Haleluya,

Baada ya kutafakari hili, nimepata maswali mengi ambayo mengine yanaweza kunifanya niendelee kujishangaa mimi mwenyewe.

Neno la Mungu ni halisi, huhitaji kuwa na mashaka kuhusu Neno la Mungu, wala huhitaji kufikiri hizi ni hadithi za zamani zilizoandikwa kuwasaidia wana Israel. Ambazo hadithi hizi haziwezi kutenda kazi sasa hivi.

Tunaposhindwa kulielewa Neno la Mungu na kuanza kutafuta kufuata mambo yetu wenyewe ambayo ni chukizo kwa Mungu wetu, tuwe na uhakika ukristo wetu upo kama kivuli tu. Ila shetani amepenyeza mambo yake mabaya kutufanya tuendelee kumtumikia yeye badala ya Mungu wetu.

Inawezekana vipi leo hii mtu anayejiita mkristo, anaenda kutafuta msaada kwa wenye pepo na wachawi. Watu ambao nguvu yao huwezi kuifananisha na nguvu ya Mungu aliye hai.

Jana katika sehemu ya 337 tulijifunza pale unapopita kwenye changamoto ngumu, unaweza kushauriwa ushauri mbaya. Usipokuwa na chujio la kuchuja ushauri mbaya na mzuri, utajikuta umemkosea Mungu wako.

SOMA:SOMA NENO UKUE KIROHO 337; Kipi Kinachokusaidia Kuchuja Maneno Ya Wanaokushauri Juu Ya Changamoto Ngumu Iliyokupata.

Kama hukupata nafasi ya kusoma ujumbe wa jana, fungua maandishi hayo ya blue kujifunza zaidi. Utajifunza mengi na utanielewa vizuri kuhusu hili ninalokueleza hapa.

Kama wakristo hatupaswi kwenda kutafuta msaada kwa waliokufa, wafu ambao hawasemi chochote. Alafu sisi tulio hai tunaona wanaweza kutusaidia, tunaacha kumwendea Mungu, tunawaendea waliokufa/wafu.

Jambo la kushangaza kidogo kwa mtu aliyefunguliwa macho yake ya rohoni, jambo la kushangaza sana kwa mtu anayesoma Neno la Mungu. Mtu aliye na maarifa sahihi ya Neno la Mungu hawezi kuacha kushangaa hili.

Lazima ajiulize inawezekana vipi mtu kwenda kutafuta msaada kwa waliokufa, wengine wanaomba mizimu ya mababu zao waliokufa iwasaidie katika mambo yao. Haitoshi hapo tu, wanatoa na sadaka ya damu ya mnyama.

Ikiwa unasoma ujumbe huu, na unaendaga kutafuta msaada kwa watu wenye pepo wa utambuzi, na wachawi wanaokusemesha mambo ya ajabu ajabu. Unapaswa kufahamu unayoyafanya ni chukizo kwa Mungu wako.

Aliyekufa hawezi kukusaidia wewe, hata kama alikuwa mcha Mungu mzuri sana, hata kama Mungu alikuwa anamtumia sana katika uhai wake. Akishakufa na habari yake imeishia hapo, sio mimi ninayesema haya, ni maandiko matakatifu yanasema.

Usidanganyike na mtu yeyote yule kuhusu kwenda kwa waliokufa kwa maombi, wala usiwe na imani kwamba watakusaidia shida yako. Ndio maana Yesu Kristo alikufa na kufufuka, vinginevyo tusingekuwa na ujasiri wa kusema tunaye Mungu aliye hai.

Rejea: Na wakati watakapokuambia, Tafuta habari kwa watu wenye pepo na kwa wachawi; waliao kama ndege na kunongona; je! Haiwapasi watu kutafuta habari kwa Mungu wao? Je! Waende kwa watu waliokufa kwa ajili ya watu walio hai? ISA. 8:19 SUV

Ukisoma mstari huo kwa makini, unaona kuna maswali mawili ya muhimu sana kwako, la kwanza linasema hivi;je! Haiwapasi watu kutafuta habari kwa Mungu wao?Ni sawa na kuulizwa hivi; je! Hupaswi kutafuta msaada kwa Mungu wako hadi uende kwa watu waliokufa?

Ambapo ukisoma mstari huohuo unakutana na hili swali tena la pili, linauliza hivi;Je! Waende kwa watu waliokufa kwa ajili ya watu walio hai?

Nadhani hadi hapo umeelewa kwanini hupaswi kwenda kwa wenye pepo, na wachawi, na watu waliokufa. Unapaswa kumwendea Mungu wako, hupaswi kuchanganya Mungu wa kweli na miungu mingine.

Unaweza kuamini hayo yaliyo kinyume na Mungu, na ukapata msaada, ila uwe na uhakika jehanamu inakuhusu kama hutotubu na kuacha.

Mungu akubariki sana kwa muda wako.

Chapeo Ya Wokovu

WhatsApp: +255759808081