Bwana Yesu asifiwe, siku nyingine tena Bwana ametupa kibali cha kuweza kukutana tena katika kupeana maarifa ya kukusaidia kushinda baadhi ya maeneo uliyo dhaifu.

Zipo tamaduni zimeweza kutufanya mpaka tunaona Biblia imekosea baadhi ya maeneo, maana kuna vitu tunaona ni dhambi kuvifanya wakati Neno la Mungu linaturuhusu kufanya. Vile vile yapo mambo tunaona ni halali kuyafanya wakati Neno la Mungu linatukataza kabisa kuyafanya hayo.

Ukikutana na utamaduni wa kabila fulani unaojua kusimamia kanuni zao, na wewe ukawa miongoni mwa kabila hilo. Uwe na uhakika utakuwa na hofu ya kuvunja taratibu za kimila zilizowekwa kwa misingi imara.

Usipokuwa na misimamo ya kweli, unaweza kujikuta unashindwa kutoka kwenye kifungo hicho. Maana yapo matishio mengi nyuma yake, ambayo mengine unaona ni hatari kwako.

Unahitaji kujengewa ujasiri wa kiMungu ndani yako, tena ujasiri mkubwa ambao utakupasa uwe na maamzi ya mtu aliyekomaa kiroho. Usipokomaa kiroho na usipoongozwa na Roho Mtakatifu, yapo maamzi utafanya yasiyo sahihi. Baadaye utakuja kujuta kwanini ulichukua uamzi wa namna ile.

Huwezi kuamka siku moja ukaweza kubadilisha utamaduni uliojengwa mababu na mababu, haitajalisha umeijua kweli ya Mungu aliye hai. Unahitaji kujua namna ya kuendana nao, maana ni ndugu zako huwezi kuacha kushirikiana nao, japo wanapaswa kujua mipaka yako ya kushiriki baadhi ya vitu.

Unajiuliza watajuaje mipaka wakati hata kuokoka kwako kwenyewe kunawapa shida, usipate shida sana kwenye eneo hilo. Wala wewe hutowaambia, tayari wenyewe wanajua mtu akishaokoka anakuwa na tabia gani.

Upo utamaduni mpya wa mtu aliyeokoka kweli, haijalishi utapita kwenye changamoto ngumu ya kutengwa na wazazi, ndugu, jamaa na marafiki. Wanajua kabisa wakristo huwa wana tabia gani, ndio maana unaweza kukutana na mtu akakupa jina la baba/mama mchungaji/mlokole, ni vile tu mwonekano na matendo yako yanaonyesha kama walivyo wachungaji/walokole.

Utamaduni ni mzuri na upande mwingine sio mzuri kabisa, Utamaduni unaweza kukupandia mbegu mbaya kiasi kwamba ukaanza kuona maandiko matakatifu yanakosea kabisa yanapokukataza jambo unalolipenda.

Vizuri tukajenga utaratibu wa kusoma Neno la Mungu, haijalishi tumeokoka kwa muda mrefu, tunaweza kuwa tumeokoka muda mrefu ila tunaishi kwa mtazamo wa tamaduni zetu za kimila. Tukifikiri ndivyo tunavyopaswa kuishi maisha ya kiroho, kumbe tumeshikilia vitu ambavyo vinatuposha na vinapotosha kweli ya Mungu.

Unaweza kuwa shahidi mwenyewe, ulivyokuwa mwanzo kabla hujaokoka, kuna vitu uliona upo sahihi kabisa kuvifanya. Ila ulivyoingia ndani ya wokovu, ukaanza kuona uliyokuwa unayafanya hayakuwa sahihi kabisa.

Utajuaje sasa unaishi katika kweli? Ni kwa kusoma Neno la Mungu, na kuliweka moyoni mwako. Unaweza kuwa shahidi wa watu wengi wamekuwa wakitenda dhambi kwa kutazama tamaduni zao. Neno la Mungu haliangalii utamaduni wa mtu, Neno la Mungu linatuweka katika njia moja ya Yesu Kristo.

Utamaduni wa kabila lako unaweza kuwa umekulea vizuri katika maadili mazuri, kumbe uzuri huo unauona mwenyewe. Maana unaweza kuwa umefundishwa kuheshimu miungu ya kwenu, na wewe ukawa umelishika sana hilo bila kujua Mungu anakataza kabisa hilo.

Sikuambii uache kuheshimu utamaduni wa kwenu, kama umegundua kuna vitu haviendani na Neno la Mungu hakuna haja ya kuendelea kushikilia vitu vitakavyokupeleka jehanamu. Hajalishi kabila lako ni zuri kiasi gani wala hajalishi ni maarufu sana duniani, kama linaenda kinyume na maandiko matakatifu, unapaswa kutoka kwenye kifungo hicho.

Mungu akubariki sana kwa muda wako.

Facebook: Chapeo Ya Wokovu

Email: chapeo@chapeotz.com

Blog: www.chapeotz.com

WhatsApp: +255759808081