Nakusalimu katika jina la Bwana wetu Yesu Kristo aliye hai, siku nyingine tena mpya kabisa Bwana ametupa kibali cha kuweza kuiona. Fursa kwetu kwenda kumzalia Bwana wetu matunda yaliyo mema.

Tukubali ukweli huu, tusipoukubali tutaendelea kubaki eneo hilo hilo kila siku bila kusogea hatua zozote. Kukubali ukweli inakufanya ujue cha kufanya, inakufanya uanze kufikiri hatua gani za kuchukua ili uweze kutoka kwenye kifungo ulichopo.

Wakati mwingine tunakataa ukweli kwa kisingizio cha kutokubali udhaifu, ila tunapaswa kujua udhaifu sio kukiri ukweli. Udhaifu tunaweza kusema ni kule kukosa imani kwa Yesu Kristo, unaanza kuishi kwa kutumia akili zako na kufika mahali unaona Yesu Kristo hawezi kukusaidia tena.

Wakristo tulio wengi ni wachanga wa kiroho, haijalishi umri mkubwa wa mwamini. Bado wengi sana ni wachanga wa kiroho kutokana na kukosa maarifa sahihi, ambayo ni Neno la Mungu.

Shida ya uchanga wa kiroho, wengi wetu hatuwezi kuiona kutokana na kujiona tupo vizuri kiroho. Maana mtu anakuwa anajiona amejazwa na Roho Mtakatifu, na hatendi tena zile dhambi zinazojulikana kama vile ulevi, uzinzi, uasherati, wizi na nyingine nyingi maarufu unazozifahamu.

Anapojiona hatendi hizo dhambi, anaona hana haja na mambo mengine zaidi ya kuendelea kutokutenda hayo anayoamini ndio akifanya atakuwa amemtenda Mungu dhambi. Badala yake huyu mtu ataenda kwa muda fulani, utamshangaa ameanguka njiani kwa yaleyale aliyoona hawezi kuyatenda, na akinyanyuka utamkuta ameanguka tena.

Kujiona kabisa una shida ya uchanga wa kiroho, inakuwa ngumu kutokana na jinsi vile tumeokoka, na kukuta wale tunaowaamini, hawajawahi kutukazania hili ninalokuambia hapa.

Uchanga wa kiroho umekuwa mzigo kwa waamini wengi, na wamegeuka kero kwa watu wengine kutokana na wao wenyewe hawajui kama wanayoyatenda wanakosea. Wanajiona wapo sahihi, na ukijaribu kumrejesha anakuwa na mgumu kuelewa kwa sababu anachojua ni ameokoka.

Mkristo kufikiri akishaokoka imetosha, ndio inamfanya aendelee kuwa mtoto katika akili zake, na hili yeye kama yeye hawezi kujitambua haraka mpaka pale atakapotoka kwenye utoto huo aliokuwa nao.

Rejea: Ndugu zangu, msiwe watoto katika akili zenu; lakini katika uovu mgeuzwe watoto wachanga, bali katika akili zenu mkawe watu wazima. 1 Wakorintho 14:20 SUV

Tutakuwaje watu wazima katika akili zetu? Maana yake kama ni wachanga wa kiroho, tunafananishwa na watoto wadogo, na Mungu hataki tuwe watoto kwenye akili zetu. Ila anatutaka tugeuzwe watoto kwenye uovu, bali tunapaswa kuwa watu wazima katika akili zetu.

Tutakuwa watu wazima kwa kupenda kusoma wenyewe Neno la Mungu, na tutakuwa watu wazima kwa kupenda mafundisho sahihi ya Neno la Mungu.

Ikiwa kama watu tuliozaliwa mara ya pili, tunapaswa kupenda kujifunza Neno la Mungu kuliko wakati mwingine wowote. Bila kuangalia umri mkubwa ulionao, ilimradi una safari ya kwenda mbinguni na unapenda kukomaa kiroho. Utapaswa kulijua Neno la Mungu, kwa kusoma mwenyewe au kwa kusikiliza mafundisho kanisani kwako, kwenye semina/mikutano ya watumishi wa Mungu au kusoma vitabu vyao au kusikiliza DVD/CD zao.

Hizo zote ni njia ya kuukulia wokovu na kutoka kwenye eneo la uchanga wa kiroho, na usipofanya bidii katika hili. Tutakuona leo upo vizuri baada ya kuokoka, lakini baada ya muda mfupi utamtenda tena Mungu dhambi kwa sababu ya kukosa msingi wa Neno la Mungu.

Rejea: Kama watoto wachanga waliozaliwa sasa yatamanini maziwa ya akili yasiyoghoshiwa, ili kwa hayo mpate kuukulia wokovu. 1 Petro 2:2 SUV

Hatuwezi kuukulia wokovu kwa maneno, tunapaswa kupenda kujifunza Neno la Mungu. Wakati mwingine tunaweza kusubiri kanisani kupata masomo ya kutusaidia na tusiyapate kwa wakati mwafaka kutokana na mwingiliano wa mambo mbalimbali. Ila kwa kusoma mwenyewe Neno la Mungu huku ukimwomba Roho Mtakatifu akusaidie kuelewa unachosoma, utapata maarifa mengi sana.

Toka kwenye eneo la utoto wa kiroho, kwa kuilisha akili yako chakula kisichokugushiwa na mapokeo ya dini/dhehebu lako. Utaanza kuona matokeo tofauti na jinsi ulivyokuwa unajiona mwanzo.

Mungu akubariki sana kwa muda wako.

Facebook: Chapeo Ya Wokovu

Email: chapeo@chapeotz.com

Blog: www.chapeotz.com

WhatsApp: +255759808081