi, mfano mzuri ni tendo la ndoa, likifanywa na watu ambao hawajaoana ni dhambi. Ila tendo ni lile lile halina tofauti kabisa na mtu aliyeoa/aliyeolewa.
Hebu tujikite kusoma Neno la Mungu, hii itatusaidia kuepuka kuonea mambo mengine aibu. Kiasi kwamba tunakosa uhuru wa kuyafanya vitu kwa kufikiri ni dhambi.
Mambo mengine huyaonei aibu tu, unayaona ni dhambi moja kwa moja na ukiona mwingine anafanya. Unamwona anamtenda Mungu dhambi, kumbe ni kukosa kwako maarifa sahihi, kumbe ni mapokeo yako mabaya ndio yanakufanya uone hivyo.
Amka ndugu, huu sio wakati wa kulala, kamata biblia yako usome mwenyewe bila kusukumwa na mtu yeyote. Hakikisha unamkaribisha Roho Mtakatifu aweze kukusaidia kuelewa vizuri zaidi, maana Neno la Mungu ni tofauti na kusoma gazeti.
Mila zinaweza kukupotosha ila Neno la Mungu litakuambia ukweli, dini yako inaweza kukuficha vitu vingi ila Neno la Mungu litakufichulia kila kitu. Utaamua mwenyewe kuendelea kubaki njia panda au kujitoa kwenye hiyo njia panda, kwa kusoma mwenyewe Neno la Mungu.
Mungu akubariki sana kwa muda wako.
Facebook: Chapeo Ya Wokovu
Blog: www.chapeotz.com
Email: chapeo@chapeotz.com
WhatsApp: +255759808081