Nakusalimu katika jina la Bwana wetu Yesu Kristo aliye hai, jambo la kumshukuru Mungu kutupa kibali kingine tena cha kuweza kuiona siku ya leo.
Wakati mwingine tumetumia muda mwingi kujikinga tusipatwe na mabaya, Lakini pamoja na kufanya hivyo, tunajikuta yametupata hayo mabaya.
Hatuwezi kukataa wala kuzuia mabaya juu ya maisha yetu, haijalishi tutajitenge na mambo maovu ya dunia hii. Bado mambo mabaya yanayoumiza mioyo yetu yatatupata tu, hatuwezi kuyakwepa katika maisha yetu.
Wakati mwingine tunajaribu kuukataa au kuukwepa ukweli huu, ila ukweli ni kwamba, hatuwezi kuzuia ubaya wote usitupate katika maisha yetu. Itategemeana na wewe utakutana na jambo gani la kuujeruhi moyo wako, ila litabaki kuwa ni jambo baya kwako.
Unapaswa kujifunza hili ili iwe rahisi kwako kuvuka pale unapokutana na changamoto ngumu za maisha yako. Maana kuna wakati umeokoka lakini unashangaa mambo mabaya yanayoumiza moyo wako, hayaishi kukujia katika maisha yako.
Huenda umeshtushwa kidogo na kichwa cha somo hili, ni vile tu unajaribu kuukataa ukweli. Ila ukweli ni kwamba huwezi kukwepa mambo mabaya katika maisha yako.
Tunaposema mambo mabaya, hatuzungumzii tu kumtenda Mungu dhambi, mambo mabaya ni pamoja na kupatwa na jambo ambalo linaondoa kabisa furaha ya moyo wako.
Unapokutana na kikwazo chochote cha namna hii, cha kukuondoa kwenye furaha yako na kukupa huzuni. Huu ni wakati mzuri kwako wa kujijua kama umekomaa kiroho au bado una uchanga wa kiroho.
Ni wakati mzuri sana wa kujua watu walio pamoja na wewe, huenda ulikuwa unaona unapendwa sana na watu. Kumbe macho yako na akili zako zilikuwa zinakudanganya, ila unapokuwa kwenye wakati mgumu unaouona mbaya kwako. Kumbe ndio wakati mzuri wa kutambua walio upande wako ni wangapi.
Yapo maeneo usipopatwa na mabaya, watu hawawezi kutambua ukuu wa Mungu ulio ndani yako, mabaya mengine yanakujia kwa makusudi maalum kabisa. Ili jina la Yesu litukuzwe katika hayo.
Ukiwa mwoga sana kupatwa na mambo mabaya, wakati mwingine shetani anaweza kutumia udhaifu huo kukuhangaisha sana moyo wako. Maana anajua hujui nafasi uliyonayo mbele za Mungu wako, hii ni kwa sababu umekosa Neno la Mungu ndani ya moyo wako.
Aliyekomaa kiroho anajua kila jambo lina wakati wake, anajua kuna kufurahia sana, na anajua upo wakati wa kuhuzunika sana. Hizi zote ni nyakati alizowekewa mwanadamu katika maisha yake, hakuna furaha ya moja kwa moja wala hakuna huzuni ya maisha yako yote.
Kila jambo lina wakati wake, ukiona leo familia yako ina furaha ya kutosha, weka akiba ndani ya moyo wako, ukiwa unajua upo wakati fulani furaha hiyo itaondoka na kuingia huzuni.
Rejea: Kwa kila jambo kuna majira yake, Na wakati kwa kila kusudi chini ya mbingu. MHU. 3:1 SUV
Haitajalisha umeokoka sana na humtendi Mungu dhambi, hizi ni nyakati zilizowekwa kwa mwanadamu, upo wakati wa kustarehe, vilevile upo wakati wa mateso makali.
Ikiwa ni hivi unapaswa kujipanga ndani ya moyo wako, kujipanga kwako ni kuwekeza maarifa sahihi ya kutosha ndani yako. Maarifa hayo ni Neno la Mungu, linakuwaje Neno la Mungu? Unapaswa kulisoma na kulifakari kila wakati.
Neno la Mungu litakusaidia sana pale utakapokutana na mambo mabaya ya kukuumiza moyo wako, Neno la Mungu linakuandaa kifikra.
Nakuhakikishia mkristo yeyote aliyekomaa vizuri kiroho, hawezi kupata mshtuko mkali kwa sababu ya matatizo yake, hawezi kukubwa na magonjwa yanayosababishwa na msongo wa mawazo.
Ukijiona unashindwa kabisa kukabiliana na mambo mabaya yaliyo mbele yako, usitafute sababu nyingine, wewe jua bado unakabiliwa na uchanga wa kiroho. Haijalishi una miaka mingapi katika wokovu, kama huna muda wa kusoma Neno la Mungu na kulitafakari, ukubali tu wewe ni mchanga wa kiroho.
Mabaya yapo tu, upende usipende, ujue utakutana nayo tu, cha msingi na kujiimarisha vizuri kiroho. Hata unapokutana nayo, iwe rahisi kwako kumruhusu Mungu asimame mwenyewe katika jambo hilo.
Mungu akubariki sana kwa muda wako.
Chapeo Ya Wokovu
Blog: www.chapeotz.com
WhatsApp: +255759808081