Kuna mahali unaweza kutamani kuingia, ukapewa sifa za mahali pale, sifa zile zikavutia kweli na kuona mahali ulipokuwa unapatafuta patakuwa penyewe. Hii ni kutokana na sifa za mahali pale.

Unaweza kuingia mahali pale, ukakuta sifa ulizopewa na mahali unapopaona, ni tofauti kabisa na sifa zile ulizoambiwa au ulizosikia kwa watu. Hii itakufanya uanze kujiuliza kipi kinawafanya watu wapaone panafaa sana wakati hapafai hata kidogo.

Inaweza kutokana na vile wanaona wao, wanaona wao panafaa sana, mkawa mmetofautiana jinsi ya kutazama mambo. Maana kuna jambo unaweza kuliona zuri kwako, kwa mwingine likaonekana baya kwake. Vivyo hivyo kwa mwingine linaweza kuonekana zuri kwao, kwako likaonekana baya.

Kila mmoja ana jinsi anapendezwa na kitu chake, japo kuna mahali tunafanana vitu vya kupenda, ila si vyote tunaweza kuvipenda kwa kila mtu. Ila tukishakuwa mahali kama watu wenye imani moja, tunakuwa kitu kimoja, maana anayetufanya tuwe kitu kimoja ni Yesu Kristo.

Sifa za mahali huwa zinatufanya tutamani na sisi kufika kujionea, sifa zile zinaweza kuwa sahihi kabisa. Ila wewe ulivyotamani kujionea, ukajikuta sivyo vile ulitafisiri kwenye akili yako, sivyo vile ulipokea hizo sifa za mahali ulipokuwa unapasikia sana kwa watu.

Unapokutana na hali kama hiyo, huwa tunaona hapafai na kupaona sivyo, kesho hata uambiwe na mwingine ni pazuri mahali pale. Utakataa kwa sababu unapaelewa vizuri sana.

Kwanini nasema haya yote, yapo makundi mengi ya whatsApp, ambayo unakutana na sifa zake kuhusu hayo makundi. Ila ukishaingia unakutana na vitu viwili tofauti na vile ulisikia, pia unaweza kukutana na sifa zilezile ulizosikia hadi zikavutia kuingia.

Tunaamini kile tunakisema kwenye kanuni zetu za Chapeo Ya Wokovu katika group la whatsApp, ndizo kanuni tunazosimamia haswa. Hakuna siku imepita bila kusoma Neno la Mungu, vile tumepanga ratiba zetu za kila siku, ndivyo tunavyoenda.

Sasa wengi wakishasikia sifa za group la Chapeo Ya Wokovu, wanakimbilia bila kujitathimini wenyewe kwanza kabla hawajasema niweke na mimi. Wanafikiri wakishafika pale watakuwa watalii tu wa kuangalia wengine wanachofanya bila wao kufanya chochote.

Badala yake wanakutana na hali tofauti na waliyotegemea wao, wanajikuta wanaondoka kimya kimya bila kuaga mtu. Tunaamini kile tunakisema ndicho tunakifanya na tunakisimamia, kuhakikisha kila mtu anahusika na kile tumekubaliana nacho.

Wengi wetu tumejikinai, tunahamasika kwa muda mchache, tunarudi tena kwenye hali zetu zilezile. Tunabaki tunaimba midomoni tunapenda Neno la Mungu, ila kwenye matendo yetu kuonyesha kweli kile tunakizungumza, tunakuwa hatuwezi kuthibitisha kwa matendo.

Chapeo Ya Wokovu whatsApp group, tumehakikisha kila mmoja anasoma Neno la Mungu. Ukishindwa kuendana na kile tumekubaliana nacho, utaondolewa kwenye kundi.

Wengi wanasema niunge, wanakiri kufuata kanuni zetu tulizojiwekea, kwa kufikiri hakuna atakayemwona kama ameshiriki neno. Anapoona tunamaanisha kweli kwa kile tunasema, anakimbia mwenyewe bila kuaga.

Tungekuwa tunadanganya kwa kile tunasema, nisingekuwa na ujasiri wa kusema haya yote. Nalazimika kusema haya kwa sababu wengi wetu tunalipenda Neno la Mungu mdomoni, ila kwenye matendo hatupo kabisa.

Utaendelea hivyo hadi lini? Amua kubadilika, acha kulipukalipuka alafu Kesho tunakuona umerudi kwenye hali yako ya udhaifu. Kama umeamua kweli kusoma Neno la Mungu, amua kutoka moyoni mwako, alafu kubali kujijengea nidhamu katika hilo.

Umeona huwezi kujisimamia kila siku, Chapeo Ya wokovu whatsApp group tumekuwekea utaratibu mzuri wa kukusaidia kukumbusha na kukusukuma usonge mbele. Vizuri pia kuungana na wenzako wenye lengo moja hata kama unaweza kujisimamia mwenyewe.

Kaa kwenye makundi yanayokupa faida, acha kujaza makundi mengi kwenye simu yako yasiyo na faida kwako. Leo unafurahia kuchati vitu vya ajabu ajabu kwenye makundi, utakuja wakati utajutia muda uliopoteza na marafiki wasiofaa.

Nakushauri usingaike kupoteza muda wako kusema uungwe group la Chapeo Ya Wokovu, kama huna nia ya kweli kusoma Neno la Mungu.

Mungu akubariki sana kwa muda wako.

Chapeo Ya Wokovu

Blog: www.chapeotz.com

WhatsApp: +255759808081