Nakusalimu katika jina la Bwana wetu Yesu Kristo aliye hai, tunapaswa kumshukuru Mungu kwa kutupatia siku nyingine tena mpya. Fursa kwetu kwenda kumzalia Bwana matunda yaliyo mema.

Kukosa maarifa sahihi ya Neno la Mungu inasababisha wengi wetu tujazwe hofu nyingi sana. Ambazo hofu hizo zinakuwa kama mateso kwetu, maana ukishakuwa na wasiwasi mwingi au hofu nyingi, hata ufanisi wako kiutendaji unapungua.

Wakati mwingine hofu hizi zimetufanya tuone hata kuokoka kwetu hakuna faida yeyote, ni vile tu tumejazwa taarifa hasi nyingi ndani mwetu. Ambazo zinatufanya kuwa njia panda kwa jambo fulani pasipo kujua namna ya kufanya.

Unaweza ukateswa na mambo ya nyuma wakati hujaokoka, ukashangaa shetani akatumia mawakala wake kukujaza hofu zisizo na msingi. Ukabaki unahangaika na hizo taarifa, hiyo hofu uliyojazwa kwenye ufahamu wako inakutafuna kiasi kwamba unaanza kuona kuokoka kwako hakuna maana.

Unaweza kujishangaa umeachana na mambo mabaya ya nyuma, lakini bado yanakunyanyasa na kukutia hofu nyingi. Kila ukifikiri unaona kama vile yanakuja kutokea tena kwako, au unakuwa mtu wa kukosa furaha kila siku.

Wakati mwingine unaweza kujishusha thamani ya utu wako kutokana na hofu uliyoijaza moyoni mwako. Ukitaka kutoka kwenye kifungo hicho, unashangaa unashindwa kutoka kwenye kifungo hicho.

Unachopaswa kujua ni kwamba, uchanga wa kiroho unakutesa, pamoja na kuambiwa Yesu Kristo alishabeba mizigo yako. Wewe bado umebeba mizigo ambayo imekuwa ikikupa shida kubwa katika maisha yako.

Umeokoka lakini hujawahi kufurahia maisha yako ya wokovu, umejaa hofu kiasi kwamba unashindwa kulala usiku ukiwa peke yako. Unahisi vitu vya ajabu ambavyo vingine umevijaza mwenyewe kutokana na kupenda kubeba kila jambo unalolisikia.

Ukiona mkristo yeyote amejaa hofu nyingi, ujue kuna mawili, ni mchanga wa kiroho, au ni vuguvugu yaani bado hajasimama katika kweli ya Mungu.

Ili kutoka kwenye tabu hii kubwa inayokusumbua, vizuri ukaamua kutoka kwenye kifungo hicho cha uchanga wa kiroho. Maisha ya kuishi kwa hofu hata kwa mambo madogo yasiyopaswa uwe na hofu, ni mateso kwako kama hutoamua kujiondoa kwenye eneo hilo.

Kuondoka kwenye hofu hii ni kulijaza Neno la Mungu kwa wingi ndani yako, kadri unavyozidi kujifunza Neno la Mungu, ndivyo na hofu inazidi kuondoka hatua kwa hatua. Baadaye unakuja kujiona upo salama kabisa ndani ya maisha yako ya wokovu, na ndani yako inakuja ile hofu ya kiMungu kabisa itakayokuzuia kutenda mabaya.

Soma Neno la Mungu kwa kumaanisha haswa, yale unayosoma yaamini halafu yaweke katika matendo yako. Ona ni halisi kabisa na yanakuhusu wewe unayesoma, usisome Neno la Mungu ukiwa na mawazo hasi juu yake.

Ukikosa imani na Neno la Mungu, hata ukisoma hutopokea kitu chochote kile. Utasoma kama habari fulani hivi kwenye gazeti, habari isiyo na uzito wowote kwako, ni kama unaburudisha akili yako.

Kuishi maisha ya wasiwasi yaliyojaa hofu nyingi zinazokutesa maisha yako, sio jambo la kuacha kabisa liendelee kukusumbua siku zote za maisha yako. Amua leo kutoka kwenye eneo hilo la uchanga wa kiroho, hata mtu akikujia na imani yake potofu uwe na uwezo wa kumtambua.

Zipo imani nyingi potofu, usipokuwa na Neno la Mungu la kutosha, utashangaa wanakujaza hofu za kutosha, na utaanza kujiona mahali ulipokuwa sio sahihi. Japo inawezekana kuwa sehemu isiyo sahihi, huku wewe unaona ni sahihi. Huko nako ni kukosa maarifa sahihi ya Neno la Mungu.

Kataa hofu zinazokunyima usingizi kwa kutumia nafasi za uchanga wako kiroho, muda wako mwingi ujikite kulijua Neno la Mungu, kwa kulisoma na kulifakari.

Mungu akubariki sana kwa muda wako.

Facebook: Chapeo Ya Wokovu

Email: chapeo@chapeotz.com

Blog: www.chapeotz.com

WhatsApp: +255759808081