Asifiwe Yesu Kristo, siku nyingine tena mpya kabisa Bwana ametupa kibali cha kuweza kuiona tena. Tuna kila sababu ya kumshukuru Mungu, na kumrudishia sifa na utukufu kwake.

Vigumu kueleweka kwanini watu wanasoma maandiko matakatifu na wengine wanasikia Neno la Mungu likihubiriwa. Lakini bado hawataki kubadili misimamo yao ya kiimani/kidini, kwa akili za kawaida unaweza kuteseka sana na ukaumiza kichwa sana.

Pamoja na kuumizwa moyo wako unaweza usipate jibu la moja kwa moja, kama hutolitazama hili jambo kiroho. Na kama hutojua Neno la Mungu lilishalisema hili tangu mwanzo.

Rejea: Mwanadamu, wewe unakaa kati ya nyumba iliyoasi, watu ambao wana macho ya kuona, ila hawaoni, wana masikio ya kusikia, ila hawasikii; kwa maana ni nyumba iliyoasi. EZE. 12:2 SUV

Ukweli usiopingika, wapo watu wengi wanaabudu mahali sio sahihi, wakifikiri wapo sahihi kumbe hawapo sahihi, wakifikiri wanaona kumbe hawaoni, na wakafikiri wanaelewa wanapotazama kumbe hawaelewi.

Viongozi wanaowaogoza ni vipofu, na kipofu hawezi kumwongoza kipofu mwenzake. Maana wote hawaoni, na wakijaribu kuongozana pamoja, mwisho wake watajikuta wametumbukia shimoni au kwenye mitaro ya maji. Na kama wapo eneo la mjini watajikuta wamegongwa na magari/pikipiki/bajaji maana hawaoni.

Watu wengi hufikiri tupo salama pale tunapoona wale tunaowaamini wanatuongoza vizuri, kumbe wanaotuongoza ni vipofu, na sisi tunaongozwa nao ni vipofu.

Biblia ipo wazi kwa hili, japo tunaweza kuisoma bado tusielewe tunachosoma. Japo upo wakati tunaweza kufikiri tunaelewa kile tunachojifunza, kumbe hatuelewi kabisa kutokana na ufahamu wetu kutiwa giza la upotovu.

Rejea: Waacheni; hao ni viongozi vipofu wa vipofu. Na kipofu akimwongoza kipofu mwenzake, watatumbukia shimoni wote wawili. Mathayo 15:14 SUV

Inawezekana hata hapa utasoma na usielewe, maana shetani amekushika moyo wako usiweze kuelewa haya ninayokueleza hapa. Ila ombi langu kwa Mungu uweze kufunguka mahali umefungwa ufahamu wako, mahali umefungwa masikio yako, na mahali umefungwa macho yako.

Ni hatari sana kuwa mahali pasipo sahihi kabisa, watu wanakupigia kelele, watu wanajaribu kukuonyesha mistari mbalimbali ya biblia takatifu. Jinsi unavyoamini vitu visivyo sahihi, jinsi unavyoabudu/unavyosali mahali pasipo sahihi, pamoja na hayo yote bado huelewi wala husikii chochote.

Neema ya Mungu ifungue ufahamu wako, ili uweze kuona na kusikia yale unayopaswa kusikia. Usiwe kama mwanafunzi asiyesikia, si umewahi kukutwa na hali hii ukiwa shuleni? mwalimu anaingia darasani kufundisha lakini anatoka hujamwelewa chochote.

Kumbe wakati anafundisha mawazo yako hayakuwa darasani kabisa, na sio kwamba mwalimu alikuwa anafundisha vitu visivyoeleweka. Hali kama hiyo ndio imewafanya walio wengi wakihubiriwa iliyo kweli ya Mungu hawataki kubadilika. Kwa sababu wana macho ila hawaoni, na wana masikio ila hawasikii.

Kibaya zaidi viongozi wao wanaowaamini ni vipofu, na wao wanaoogozwa nao ni vipofu. Lakini wao wanaona wapo sahihi kabisa, na wanaona Mungu yu pamoja nao, na wanaona wanaongozwa na Roho Mtakatifu.

Mambo ya kusikitisha kidogo ila ukweli ndio huo, na anapotokea mmoja wao akafunguliwa akaanza kusikia na kuona. Anaonekana ameasi imani yao, akijaribu kuwasemesha na kuwaeleza kile anakiona, atakachoambulia ni kuonekana mtu mbaya na kutengwa/kufukuzwa.

Usifurahie sana upo mahali sahihi, wakati mwingine unaweza kuona hivyo kumbe sio kweli upo mahali sahihi. Cha kuzingatia ni kusoma Neno la Mungu kwa bidii zako zote, huku ukimsihi Mungu kupitia Roho wake Mtakatifu akufundishe kuelewa kile unasoma.

Vinginevyo ndugu zangu katika Kristo Yesu, tutakuwa tunafikiri tunasali mahali sahihi, kumbe tunasali mahali ambapo sio sahihi. Hata kama mazingira ya dini zetu au madhehebu yetu yatakuwa yanatuonyesha tupo mahali sahihi.

Mungu akubariki sana kwa muda wako.

Facebook: Chapeo Ya Wokovu

Email: chapeo@chapeotz.com

Blog: www.chapeotz.com

WhatsApp: +255759808081