Nakusalimu katika jina la Bwana wetu Yesu Kristo aliye hai, ashukuriwe Yesu Kristo kwa kuendelea kutupa kibali kingine tena cha kuweza kuiona siku mpya.

Bila matendo hatuwezi kuthibitisha upendo wetu juu ya kile tunasema tunakipenda, upendo sahihi na wa kweli, unaendana na matendo ya mtu.

Matendo ndio yanathibitisha kuwa huyu mtu anamaanisha kwa kile anakikiri kwenye kinywa chake, pasipo matendo hatuwezi kusema huyu mtu anamaanisha kwa kile anakiri kwa kinywa chake.

Kutamka tu mdomoni bila matendo yeyote yanayoonyesha huyu mtu anachokiongea kinaendana na kile anakizungumza. Hatuwezi kupata ujasiri wa kusema huyu mtu yupo vizuri.

Tunapata ujasiri wa kutamka huyu mtu yupo vizuri kwa sababu tumewahi kuona matendo yake, kutenda kwake kunawafanya wengine wawe na ujasiri wa kumtetea kwa watu wengine wanaotaka kumsema vibaya.

Matendo ya mtu ndio yanatuthibitishia yale yaliyo ndani ya moyo wake, yale anayonena kwenye kinywa chake, bila kuyaona katika matendo ya nje. Bado hatuwezi kusema huyu mtu anamaanisha kwa kile anakitamka mdomoni.

Kile kilicho ndani ya moyo wa mtu, ndicho kinasukumwa nje, kinaposukumwa nje kinakugeuka matendo. Hatuwezi kusema tuna upendo alafu matendo yetu ya nje yanaonyesha kinyume na kile tunakikiri kwa vinywa vyetu.

Wengi sana wanaanza vizuri kusoma Neno la Mungu, wanakuwa na hamu kweli kutoka ndani ya mioyo yao. Ila wanapoanza kuziweka hamu zao katika matendo, wanajikuta wanaishia njiani na kufanya mambo mengine kabisa kinyume na kile wanasema wanakipenda.

Tumeona upendo wa kweli upo katika matendo, ikiwa unasema unapenda Neno la Mungu alafu kwenye matendo haonyeshi kile unakitamka. Bado hatuwezi kuthibitisha upendo wako ni wa namna gani.

Kufanikiwa kwako kusoma Neno la Mungu bila kukwama kwama, sukuma upendo katika matendo. Matendo yako yawe kwenye eneo la mpango usiokwama njiani.

Jikatae mwenyewe pale unapojikuta unasema unapenda Neno la Mungu, alafu husomi kabisa Neno la Mungu. Hakikisha unajikanya mwenyewe, na kujirejesha mwenyewe pale unapoona ulitoka nje ya mstari.

Bila kufanya hivyo utaendelea kujiona unapenda Neno la Mungu, huku huonyeshi chochote kuhusu upendo wako wa Neno la Mungu. Matendo yako ndio yatathibitisha kweli huyu mtu anapenda kusoma Neno la Mungu.

Hatufanyi hivyo kwa maonyesho, ila matendo yetu ndio yanatufanya tuonekane hivyo. Vile tunaishi, na kufanya kila siku yale tunayapenda kuyafanya, yanatutambulisha kwa jamii zetu ni watu namna gani.

Tukiwa watu wa maneno matupu bila matendo, napo watu watatujua kuwa huwa tunaongea tu maneno mengi ila hakuna tunachoweza kukifanya.

Nakuhakikishia unaweza kufanikiwa kwenye eneo hili la usomaji wa Neno la Mungu, ikiwa tu utageuza maneno kuwa matendo. Ukipunguza kuongea sana, na ukafanyia kazi ule upendo wako unaouona ndani yako juu ya Neno la Mungu, utaanza kuona mabadiliko ndani yako.

Vinginevyo ukae kimya, maana unapoendelea kusema unapenda Neno la Mungu alafu husomi, na wala huna muda wa kukaa ukalisoma na kulitafakari. Tunashindwa kukuelewa kabisa, maana hatuoni vitendo vyovyote vinavyotambulisha upendo wako.

Fahamu hata imani yako inahitaji matendo, maana imani bila matendo imekufa. Ikiwa imani bila matendo imekufa, hata upendo bila matendo ni kudanganyana.

Rejea: Maana kama vile mwili pasipo roho umekufa, vivyo hivyo na imani pasipo matendo imekufa. Yakobo 2:26 SUV

Umeona hapo? Hata mwili pasipo roho umekufa, upendo wa maneno matupu pasipo kusoma Neno la Mungu ni kujidanganya. Tunahitaji kuona upendo wa matendo katika kusoma Neno la Mungu.

Mungu akubariki sana kwa muda wako.

Chapeo Ya Wokovu

chapeo@chapeotz.com

www.chapeotz.com

+255759808081