Nakusalimu katika jina la Bwana wetu Yesu Kristo aliye hai, bila shaka unaendelea na mpango wako wa kusoma Neno la Mungu. Na kama uliacha mpango huu ni nafasi kwako kurudi tena kuliko kuacha kabisa.

Rahisi sana kujishawishi na kujipa moyo ukaona uache kwanza kusoma Neno la Mungu kutokana na mazingira magumu na Nyakati ngumu unazopitia wakati huo.

Kuacha kwako kusoma Neno la Mungu kwa kisingizio cha kumpumzika kwanza, kwa muda usiojulikana hadi pale utakapokuwa sawa. Inaweza ikawa ndio tiketi yako ya kuondoka moja kwa moja kwenye mpango wako wa kusoma Neno la Mungu.

Mwanzoni unaweza kuona utarudi siku fulani, utashangaa siku hiyo inafika na bado mambo hayajakaa sawa. Tena changamoto zinaweza zikawa zimeongezeka zaidi ya mwanzo, wakati zinaendelea kupandana hizo changamoto, na huku wewe unazidi kupoa.

Unapopoa unaanza kuona uvivu kurudi tena kwenye ratiba yako ya kusoma Neno la Mungu, hapo ndio inabaki unatamani moyoni mwako kusoma Neno la Mungu. Lakini huwezi kuchukua hatua zozote za kufanya hivyo, na ukijaribu kujikaza kidogo unaona kuna kitu kinakuvuta nyuma.

Usikubali kuzimisha moto uliowaka ndani yako, bali endelea kuchochea moto zaidi ya jana, bidii yako isiondolewe na changamoto ngumu za maisha yetu ya kila siku.

Kila kukicha utakutana na changamoto tofauti kabisa na ya jana, tena ukiwa unazisubiria ziishe, badala ya kuisha kwanza zitazidi kuongezeka mpya kila siku.

Bora kukosa nafasi kwa sababu maalum ambayo usingeweza kuizuia kuliko kujipumzisha hadi upite changamoto unayopitia wakati huo. Huko ni kujiondoa kabisa kwenye mpango wako wa kusoma Neno la Mungu.

Usifikiri nakueleza hadithi fulani, wengi sana waliojaribu kupumzika wakati wanapitia changamoto, walipotelea huko moja kwa moja. Hadi leo wanaimba wimbo usio na mwisho “nilikuwaga nasoma sana Biblia” lakini hawajawahi kurudi tena waendelee na ratiba yao.

Neno la Mungu linasema, moto wa madhabahu utatunzwa siku zote usije ukazimika. Maana ipo shida kuacha moto uzimike madhahuni;

Rejea: Moto utatunzwa uwake juu ya madhabahu daima; usizimike.Walawi 6:13 SUV

Ikiwa moto wa madhabahu utatunzwa daima usizimike, je! wewe unakubalije haraka changamoto kukufanya upoe kiroho chako?

Moto wa Roho Mtakatifu uendelee kuwaka ndani yako bila kuzimisha moto huo, changamoto unazopitia zisije zikakufanya ukapooza kiasi kwamba ukaona uache kwanza kusoma Neno la Mungu.

Utamruhusu shetani akushikilie huko huko kwenye kupumzika kwako, badala yake itabaki historia nzuri uliwahi kusoma Neno la Mungu. Wakati huo umepoa na haupo tena kwenye mpango wako wa kusoma Neno la Mungu kila siku.

Binafsi nimeshakataa jambo lolote kuniondoa kwenye mpango nilioanzisha katika maisha yangu ya wokovu, nimeamua kusoma Neno la Mungu maisha yangu yote hapa duniani. Sitegemei kuacha hili jambo mpaka naondoka hapa duniani.

Sijui wewe unayesema kila siku utaanza kusoma Neno la Mungu, ukianza siku moja ya pili unaacha, unaanza kuimba tena wimbo wako wa nitaanza kesho, mara kesho kutwa, mara wiki ijayo, mara mwezi ujao, hadi unamaliza mwaka bado unaimba wimbo ule ule.

Amua kubadilika kuanzia leo, ukijua Neno la Mungu ni muhimu sana kwako, pasipo Neno la Mungu utamtenda Mungu dhambi sana, utadanganywa sana, utashindwa kusamehe, utashindwa kushuhudia matendo makuu ya Mungu mbele ya wasiomjua, na mengine mengi.

Mungu akubariki sana kwa muda wako.

Chapeo Ya Wokovu

www.chapeotz.com

+255759808081